Mmoja aliyeshtakiwa kwa mauaji aachiwa, mwenzake ang’ang’aniwa

Sumbawanga. Mahakama Kuu, Masijala Ndogo ya Sumbawanga, imemkuta Budagala Shija, mkazi wa Wilaya ya Tanganyika, na kesi ya kujibu, huku ikimuachia huru mtuhumiwa mwenzake, Nyalu Salu, waliokuwa wakishtakiwa kwa kesi ya mauaji.

Budagala na Nyalu walikuwa wakikabiliwa na shtaka la mauaji kinyume na vifungu vya 196 na 197 vya Kanuni ya Adhabu, wakidaiwa kumuua Ramadhan Hamis Februari 5, 2022, katika Kijiji cha Bungwe, Wilaya ya Tanganyika, Mkoa wa Katavi, kwa kumchapa viboko 15 sehemu mbalimbali za mwili wake, ikiwamo kichwani.

Baada ya upande wa mashtaka kufunga ushahidi wake, mahakama ilibaini kuwa Budagala ana kesi ya kujibu, huku ikiona kuwa ushahidi haujamuunganisha Nyalu na kosa hilo, hivyo hakuwa na kesi ya kujibu.

Uamuzi huo umetolewa Februari 20, 2025, na Jaji Abubakar Mrisha. Katika nakala ya uamuzi huo inayopatikana kwenye mtandao wa mahakama, Jaji Mrisha alieleza kuwa baada ya kutathmini ushahidi wa mashtaka, mahakama imeona kuwa Budagala ana kesi ya kujibu kwa mujibu wa Kifungu cha 230 cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA).

“Hata hivyo, sijashawishika hata kidogo kuwa upande wa mashtaka umefanikiwa kufungua kesi dhidi ya Nyalu, ambaye ushahidi haujamtia hatiani kwa njia yoyote ile. Naamuru Nyalu aachiliwe,” amesema Jaji Mrisha.

Awali, katika kesi hiyo, upande wa mashtaka uliwasilisha mashahidi sita pamoja na vielelezo viwili, vikiwemo maelezo ya onyo ya washtakiwa na ripoti ya uchunguzi wa mwili wa marehemu.

Jaji alisema kuwa kutokana na ushahidi uliotolewa, mambo matatu muhimu yanapaswa kuzingatiwa. Kwanza, upande wa mashtaka umeonyesha kuwa kabla ya kifo chake, marehemu alikamatwa na kundi la walinzi Februari 2, 2022, alipokuwa akionyesha michezo ya video katika duka la kaka yake.

Ilidaiwa kuwa watuhumiwa walifika kwenye eneo hilo na kuamuru watu wote wa kabila la Wasukuma kutoka nje. Marehemu alipoanza kutoka, alikamatwa na kupewa adhabu kwa kuchapwa viboko 15 sehemu mbalimbali za mwili wake, ikiwemo kichwani.

Ushahidi wa mashahidi unaonyesha kuwa mshtakiwa wa kwanza, Budagala, alihusika moja kwa moja katika tukio hilo na anashtakiwa kwa kuwa mmoja wa waliomshambulia marehemu.

“Hata hivyo, ushahidi wa upande wa mashtaka haujaonyesha ikiwa mshtakiwa wa pili, Nyalu, alikuwepo eneo la tukio au alihusika kwa namna yoyote katika mauaji hayo,” amesema Jaji.

Jaji Mrisha aliongeza kuwa, kwa mujibu wa ushahidi wa shahidi wa tano, ambaye ni daktari aliyefanya uchunguzi wa mwili wa marehemu baada ya kutambuliwa na ndugu, chanzo cha kifo kilitokana na majeraha ya ubongo.

“Kutokana na ushahidi na tathmini hiyo, ni hitimisho langu kuwa upande wa mashtaka umefungua kesi dhidi ya Budagala, ambaye ana kesi ya kujibu,” ameongeza Jaji.

Related Posts