Goma. Umati wa maofisa wa polisi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) wamekacha na kujiunga na kundi la waasi la M23, huku wakijisajili kwa ajili ya kupatiwa mafunzo ya kijeshi na waasi hao.
Reuters imeripoti jana kuwa askari hao waliovalia sare za kijeshi za rangi ya bluu walionekana wakiimba na kupiga makofi katika mji wa Bukavu uliotekwa na M23 Jumamosi Februari 16,2025.
Kwa mujibu wa Msemaji wa Muungano wa Waasi wa Alliance Fleuve Congo (AFC/M23), Lawrence Kanyuka, takriban maofisa wa polisi 1,800 wamejisalimisha huku wakijisajili kwa ajili ya kupatiwa mafunzo na wengine 500 wakifanya hivyo siku moja baadaye.
Askari hao wanajiandaa kwa ajili ya kupatiwa mafunzo mapya chini ya mamlaka ya waasi hao (M23) ambao wanadaiwa kuungwa mkono na Serikali ya Rwanda, japo Rais Paul Kagame kukanusha madai hayo.
Pia M23 hawaonyeshi dalili za kukata tamaa kusonga mbele badala yake wanaonyesha nia yao ya kubaki na kutawala.
Waasi wa M23 walivamia mji wa pili kwa ukubwa mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) wa Bukavu, wiki moja iliyopita na kuibua uporaji na machafuko wakati vikosi vya Congo vilipojiondoa katika mji huo.

Kutekwa kwa maeneo makubwa mashariki mwa Congo na rasilimali muhimu za madini na waasi wa M23 kumeongeza hofu ya vita kubwa zaidi na kusababisha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kutoa tamko kuwa linawataka waasi hao wasitishe mapigano.
Hata hivyo, hakuna dalili kwamba mwito huo utazingatiwa huko Bukavu. Maofisa wa polisi waliokusanyika, wakiwa wamevaa sare mpya, waliambiwa kuwa wataondoka kwa mafunzo ya siku chache kisha kurejea kuisaidia M23.
“Mrejee kwetu mkiwa na afya njema ili kwa pamoja tuendelee kukomboa nchi yetu,” alisema Kamanda wa Polisi, Jackson Kamba.
Mpaka sasa Serikali ya Congo haijazungumza chochote kuhusiana na suala hilo.
Wakazi kadhaa walionyesha hofu kuhusu uamuzi huo wa askari polisi kusalimu amri na kujiunga na M23.
“Japo baadhi ya shughuli zimeanza kurejea ila kuwasili kwa M23 huko Bukavu kumelemaza maisha ya eneo lote, ingawa shughuli fulani zinaanza tena kwa namna tofauti. Hatuwezi kushangilia chochote kilichofanywa kwa nguvu,” alisema Mkazi wa Bukavu, Josue Kayeye.
Vikosi vya Jeshi la Ulinzi la FARDC viko katika wakati mgumu kwenye uwanja wa mapambano hususan katika Mji wa Minembwe ulioko eneo la mlimani mwa Jimbo la Kivu Kusini, na uwanja wake wa ndege ukiwa mikononi mwa M23 tangu Ijumaa iliyopita.

Kwa mujibu wa chanzo cha habari kutoka ndani ya jeshi la nchi hiyo na Umoja wa Mataifa, siku chache zilizopita kiongozi wa waasi, Kanali Makanika aliuawa katika shambulizi la ndege isiyo na rubani (droni) ya FARDC.
Wakuu wa vikosi vya ulinzi vya mataifa ya Afrika Mashariki nao walikutana jijini Nairobi, Kenya Ijumaa Februari 21, 2025 kujadili mgogoro huo.
Ripoti ya ndani ya mkutano huo, iliyopokelewa na Reuters, ilionyesha kuwa kundi hilo lilisema halina picha ya wazi ya hali ilivyo mashariki mwa DRC.
Hata hivyo, wakuu hao wa vikosi vya kijeshi walipendekeza kufanyika kwa mazungumzo ya moja kwa moja kati ya pande zote za mzozo, kulingana na ripoti hiyo iliyonukuliwa na Reuters.
Pia Serikali ya DRC imekataa kufanya mazungumzo na waasi wa M23.
Imeandikwa na Mgongo Kaitira kwa msaada wa Mashirika.