Doyo avipa ramani vyama vinavyohitaji muungano

Dar es Salaam. Katibu Mkuu wa Chama cha National League for Democracy (NLD) Doyo Hassan Doyo amesema kama vyama vitahitaji muungano ni lazima vipiganie kwanza mabadiliko ya Sheria ya Vyama vya Siasa ili kama wataungana kila chama kipate haki yake baada ya uchaguzi.

Doyo amesema hayo wakati akimkaribisha mwenyekiti wa NLD kufungua mkutano wa kamati kuu ya chama hicho iliyoketi leo Jumapili Februari 23, 2025 jijini Dar es Salaam.

Kiongozi huyo amesema suala la muungano wa vyama vya siasa wao ni waathirika huku akidai uchaguzi wa 2015 waliungana kupitia Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), lakini maeneo waliyokubaliana NLD itaweka wagombea, yaliingiliwa.

“Mwaka 2015 tuliingia ushirikiano na Chama cha Wananchi (CUF) Chadema na NCCR Mageuzi lakini jambo la kusikitisha katika ushirikiano huo, chama chetu kilidhulumiwa vya kutosha maeneo ambayo tulikubaliana tusimamishe wagombea vyama hivyo vilikuja kuweka wagombea,hivyo mtu anapokuja na hoja sasa kwamba tushirikiane kuikabili CCM kwenye uchaguzi mkuu tunamuona adui,” amesema.

Doyo amesema hawaafiki msimamo huo  kutokana na wao kutonufaika na muunganiko wowote wa vyama vya siasa wanapoungana kuikabili CCM.

Kiongozi huyo wa NLD amesema kila chama cha siasa kina malengo yake hasa kukamata dola na masilahi mengine wanayopata ni kupata ruzuku na wabunge wa viti maalumu kulingana na idadi ya kura watakazopigiwa wakati wa uchaguzi.

“Mfano ukifikisha kura asilimia tano kwenye uchaguzi mkuu unapata wabunge wa viti maalumu kuanzia 0 hadi 10, ukipata kura za urais kuanzia asilimia 5 unapata ruzuku kuanzia Sh100 milioni, sasa unaposalimisha chama chako kwenda chama kingine kwa nafasi ya urais ambaye ndiye anayetambulika kubeba haki zote hizo maana yake hampati haki hizo”amesema.

Kuhusu msimamo wa Chadema wa ‘No Reform No Election’  Doyo amesema hiyo ni ajenda ya Chadema na sio ya Watanzania.

Doyo amesema kama Chadema inaendelea na msimamo huo ina maana wana njia nyingine wanataka kutumia kuleta mageuzi.

Msimamo huo wa NLD unakuja wakati ambao Chama cha ACT Wazalendo kupitia kwa kiongozi wa chama hicho Dorothy Semu aliyetangaza kuwa, chama hicho kina jukumu la kusukuma ajenda ya kuwa na muungano wa vyama makini kuelekea uchaguzi mkuu.

Februari 18 mwaka huu Chama cha NCCR Mageuzi kilisema hakiko tayari kuungana na chama chochote kwenye uchaguzi mkuu ujao ambao kimethibitisha kitashiriki kikamilifu.

Pia, Februari 19, 2025 CUF ilisema hatima ya mpango wa kuunda muungano mseto wa kushirikiana na vyama vingine vya upinzani kukikabili CCM, katika uchaguzi mkuu.

Related Posts