Dar es Salaam. Madereva wa malori kutoka nchi nne wamedai kuvamiwa na watu waliovalia sare za kijeshi walipokuwa wakisubiri kuvuka mpaka kati ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na Zambia, katika eneo la Kasumbalesa, Lubumbashi.
Uvamizi huo umetokea usiku wa kuamkia jana Jumapili, Februari 23, 2025 takriban kilometa 10 kabla ya kufika mpakani, huku malori yakiwa yamesimama kwenye foleni ya kuvuka mpaka.
Akizungumza na Mwananchi kupitia ujumbe mfupi wa simu, Balozi wa Tanzania nchini DRC, Said Mshana, amesema bado hajapokea taarifa rasmi kutoka kwa madereva au viongozi wao lakini anaendelea kufuatilia suala hilo.
“Nafuatilia, sijapata taarifa yoyote kutoka kwa viongozi wao wala dereva yeyote,” amesema Balozi Mshana.
Juma Mohamed, mmoja wa madereva waliokuwepo eneo la tukio, ameiambia Mwananchi kuwa wavamizi hao waliwataka madereva wawape fedha na chakula.
“Hapa jirani kuna mlima ambao unasemekana kuwa kambi ya jeshi. Walikuja wakiwa wamevalia sare za kijeshi, wakatoa amri ya kupewa chakula, pesa na simu. Dereva aliyekataa alishambuliwa na vioo vya magari vilivunjwa. Walioathirika zaidi ni madereva kutoka Tanzania na Zambia,” amesema Juma.
Kwa sababu ya foleni ndefu katika mpaka huo, madereva wamelazimika kuegesha magari yao hadi maeneo ya porini, kwa sababu mpaka huo hufungwa saa 12 jioni na kufunguliwa saa moja asubuhi kwa saa za DRC.
Juma amesema madereva waliovamiwa walikuwa wanasafirisha mizigo kutoka DRC baada ya kushusha mizigo yao ya awali. Malori yaliyoshambuliwa yalitokea Tanzania, Zambia, Zimbabwe na Afrika Kusini.
“Lakini ilipofika saa 5 asubuhi, magari yalianza kuruhusiwa kupita ingawa msongamano ulisababishwa na vurugu za usiku huo,” amesema dereva huyo.
Dereva mwingine, aliyejitambulisha kwa namba ya D1186, amesema kupitia mawasiliano na viongozi wa madereva, wavamizi walikuwa na silaha na walifyatua risasi kiholela.
“Tumepata uvamizi hapa. Madereva wote tulilazimika kukimbia. Walikuwa wakifyatua risasi ovyo na kupora mali zetu. Wakimkuta dereva kwenye gari, walimchukulia kila kitu,” amesema.
Kwa kuhofia usalama wao, amesema baadhi ya madereva walikimbilia msituni, “lakini waliporudi, walikuta vioo vya magari yao vimevunjwa. Wengi walikimbilia tena msituni kwa kuhofia wavamizi hao kurudi tena.”
Amesema kutokana na taharuki iliyokuwapo, baadhi ya magari yaligongana, kwa sababu madereva hawakuelewa hali halisi ya usalama na kama waliovamia walikuwa wanajeshi halisi au watu waliovaa sare zao.
Mwenyekiti wa Chama cha Wamiliki wa Malori ya Kati na Madogo Tanzania (Tamstoa), Chuki Shabani amesema matukio ya uvamizi kwa madereva Congo si jambo geni.
“Uvamizi kwa madereva nchini Congo ni jambo la kawaida. Wavamizi hawa hufika na kupora kila wanachokiona. Hawa si sawa na M23, kwani mara nyingi hawawaumizi Watanzania, lakini wale wanaoshambulia maeneo ya mpakani ni wakatili zaidi. Tumelalamika serikalini kuhusu suala hili kwa muda mrefu, kwani tunapoteza ndugu na mali,” amesema Shabani.
Ameongeza kuwa, endapo ingekuwa uamuzi wao, wangeepuka na safari za kuingia DRC kwa sababu ya ukosefu wa usalama.
Mmoja wa maofisa waliopo DRC, ambaye hakutaka kutajwa jina amesema huenda waliofanya uvamizi huo ni waasi wa kundi la Codeco.
“Tukio hili limesikika na wanaofanya haya ni waasi wa kundi la Codeco. Eneo hilo lina madini ya shaba na waasi hutumia sare za kijeshi kufanya uvamizi. Raia wengi hawawezi kutofautisha kati ya waasi na wanajeshi wa kweli,” amesema ofisa huyo.
Wakati tukio hili likitokea, Februari 8, 2025, wakuu wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) walipitisha azimio la pamoja la kusitisha mapigano ndani ya DRC.
Katibu wa EAC, Veronica Nduva alitangaza kuwa viongozi wa mataifa hayo wamekubaliana kuanzisha mazungumzo kati ya Serikali ya DRC na makundi mbalimbali ya kijeshi na yasiyo ya kijeshi, likiwamo Kundi la M23, kupitia michakato ya Luanda na Nairobi.