Dar es Salaam. Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Amana imekabidhiwa hati ya umiliki ardhi wa eneo la hospitali hiyo lenye ukubwa wa kilomita za mraba 26,642 ikiwa ni miaka 70 tangu kuanzishwa kwake 1954.
Kwa kipindi chote hospitali hiyo iliyoanza kutoa huduma ya mama na mtoto kama zahanati kabla ya Uhuru na baadaye Hospitali ya Manispaa kabla ya kuwa ya rufaa mwaka 2018, haikuwa na hatimiliki.
Hati hiyo imekabidhiwa leo Alhamisi, Mei 16, 2024 na Katibu Mkuu, Wizara ya Afya, Dk John Jingu kwa Mganga Mfawidhi wa Amana, Dk Bryceson Kiwelu.
Dk Jingu ameitaka hospitali hiyo kuanza mipango ya ujenzi wa kuitanua kwa kufuata ujenzi wa majengo ya juu ili kutatua changamoto za ufinyu wa eneo.
“Mlikuwa mnakaa kienyeji. Tunajua eneo mlilonalo hapa si kubwa, tunahitaji mipango mizuri na matumizi bora ya ardhi yetu, inabidi itumike kwa ujenzi wa majengo ya kwenda juu. Miundombinu imesambaa, lakini kutokana na eneo tulilonalo sasa tuna uhakika kwamba tutajenga majengo ya kusimama wima,” amesema.
Sababu kukosekana hatimiliki
Dk Kiwelu amesema kuchelewa kupata hatimiliki, kulitokana na kuhamishwa mara kwa mara kwa watendaji wakuu kutoka ofisi ya mwanasheria, wizarani na makatibu wakuu.
“Leo ndiyo tumekabidhiwa hati, haya yalikuwa maeneo ya Serikali kwa miaka hiyo yote, yalipimwa lakini hati ilikuwa haijapatikana. Hili siyo eneo pekee lililokuwa na changamoto hii, kuna maeneo mengi hayana hati, tumekuwa tukifuatilia kwa muda mrefu zaidi ya miaka mitano lakini kutokana na mabadiliko na taratibu za ardhi anayetakiwa kusaini hati ni Katibu Mkuu Wizara ya Afya,” amesema.
Dk Kiwelu amesema saini inatakiwa kuwekwa na Katibu Mkuu na mwanasheria, wote wawepo pamoja.
“Awali tulipeleka majina ya katibu mkuu aliyekuwepo, mwanasheria mkuu aliyekuwepo, kabla hawajasaini wakahamishwa, tukaandaa nyingine ya Profesa Abel Makubi akabadilishwa kabla hawajasaini,” amesema.
“Kwa sasa tumefanikiwa hati kusainiwa japo eneo la NHC ambalo tumeliomba bado hatujakabidhiwa, lakini endapo tutapata hati ya eneo hilo tutaenda kufanya mabadiliko ya hati ya kuongeza eneo,” amesema Dk Kiwelu.
Amesema kulikuwa na changamoto ya hoja ya ukaguzi kwa miaka mingi kuhusu eneo hilo kwamba mtu anaweza kudai ni lake, na kama huna hati huwezi kusema unalimiliki.
“Hivyo tumefuta hoja hii ya ukaguzi,” amesema.
Dk Jingu pia amekagua huduma za afya ndani ya hospitali hiyo na utekelezaji wa miradi inayoendelea, huku akizungumzia tiba mtandao itakayoanza hivi karibuni katika hospitali hiyo na nchini kwa ujumla.
“Badala ya mtu kuamka asubuhi kuja kujipanga hapa, tutumie mfumo wa Tehama kufanya miadi na wataalamu wa afya, kwa anayetaka kuja kumuona daktari itapunguza kupoteza muda hospitalini kama amepangiwa saa tano atafika muda huo, hiyo itasaidia kuboresha ubora wa huduma,” amesema.
“Tiba mtandao si tu kwa wale wenye simu janja pekee, bali pia kuna namba zitakuwepo za kupiga hospitali husika na kutoa miadi ya kuonana na daktari unayemtaka, bila kujali unatokea wapi,” amesema.
Yusuph Migomba, mgonjwa aliyefika kwa matibabu katika hospitali hiyo amesema: “Changamoto tunazokumbana nazo hapa ni foleni ya wagonjwa, nimetuma mtoto tangu asubuhi anishikie nafasi ili niwahi kupata huduma lakini mpaka nafika hapa hakuna huduma niliyoipata mpaka sasa,” amesema.
Akipokea maoni hayo, Dk Jingu ameeleza katika kuimarisha huduma za afya, tiba mtandao itasaidia kupunguza foleni na kumwezesha mgonjwa kuweka miadi na kufika muda aliopangiwa kuonana na daktari na siyo kupanga foleni.
“Tuna vifaa vya kisasa vya kutoa huduma, tumewekeza katika vifaa ambavyo vinamwezesha mhudumu kutoa huduma kwa wakati. Tunawashukuru watoa huduma za afya hasa hapa Amana, wanafanya jitihada nyingi kuhakikisha wanaenda na wakati katika kutoa tiba,” amesema Dk Jingu.
Imeandikwa na Glorian Sulle