Februari 21, 1965, saa 9:30 alasiri, New York, Marekani, taarifa kutoka Hospitali ya Columbia Presbyterian, ilikuwa yenye mguso mkubwa wa simanzi. Kiongozi wa kijamii, Malcom X au el-Hajj Malik el-Shabazz, alikuwa amekamilisha tarakimu zake duniani.
Miaka 60 imetimia tangu nafsi ya X ilipoagana na mwili. Wanaharakati na viongozi wa kijamii wanaibuka kizazi kwa kizazi.
Pamoja na hivyo, watu wote wanaweza kukutana kwenye mwafaka huu; X ni mmoja tu, hakuna kama yeye kabla yake, hayupo mwingine mfano wake tangu alipoingia kaburini.
Miongo sita imekamilika akiwa amepumzika kwenye makaburi ya Ferncliff, Hartsdale, New York. Nguvu yake ya ushawishi, misimamo na mitazamo yake, ni chachu ya kufananishwa au kulinganishwa na viongozi wengine mashuhuri wa kijamii hadi wanaharakati.
Marcus Garvey, aliyeanzisha vuguvugu la Wamarekani weusi kurudi barani Afrika aliloliita “Back to Africa”, Martin Luther King Jr, kiongozi wa kijamii aliyeweka rekodi ya utetezi wa haki za raia kupitia maandamano ya amani na hotuba zenye kugusa nyoyo, Tupac Shakur, mwana-Hip Hop mwenye ushawishi zaidi kupata kutokea, na wengine, wamekuwa wakifananishwa na X.
Uchambuzi wa wasifu wa X, jinsi alivyokusanya maono yake kutoka Asia hadi Afrika, ujasiri wake wa kujenga hoja zenye kuwatikisa watawala na jumuiya kubwa ya Wazungu, alivyoweza kujifanyia tathmini na kutoa mtazamo au msimamo mpya dhidi ya aliokuwa nao kabla, ni mambo yanayompambanua X kuwa wa kipekee. Hafanani na Garvey, King, Tupac wala yeyote.
Moyo wa kimapinduzi wa X ni zawadi ya asili, lakini kichocheo ni maisha ya ubaguzi na manyanyaso ambayo yeye na jamii yote ya Wamarekani weusi waliyapitia. Alikuwa mwanafunzi mwenye kipawa kikubwa darasani.
Aliweka nadhiri ya kusoma sheria ili akabiliane na mifumo ya kisheria iliyokuwa ikikandamiza watu weusi.
X, alisoma ‘high school’ za West Junior, iliyopo Lansing, jimbo la Michigan, Marekani, kisha Mason, jijini Mason, Michigan. Akiwa Mason, aliambiwa na mwalimu Mzungu kuwa masomo ya sheria hayawafai watu Weusi. X aliona mfumo wa elimu ya Weupe hauna uhalisia kwa Weusi, akaacha shule kabla ya kuhitimu.
Mguu ulioondoka Mason High School haukuwa na heri hata kidogo. X, aliingia mtaani akiwa na fikra mbaya.
Kuwawinda matajiri wa Kizungu na kuwaibia. X, akiwa na umri kati ya 14 na 21, angezunguka majiji ya Boston (Massachusetts), Flint (Michigan) na New York kwenye kitongoji cha Harlem, akifanya vibarua na kutafuta upenyo wa kuwaibia Wazungu.
Hatima ya maisha hayo ya zigzaga ilikuwa jela. Mwaka 1946, X akiwa Boston, alikamatwa alipokuwa amekwenda kwa fundi kuchukua saa aliyoipeleka kwa ajili ya matengenezo. Ilikuwa saa ya wizi.
Alishitakiwa kwa makosa ya wizi na kuhukumiwa kifungo jela cha miaka nane hadi 10 kwenye gereza la Charlestown. Miaka miwili baadaye alihamishiwa gereza la Norfolk, Massachusetts.
Kujiunga na Nation of Islam
Jela ni nusu jehanamu kwa aliyeamua kutafsiri hivyo, ila kuna ambao kwao maisha ya gerezani ni mwanzo wa safari ya mbinguni. Ndivyo ilikuwa kwa X. Kuta za gereza zilimkutanisha na John Bembry, alikuwa binadamu muungwana na mwenye nidhamu ya hali ya juu katika maisha.
Bembry alipata maarifa mengi kupitia kujisomea. Alimwambukiza X. Safari ya kujifunza mambo mapya ilimfikisha X kwenye madhehebu ya Nation of Islam, ambayo ni jumuiya ya kiharakati ya dini ya Kiislam, Marekani, alivutiwa na Nation of Islam.
Reginald ni kaka wa X. Naye akiwa mtu huru, alivutiwa pia na mafundisho ya Nation of Islam. Reginald alikuwa akimwandikia barua X mara kwa mara, akimtaka kufuata yale yaliyoelekezwa na Nation of Islam, vilevile kujitenga na yaliyokatazwa. X, alikuwa mvutaji sigara aliyekubuhu. Alianza kuacha wakati huo.
Mwaka 1948, X, alimwandikia barua aliyekuwa Kiongozi wa Nation of Islam, Elijah Muhammad.
Alimweleza nia yake ya kujiunga na Nation of Islam. Elijah alimpa maelekezo X ya kutubu makosa yake na kuwa mnyenyekevu kwa Mungu. Ni wakati huo X alisilimu na kuwa muumini wa Nation of Islam.
Mwongozo wa Elijah kwa waumini wa Nation of Islam ulikuwa kuachana na majina yao ya awali wanaposilimu na kuchukua mapya, ambayo yangewatambulisha kuwa ni Waislam. X, alianza kujiita Malcolm X. Jina lake la vyeti vya kuzaliwa ni Malcolm Little.
X, alijitenga haraka na jina la “Little” kwa kuwa ni la ukoo wa Wazungu waliowatumikisha babu na bibi zake nyakati za biashara za utumwa.
Badala ya Little ndiyo aliweka X. Kuanzia mwaka 1950, nyaraka zote alizoandika au kusaini, alijitambulisha kama “Malcolm X”, badala ya Malcolm Little.
Alisema kuwa X ni kiwakilishi cha jina lake la Kiafrika ambalo hakulijua. Elijah alimpa jina la Malik el-Shabazz, lakini halikuweza kuwa na nguvu ya kulifunika “Malcolm X”.
Alipokwenda kuhiji Makka, Saudi Arabia, hivyo kupata daraja la hajj, alianza kujitambulisha kama el-Hajj Malik el-Shabazz. Bado Malcolm X lilikuwa jina linalomtambulisha. Alichagua Malik kwa sababu ni Kiarabu cha Malcolm.
Mwaka 1952 alitoka jela kwa msamaha. Haraka sana alidhihirisha kipawa chake cha kuhubiri, akajikita pia kwenye harakati za kupigania haki za watu Weusi. Chuki ya X kwa Wazungu ilikuwa juu. Alipojiunga na Nation of Islam, iliongezeka.
Nation of Islam walihubiri kuhusu Wazungu na Wamarekani wenye asili ya Afrika, Kusini ya Jangwa la Sahara, wagawane majimbo kila jamii iishi kwao, ili amani ya kudumu ipatikane Marekani.
Walihubiri pia Wamarekani wenye asili ya Afrika, Kusini ya Jangwa la Sahara kurudi nyumbani.
Kipindi chote, X baada ya kutoka jela, alihubiri kwa kuwatambulisha Wazungu kuwa ni maadui wa Afrika. Hotuba zake kali zilimfanya ajenge ufuasi mkubwa, na alipendwa sana ndani ya jumuiya ya Weusi, walioishi kinyonge na kujenga matumaini kupitia wenzao wenye ujasiri wa kuwakabili Wazungu.
Katikati ya mapambano yake dhidi ya Wazungu, X aliwahi kuulizwa kama hahofii maisha yake, alijibu: “Sihofii, na kwambia, mimi ni mtu ninayeamini nilikufa miaka 21 iliyopita. Ninaishi kama mtu ambaye tayari ameshakufa. Sina hofu dhidi ya mtu yeyote wala kitu chochote.”
X, aliwatambulisha Wazungu kuwa watu wenye macho ya bluu na hudhurungi (brown). Alipokuwa kwenye mikutano ya hadhara, alipoona Wazungu, alisema: “Naona baadhi ya maadui zetu wapo hapa.” Rejea hotuba ya X, “The Ballot or the Bullet” – “Kura au Risasi”, aliyoitoa Cory Methodist Church, Cleveland, Ohio na King Solomon Baptist Church, Detroit, Michigan, Aprili 3 na 12, 1964.
Aprili 20, 1964, X, alikuwa mmoja wa waumini walioanza ibada ya Hijja, Makka, Saudi Arabia, ambayo ilikamilika Aprili 22, 1964, kwa ibada ya Eid-al-Adha.
Aliyoyashuhudia wakati wa Hijja, kuanzia mwanzo, Siku ya Arafa (Aprili 21, 1964), hadi Eid-al-Adha yenyewe, ilimfanya X abadili mtazamo kwa kiasi kikubwa.
Kuona watu wa rangi zote wakikusanyika pamoja, bila ubaguzi, wakifanya ibada kwa unyenyekevu mkubwa, ilimgusa X. Marekani aliwatambua Wazungu ni maadui. Alipofika Makka, aligundua kumbe kuna Wazungu ambao angeweza kuwaita ndugu.
Kupitia andiko lake, alilolipa jina “Letter from Mecca” – “Barua Kutoka Makka”, X alisimulia upendo aliouona kwa watu wa rangi zote, ambao hakuwahi kuushuhudia kabla. Safari hiyo ya Hijja ndiyo iliyobadili mtazamo wa X, kutoka chuki iliyopitiliza na kuyaelekea masuala ya kimsingi ili jamii zote ziishi kwa usawa.
X, alipotoka Makka, alifanya ziara Afrika. Akakutana na vuguvugu la ukombozi wa Bara la Afrika.
Alivutiwa na mfumo, maono na shabaha ya uliokuwa Umoja wa Nchi Huru za Kiafrika (OAU), ambao uliasisiwa na Baba wa Taifa la Tanzania, Mwalimu Julius Nyerere na viongozi wengine wa mataifa 31 ya Afrika.
Aliporejea Marekani, X alijitenga na Nation of Islam, akawa mfuasi wa Sunni Islam. Kidini, alianzisha taasisi ya Muslim Mosque, Inc (MMI), halafu kuendesha harakati za kiraia, alifungua jukwaa aliloliita Organization of Afro-American Unity (OAAU).
Kutoka OAU ya akina Mwalimu Nyerere, X aliongeza A moja, kupata OAAU. Badala ya Africa ya OAU, yeye aliweka Afro-American.
Uamuzi wake wa kuhama Nation of Islam uliibua chuki na uhasama mkubwa. X, binafsi na mkewe, Betty X “Betty Shabazz, walipokea ujumbe wa vitisho kila mara. Ilipofika Februari 21, 1965, X, mbele ya mkewe na baadhi ya mabinti zake, alipigwa risasi, zilizoondoa uhai wake. Alikuwa na umri wa miaka 39 wakati mauti yanamkuta.
X, alikuwa akijiandaa kuhutubia umati wa watu 400, ukumbi wa Audubon Ballroom, Manhattan, New York.
Alikuwa na mkewe, vilevile binti zake. Yupo mtu aliingia ukumbini na kupaza sauti kuwa kuna mtu aliweka mkono kwenye mfuko wake. Alilalama “Nigga, get your hand Outta my pocket.”
X na walinzi wake waliposogea ili kuweka sawa mambo, yule mtu aliyekuwa akipaza sauti, aliiona fursa na kumshambulia X kwa mapigo mfululizo ya risasi. Uchunguzi wa mwili wa X, ulitoa majibu kwamba alipata majeraha 21 ya risasi.
Thomas Hagan au Talmadge Hayer, alikuwa muumini wa Nation of Islam na jina lake la Kiislam ni Mujahid Abdul Halim.
Ndiye alimpiga risasi na kumuua X. Kupitia kiapo cha kisheria mahakamani mwaka 1977, Hagan alikiri kumuua X kama kisasi baada ya mwanaharakati huyo kumkosoa Kiongozi wa Nation of Islam, Elijah Muhammad.
Pamoja na kuvutiwa na OAU, X alipenda vuguvugu la uhuru wa Kenya kupitia mapambano, Mau Mau (1952 mpaka 1960). Alitaka Wamarekani Weusi waige Mau Mau dhidi ya Wazungu.
Alimpenda Makamu wa Rais wa kwanza Kenya, Jaramogi Oginga Odinga. Alimhusudu Waziri Mkuu wa kwanza wa DRC, Patrice Lumumba. Mtoto wa nne wa X, anaitwa Gamilah Lumumba, kwa heshima ya Lumumba.
Mei 19, 1925, jiji la Omaha, jimbo la Nebraska, familia ya baba, Earl Little na mama, Louise Helen Little, ilimpata mtoto wao wa nne. Wakamwita Malcolm. Jumla, Earl na Louise walipata watoto saba.
Wazazi wa X wote walikuwa wanaharakati na walivutiwa zaidi na falsafa za Marcus Garvey. Earl, Baba wa X, alikuwa kiongozi wa taasisi ya Universal Negro Improvement Association (UNIA) katika eneo lao, Louise, mama wa X, alikuwa katibu na ripota wa habari za watu Weusi kutoka Omaha kwenda ulimwengu wa Negro.
Kupitia msimamo huo wa wazazi wake, familia ya X, ilijikuta katikati ya mapambano na taasisi ya kidini madhehebu ya Kiprotestant, Ku Klux Klan, ambao walikuwa Wazungu wahafidhina, vilevile kikundi cha cha kigaidi cha Black Legion, ambacho kilikuwa kikipigania ukuu wa Wazungu (White Supremacy).
X alipokuwa na umri wa miaka sita, baba yake alipoteza maisha katika ajali barabarani. Louise, mama wa X, alisema kuwa Earl aliuawa na kikundi cha Black Legion. Kisha, Louise alipatwa na matatizo ya akili, akalazwa Hospitali ya Magonjwa ya Akili ya Kalamazoo, Michigan. Kutokana na mazingira hayo, watoto walitawanyika, wengine, hasa wadogo walilelewa vituo vya watoto wanye uhitaji.
X, alikuwa mmoja wa watoto waliolelewa kwenye vituo, wakati mwingine aliishi kwa ndugu zake. Baada ya X kuwa mtu mzima, ikiwa ni baada ya miaka 24 mama yao akiishi hospitali, kwa kushirikiana na ndugu zake, walimtoa hospitali na kuanza kumlea wenyewe. Louise alifariki dunia Desemba 18, 1989.
X, alifunga ndoa na Betty Januari 14, 1958. Katika ndoa yao walipata watoto sita wote wa kike. Attallah (1958), Qubilah (1960), Ilyasah (1962), Gamilah Lumumba (1964) na mapacha, Malikah na Malaak (1965).
Mwaka 1995, Qubilah, alifunguliwa mashitaka ya kula njama kutaka kumuua Kiongozi wa Nation of Islam, Louis Farrakhan, akidai ndiye mhusika mkuu wa mauaji ya baba yake. Farrakhan alijitokeza kumtetea Qubilah. Kisha, Betty na Farrakhan walifanya mkutano wa maridhiano kwenye ukumbi wa Apollo Theatre, Upper Manhattan, New York. Betty, alifariki dunia mwaka 1997.