Vatican: Papa Francis anaonyesha dalili za awali figo zake kufeli

Roma. Vatican imesema Papa Francis bado yuko katika hali mahututi, huku vipimo vya damu vikionyesha kuwa ameanza kuonyesha dalili za awali za figo zake kufeli.

Hata hivyo, hali hiyo inayomsumbua kiongozi huyo wa Kanisa Katoliki duniani (88) imedhibitiwa na wataalamu kwa kiwango cha juu, huku akiendelea kupambana na nimonia iliyopo katika mapafu yote mawili.

CNN imeripoti usiku wa kuamkia leo Jumatatu Februari 24,2025, kuwa Papa Francis, ambaye amelazwa hospitali kwa zaidi ya wiki moja, hajaonyesha matatizo zaidi ya kupumua tangu jana jioni.

“Baadhi ya vipimo vya damu vinaonyesha dalili za awali na za chini za kushindwa kufanya kazi kwa figo zake, ambazo kwa sasa zimedhibitiwa,” ilieleza taatifa ya Vatican.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Papa Francis, ambaye bado anapumua kwa msaada wa oksijeni inapohitajika, alishiriki jana katika Misa Takatifu akiwa kwenye nyumba yake iliyopo ghorofa ya 10 ya hospitali ya Gemelli mjini Roma Jumapili asubuhi, kulingana na taarifa hiyo.

Vatican ilisema miongoni mwa waliohudhuria ibada hiyo ni pamoja na madaktari wanaomhudumia hospitalini.

“Ugumu wa hali yake ya kiafya na umuhimu wa kusubiri matibabu ya dawa kutoa majibu fulani ni miongoni mwa masuala ambayo yanatulazimu kumuongezea uangalizi wa hali ya juu,” ilisema Vatican.

Mapema Jumapili, Vatican ilisema Papa Francis aliwekewa oksijeni ya kiwango cha juu baada ya kupata matatizo ya kupumua, kisha kupata usingizi wa kutosha.

Papa aliwashukuru wafanyakazi wanaoendelea kupambania maisha yake kwa kumpatia matibabu hayo, wakati wa ibada iliyofanyika Jumapili.

Mapema Jumamosi, Vatican ilisema atabaki hospitali baada ya kukumbwa na nimonia na hataweza kuongoza sala ya kila wiki ya Angelus, ikiwa ni mara ya tatu tu katika karibu miaka 12 ya huduma yake kama Papa.

Hali ya Papa ilionekana kuwa inaimarika mapema wiki hii, huku Vatican ikieleza kuwa alikuwa akionyesha matumaini kwenye matibabu ya nimonia.

“Je, Papa yuko nje ya hatari? Hapana. Milango yote miwili iko wazi. Je, yuko kwenye hatari ya kifo cha ghafla? Hapana. Tiba inahitaji muda kufanya kazi,” alisema Sergio Alfieri, ambaye ni daktari wa upasuaji aliyemfanyia upasuaji Papa hapo awali.

Kiongozi huyo wa Kanisa Katoliki alilazwa hospitalini jijini Roma Februari 14 na awali alifanyiwa vipimo vya maambukizi kwenye njia ya upumuaji. Baadaye aligunduliwa kuwa na nimonia katika mapafu yote mawili baada ya kufanyiwa kipimo cha CT.

Francis, ambaye anatoka Argentina, ana udhaifu wa kupumua. Akiwa kijana, aliwahi kuugua nimonia kali iliyosababisha kuondolewa kwa sehemu ya pafu lake moja.

Mwaka 2021, madaktari pia walimfanyia upasuaji wa kuondoa sehemu ya utumbo mpana kutokana na ugonjwa uitwao Diverticulitis, ambao unaweza kusababisha uvimbe au maambukizi ya utumbo.

Alilazwa hospitalini kwa sababu ya changamoto ya bronchitis mwaka 2023, na katika miezi ya hivi karibuni alikumbwa na ajali mbili ambapo aliumia kidevu na mkono wake.

Huu ni muda wa tatu mrefu zaidi kwa Papa Francis kuutumia hospitalini tangu achaguliwe kuwa Papa.

Madaktari wake wamemshauri kupumzika kabisa. Hata hivyo, akiwa hospitalini alikuwa anaendelea na baadhi ya kazi, ikiwa ni pamoja na siku mbili za kwanza hospitalini ambapo alipiga simu yake ya kila siku kwa Mchungaji Gabriel Romanelli na msaidizi wake, Padre Yusuf Asad, huko kaskazini mwa Gaza.

Wamekuwa wakiwasiliana mara kwa mara tangu Israeli ilipoanzisha mashambulizi yake eneo la Gaza nchini Palestina dhidi ya Hamas Oktoba 7, 2023.

Francis pia ameendelea kusaini maamuzi akiwa hospitalini, msemaji wa Vatican Matteo Bruni aliambia CNN.

Hadi sasa, ni wasaidizi wake wa karibu pekee waliomtembelea, msemaji huyo wa Vatican aliieleza CNN.

Jumatano, Waziri Mkuu wa Italia, Giorgia Meloni, alimtembelea na kumjulia hali kwa dakika 20.

“Tulitania kama kawaida. Hajapoteza ucheshi wake wa kawaida,” waziri mkuu huyo alisema katika taarifa yake kwa umma.

Taarifa zinadai kuwa waumini wamekusanyika nje ya miji mikuu ya Italia na Argentina na kwenye makanisa wakiwa na mishumaa ili kumuombea kiongozi huyo arejee kwenye hali ya utimamu wa kiafya.

“Daima tunamweka katika nia zetu,” alisema Rodomina Valdez, raia wa Argentina (45) katika Kanisa Kuu la Metropolitan, jijini Buenos Aires nchini humo.

“Lakini tunachoweza kufanya ni kumweka katika sala zetu na kutoa kafara au hata kufanya toba kwa njia yoyote,” aliongeza.

Imeandikwa na Mgongo Kaitira kwa msaada wa Mashirika.

Related Posts