Dar es Salaam. Suala la mipango ya matumizi bora ya ardhi, limetajwa kuwa suluhisho la changamoto zinazosababisha migongano kati ya wanyamapori na binadamu vijijini na kusababisha ugumu wa pande hizo mbili kuishi pamoja.
Hayo yamebainishwa leo Mei 16, 2024 wakati wa majadiliano yaliyoandaliwa na Chama cha Waandishi wa Habari za mazingira Tanzania (JET) wanaotekeleza mradi wa USAID Tuhifadhi Maliasili kwa lengo la kuhamasisha utunzaji wa mazingira.
Akizungumza kwenye majadiliano hayo, Ofisa Wanyamapori Mkuu na Mratibu wa maliasili, Mazingira na Mabadiliko ya Tabianchi kutoka Ofisi ya Rais (Tamisemi), Hawa Mwechaga amesema asilimia 55 ya misitu inapatikana kwenye maeneo ya serikali za mitaa na ambako ndiko kuna wakulima na wafugaji.
Hata hivyo, amesema njia pekee ya kufanya binadamu na wanyamapori waishi pamoja ni suala zima la mipango ya matumizi bora ya ardhi. Amesema Tamisemi kama wizara ya uratibu, inashirikiana na Wizara ya Maliasili ma Wizara ya Ardhi katika kuangalia usalama wa wanyamapori.
“Ni vizuri tukaona umuhimu wa kuainisha maeneo, mnyamapori apite wapi, lakini wenzetu wa kilimo wanapaswa kulima wapi. Kwa hiyo Tamisemi tunashirikiana na wadau na tunafanya vizuri.
“Kuna maeneo ambayo tumeanza kutenga, kwa bahati mbaya unakuta eneo ni ushoroba lakini kuna wafugaji wanafuga pale, au unakuta kuna msitu wa kijiji, unafanyaje hapo?” amebainisha ofisa huyo wa Tamisemi.
Ameongeza kuwa hekta milioni 21 za misitu ziko kwenye ardhi za vijiji, kwa mujibu wa utafiti uliofanyika mwaka 2015, kati ya hizo, hekta milioni 3.5 zinamilikiwa na halmashauri pamoja na misitu mingine inayomilikiwa na jamii.
“Tuna changamoto ya migogoro ya matumizi ya maeneo, mtu mwingine anakwenda kujenga kwenye mapito ya wanyama, kwanini anajenga? Tembo anapita pale tangu wakati wa ukoloni lakini wewe umefika pale unatamani mikorosho, unajenga kibanda chako.
“Kumbe tembo yeye anajua hii ndiyo njia yangu, akifika anahisi wewe ni mvamizi, halafu na wewe unasema tembo ni mvamizi,” amesema Mwechaga.
Hata hivyo, ofisa huyo wa Tamisemi amesema changamoto kubwa katika utekelezaji wa mipango hiyo ni upatikanaji wa rasilimali fedha, ambapo hadi sasa hawajafika asilimia 50 ya vijiji vilivyopo nchini kwa kuviwekea mipango bora ya matumizi ya ardhi.
“Serikali inaendelea kuongeza bajeti kwenye mamlaka za serikali za mitaa kuona wanakwenda kuhifadhi lakini na kutoa elimu kwa wananchi kuhusu masuala ya uhifadhi,” amesema Mchaga wakati majadiliano hayo.
Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa Wanyamapori kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii, Fortunata Msofe amesema wananchi wana fursa kubwa ya kunufaika na shughuli za utunzaji wa misitu hasa ya biashara ya hewa ukaa
Amesema shirika la USAID kupitia mradi wake wa “USAID Tuhifadhi Maliasili” wameweza kutambua shoroba 11 za wanyamapori na pia shoroba za kipaumbele ambazo zisipofanyiwa mipango ya matumizi bora ya ardhi, zinaweza kupotea kabisa.
“Mradi huu umeanza kuongoa shoroba mbili ambazo zimefikia hatua ya mwisho ya kutangazwa kama shoroba, moja ya shoroba hizo ile inayounganisha hifadhi ya Mlima Udzungwa na hifadhi ya Taifa ya Nyerere.
“Pia, tuna ushoroba mwingine kaskazini mwa Tanzania ambao unaunganisha hifadhi ya taifa ya Tarangire na hifadhi ya Taifa ya Ziwa Manyara, ushoroba huu unafahamika kama Kwakuchinja,” amesema mkurugenzi huyo.
Mmoja wa waandishi wa habari walioshiriki majadiliano hayo, faraja Masinde amesema majadiliano hayo yamemwongezea uelewa wa namna uhifadhi unavyoweza kuwanufaisha wananchi huko vijijini.
“Nimejifunza kwamba vijiji vinanufaika sana na shughuli za uhifadhi hususani kupitia biashara ya hewa ya ukaa. Kupitia biashara hiyo, wanapata fedha za kuboresha huduma za kijamii kama vile kujenga zahanati na shule,” amesema Masinde.