Dar es Salaam. Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango amesema Serikali inatambua thamani ya utumishi wa Askofu Mkuu wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Jude Thaddaeus Ruwa’ichi katika kipindi cha miaka 25 alichotumikia utume wake nchini.
Akizungumza leo Mei 16, 2024 akimwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan kwenye adhimisho la misa ya jubilei ya miaka 25 ya uaskofu wa Ruwa’ichi katika Parokia ya Bikira Maria wa Fatima, Msimbazi Centre, Dar es Salaam, Dk Mpango ametaja mchango wake ambao ni faida kwa Taifa.
Amesema jambo kubwa ni kushukuru ndiyo maana hata Serikali inashukuru kwa matunda ya kazi yake ya uaskofu katika sehemu zote alizohudumu kwa kuacha alama nzuri na kubwa nchini.
“Mchango wako tunafahamu na tunashukuru kwa mfano katika kuanzisha Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agustino (SAUT) Mwanza. Hata vyuo vishiriki vya Mtwara, Songea na Moshi,” amesema.
“Hata hapa Dar es Salaam umeongeza parokia nyingi nadhani takribani 100, pia wana Dar es Salaam wamehamasika kuanza ujenzi wa Kanisa Kuu la Maria Mtakatifu Mama wa Mungu kule Gezaulole chini ya uongozi wako,” amesema Dk Mpango.
Amesema Rais Samia amemzawadia Sh10 milioni Askofu Ruwa’ichi kwa kutambua mchango wake kwa kanisa na Taifa kupitia huduma na uongozi wake.
Dk Mpango na familia yake wamemzawadia monstrance (chombo maalumu kinachotumika kuwekea Ekaristi Takatifu wakati wa Baraka ya Sakramenti Kuu).
Dk Mpango amekumbusha kushukuru kwa kusema asante kwa kila jambo, akisema kushukuru ni kumcha Mungu kama Biblia Takatifu inavyoelekeza.
Ametoa mfano wa wenye ukoma 10 ambao alirudi mmoja pekee kushukuru.
“Napenda kuwaambia Watanzania wote tushukuru kwa kujaliwa amani na kuishi kwa ushirkiano bila kujali dini wala rangi. Tunao wajibu wa kumshukuru Mungu kwa kutupatia nchi nzuri ya Tanzania,” amesema.
Amesema Mungu anawapatia wanadamu baraka ya uhai, afya, furaha na hewa safi hivyo milango ya riziki inafunguka pale mtu anaposhukuru.
Dk Mpango amesema mtoa shukurani anatambua mchango wa kutendewa mema na Mungu.
“Tunapomshukuru Mungu hata katika tukio hili tunaposhukuru kuhusu Askofu Je, na sisi tujiulize tunawashukuru wenzetu? Wanaotupikia chakula, tunaowatuma, wazazi waliotuzaa, marafiki, wafanyakazi wenzetu na majirani, tunakumbuka kuwaambia asante?” amehoji.
“Kwa maswali haya tujitafakari kuwa tuwe tunashukuru. Kama Watanzania tunawajibu wa kushukuru Mungu kwa neema anazotupatia kwa kusali,” amesema.
Dk Mpango amesisitiza utunzaji wa mazingira kwa kuyathamini, akielekeza kutokata miti, kutoharibu vyanzo vya maji, uchafuzi wa mazingira ya mito na bahari ili kuitunza Tanzania.
Kiongozi Mkuu wa Kanisa Katoliki, Papa Francis kupitia Balozi wake Tanzania, Askofu Mkuu Angelo Accattino ambaye ni Balozi wa Vatican nchini, ametoa baraka na pongezi nyingi kwa Askofu Mkuu Ruwa’ichi kwa utumishi wake wa muda wote.
Askofu Mkuu wa Jimbo la Nairobi amesema wamefurahi juu ya utumishi wake, akituma salamu kutoka Kenya akisema wanamtakia kila la kheri.