Wanne mbaroni wakidaiwa kuua, kudumbukiza mwili kwenye shimo la choo

Kyerwa. Jeshi la Polisi Mkoa wa Kagera linawashikilia watu wanne kati ya saba wakiwamo wanafamilia wa Kijiji cha Kishanda Kata Kibare wilayani Kyerwa kwa tuhuma za mauaji ya Francis Butoto (70).

Miongoni mwa wanaoshikiliwa ni Flora Francis aliyekuwa mke wa marehemu na Denis Mzola, mtoto wa Flora na ndugu zake Kajungu Bitakara na George Bitakara wanaotuhumiwa kumuua kwa kumnyonga Francis na mwili wake kudumbukiza kwenye shimo choo.

Baada ya tukio hilo kutokea, inadaiwa wanakijiji wa eneo hilo walijichukulia sheria mkononi kwa kuharibu mali za wanafamilia hao, ikiwamo kukatakata migomba na kuharibu nyumba.

Leo Jumapili, Februari 23, 2025, Kamanda wa Polisi Mkoa Kagera, Brasius Chatanda amesema tukio hilo la mauaji linadaiwa kutokea Februari 16, 2025 na wanawashikilia watu wanne na wengine watatu wanaendelea kuwasaka.

Baadhi ya mali zilizoharibiwa na wananchi wenye hasira kali kutokana na mauaji ya Francis Butoto (70).

Amesema Flora akishilikiana na watoto na ndugu zake wanahusishwa na tukio hilo.

 Amesema tayari polisi wanawashikilia watu wanne kituo cha Polisi Kyerwa na wengine watatu wanahusishwa na mauaji ya hayo ya kumnyonga baba wa familia hiyo na kudumbukiza chooni wakiamini hataonekana.

“Mwili wa marehemu bahati mbaya siku kadhaa ukanyanyuka juu na chanzo cha unyama huo kimebainika kuwa ugomvi wa familia na mgogoro wa matumizi ya shamba na mali zake ambazo alikuwa hawashilikishi wanafamilia,” amedai Kamanda Chatanda.

Lenatus Francis ambaye ni mtoto wa marehemu, amedai kuwa ugomvi wa mama wa kambo na baba yake umekuwepo kwa kipindi kirefu na kusababisha yeye na wadogo zake wawili wa kike wakahama nyumbani hapo.

Amesema baba yao alipotea tangu Februali 16, 2025 na alipopata taarifa hizo kutoka kwa majirani aliamua kutoa taarifa kwa mwenyekiti wa kijiji kisha wakaanza kumtafuta na jana Jumamosi Februari 22, 2025 mwili wake umekutwa umedumbukizwa ndani ya choo kilichokuwa kinatumiwa na familia.

Muonekano wa mashamba yaliyofyekwa na wananchi na mali zilizoharibiwa yakiwemo magari, nyumba na pikipiki

Mwenyekiti wa kijaji cha Kishanda, Nshekanabo Thomas amesema hilo ni tukio la pili kutokea la kwanza lilitokea Januari 2025 la mwanamke kuamua kudaiwa kumuua mume wake kisa wivu wa mapenzi eneo la Kitongoji cha Rwanjali.

Nshekanabo amesema baada ya tukio hilo wananchi walichoma mali za marehemu yakiwamo magari, mashamba na nyumba jambo liloleta taharuki.

“Naomba Jeshi la Polisi kulingana na mfululizo wa matukio haya kwenye eneo langu basi waweke kambi na elimu ili kunusuru watu wengine wenye fikra mbovu kama hizi,” amesema Nshekanabo.

Related Posts