Mabrouk alitoa kauli hiyo akimwakilisha Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, katika mbio za Samia Marathon, zilizofanyika katika viwanja vya Shule ya Msingi Mtongani, Mlandizi, Kibaha Vijijini.
Alisema Rais Samia amekuwa mfano wa uchapakazi na maendeleo katika nchi, hivyo aliwataka Watanzania kumuunga mkono ili kuleta mafanikio zaidi.
Kauli mbiu ya mbio hizo ilikuwa ni kuhamasisha wananchi kujitokeza kupiga kura katika uchaguzi mkuu Oktoba mwaka huu ambapo Mabrouk alikumbusha kuwa ingawa wengi hujiandikisha, bado kuna changamoto ya kushindwa kujitokeza kupiga kura.
Aliwataka wananchi kuwa sehemu ya mchakato wa uchaguzi kwa haki na kwa wingi.
Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa kupitia Wazazi mkoani Pwani Hamoud Jumaa, alisisitiza umoja na mshikamano kuelekea uchaguzi mkuu.
Jumaa alisema umoja ndani ya chama utaleta ushindi kwa CCM na alisisitiza kuwa amani na utulivu vinahitajika ili kudumisha mafanikio ya taifa.
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi Mkoa wa Pwani, Josian Kituka, aliwashukuru wadau wote waliofanikisha mbio za Samia Marathon, na kueleza lengo kuu la mbio hizo ni kuhamasisha wananchi kujitokeza kupiga kura.
Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Abubakar Kunenge, alieleza mafanikio makubwa yamepatikana chini ya uongozi wa Rais Samia ambapo kwenye nishati ya umeme vijijini imefikia asilimia 98, katika sekta ya elimu shule mpya za msingi na sekondari, mabweni yamejengwa,ukarabati wa maboma, na katika sekta ya maji, upatikanaji umefikia asilimia 83.