Mabadiliko ya mtindo wa maisha yamvuta Dk Biteko kuhamasisha afya bora

Moshi. Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko, amewataka Watanzania kuishi maisha yanayofuata misingi ya afya bora na kuzingatia mazoezi ya mara kwa mara ili kuepuka magonjwa yasiyoambukiza.

Amesema imekuwa ni desturi ya watu kufanya mazoezi kisha kula vyakula visivyo na ubora, hali inayoongeza tatizo badala ya kulimaliza.

Dk Biteko amesema hayo leo Jumapili, Februari 23, 2024, alipozungumza mjini Moshi na wanariadha kutoka maeneo mbalimbali ya ndani na nje ya nchi.

“Naendelea kuwahimiza Watanzania kuendelea kuishi maisha yanayofuata misingi ya afya bora kama kuendelea kufanya mazoezi kwa wakati wote,” amesema Dk Biteko.

Pia ameongeza, “Watanzania tuwe na utaratibu wa kufanya mazoezi na iwe ni tabia ya kudumu miongoni mwetu na kujiepusha na maradhi mbalimbali hasa magonjwa yasiyoambukiza.”

Amesema ulaji unaozingatia mlo kamili unasaidia kujenga mwili na kuulinda na maradhi mbalimbali.

“Niombe pia mzingatie ulaji unaozingatia afya bora wakati wote unapokula, tuzingatie uwepo wa mlo kamili katika ulaji wetu, ili tuweze kuimarisha afya zetu.

“Leo tumekimbia, tumechoma mafuta mengi sana, itashangaza tena jioni turudi kwenye ule mlima wa ugali, itakuwa kile ulichokichoma umekirudishia siku hiyo hiyo,” amesema.

Pamoja na mambo mengine, amewataka Watanzania kutumia michezo kama kichocheo cha kudumisha amani na upendo miongoni mwao.

“Mashindano haya yawe kichocheo cha kudumisha amani na upendo miongoni mwa Watanzania, kutuweka pamoja kama nchi moja na kamwe isiwe eneo pekee la kuwafanya watu kuangaliana kwa namna wanakotokea ama utaifa wao,” amesema Dk Biteko.

Akizungumza, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Profesa Palamagamba Kabudi, amesema wizara hiyo itaendelea kushirikiana na wadau kuweka mazingira mazuri kwa vijana wa Kitanzania kushiriki shughuli mbalimbali za michezo ili kujiandaa vyema kushindana kimataifa.

 Amesema katika kutimiza azma hiyo, wizara inajenga viwanja vya kisasa vya mipira ya miguu Jijini Arusha na Dodoma, ambavyo pia vitakuwa na miundombinu ya michezo ya riadha.

“Viwanja hivi vitawapa fursa wanariadha wa Kitanzania kujinoa na kufanya mazoezi ya kutosha ili waweze kushindana kimataifa, lakini programu hiyo pia itachochea uibuaji na ustadi wa vipaji vya mchezo wa riadha hapa nchini,” amesema Profesa Kabudi.

Related Posts