Wakimbilia polisi baada ya kutolewa mapepo kwa kuchapwa viboko

Kenya. Waumini wawili wanawake, Mercy Rono (38) na Mercy Cherotich (30) kwa sasa wanauguza majeraha baada ya kutandikwa viboko na mchungaji wao, aliyedai kuwatoa mapepo kwa njia hiyo.

Kwa mujibu wa tovuti ya Tuko, tukio hilo limetokea kwenye Kanisa la Betheli katika eneo la Kapkwen, Kaunti ya Bomet nchini Kenya ambapo katika kuwatoa mapepo wachafu waumini hao,  mchungaji aliwatandika viboko na kushindwa kuvumilia maumivu.

Inaelezwa baada ya uchungu wa viboko kuzidi wanawake hao walikimbia na kwenda kutoa taarifa polisi, huku mchungaji huyo na watu wengine waliohusika kutoroka na sasa wanatafutwa.

Kwa upande wake Ofisa Mkuu wa Afya wa Kaunti ya Bomet, Felix Langat amethibitisha kwamba wanawake hao wamepata majeraha mengi katika miili yao.

Kamanda wa Polisi wa kata ya Bomet, Edward Imbwaga ametoa agizo la kufungwa kwa kanisa hilo mara moja huku polisi wakiendelea na msako wa mchungaji na wenzake waliotoroka baada ya kutekeleza tukio hilo.

“Tunachunguza usajili wa kanisa na kwa jinsi linavyofanya kazi kwa muda mrefu. Ripoti zinaonyesha kuwa waumini wake wengi ni wanawake,” Kamanda Imbwaga amesema.

Hata hivyo, shambulio hilo limezua ghadhabu kwa umma, huku wakazi wenye hasira wakitishia kulibomoa iwapo viongozi wataruhusu kufunguliwa tena.

Related Posts