Aliyeshtakiwa kwa kujaribu kuua Musoma aachiwa huru

Arusha. Mahakama Kuu Masijala Ndogo ya Musoma imemuachia huru, Zilipa Makondoro, aliyekuwa ameshtakiwa kwa kosa la kujaribu kumuua, George Kaloko kwa kumjeruhi kwa kutumia jembe kichwani.

Mahakama hiyo imefikia uamuzi huo baada ya kupitia ushahidi uliotolewa na upande wa mashitaka na kusema umeshindwa kuthibitisha mshtakiwa huyo ndiye alimjeruhi George.

Hukumu hiyo imetolewa Februari 21, 2025 na Jaji Marlin Komba aliyekuwa akisikiliza kesi hiyo ambapo nakala yake inapatikana katika mtandao wa Mahakama.

Alisema ni kanuni ya kawaida ya sheria katika kesi za jinai, upande wa mashitaka una wajibu wa kuthibitisha kwa kiwango kisichoacha mashaka kuwa mtu aliyeshtakiwa ni kweli alitenda kosa husika.

“Kwa kufanya hivyo upande wa mashitaka lazima uthibitishe mtuhumiwa alitaka kumuua George na ni sheria kwamba mshtakiwa hapaswi kutiwa hatiani kwa sababu ya utetezi dhaifu.”

“Katika kesi hii nimeona upande wa mashitaka umeshindwa kuthibitisha kwamba mshtakiwa aliyefikishwa katika Mahakama hii ambaye alimjeruhi mwathiriwa, na kushindwa zaidi kuthibitisha shambulio hilo lililenga kusababisha kifo, hivyo kumwona mshtakiwa Zilipa hana hatia na namuachia huru kwa kosa la kujaribu kuua kinyume na kifungu cha 211(a) cha Kanuni ya Adhabu,”amesema.

Jaji huyo kabla ya kufikia hitimisho hilo alieleza kesi ya mashitaka ilijengwa na shahidi mmoja ambaye ni wa tatu, Atione Kaloko, ambaye alishuhudia George akishambuliwa.

Jaji alieleza kwa mujibu wa shahidi huyo alisikia sauti za watu wakizozana na alipokwenda sauti ilipokuwa ikitokea alishuhudia Zilipa akichukua jembe, kuligeuza na kumpiga George kichwani ambaye alianguka chini na mshtakiwa alikimbia.

Shahidi huyo alidai jembe hilo liliachwa eneo la tukio wakati George akipelekwa hospitali, ila Jaji katika uamuzi wake alieleza haijathibitishwa kati ya shahidi wa pili na tatu ni nani aliyemchukua George baada ya kushambuliwa na kumpeleka Polisi kisha hospitali kwa ajili ya matibabu.

Jaji Komba alisema suala lingine Mahakama iliangalia ni mahali jembe lilipopatikana ambapo shahidi wa tatu alidai jembe liliachwa eneo la tukio huku shahidi wa tano ambaye ni Polisi akidai jembe lilikuwa nyumbani kwa Zainab Samwel.

“Shahidi wa tano alidai Novemba 9, 2021 alipokwenda kuchora ramani ya eneo la tukio alijulishwa jembe lilikuwa kwa Zainab, shahidi wa saba alidai mshtakiwa aliwapa jembe kutoka kwenye nyumba ya Zainab,” amesema.

“Mtuhumiwa alikuwa kizuizini tangu alipokamatwa Novemba 6, 2021 na aliacha jembe kwenye eneo la tukio, inawezekanaje kwamba mshtakiwa angejua jembe lilipo Novemba 9, 2021 na kuwapa polisi? Nani wa kuamini kati ya shahidi wa tano na saba waliosema jembe lilipo,” alihoji Jaji

Jaji alisema katika utetezi wake mshtakiwa alieleza ni Zainabu ndiye alimpiga mwathiriwa wakati (mtuhumiwa) alipokuwa akipigana naye (George).

Jaji alisema Mahakama hiyo haikupata picha ya x-ray ambayo ingesaidia kuonyesha ukubwa wa tatizo na kuwa anaona upande wa mashitaka ulitakiwa kutoa ushahidi juu ya ukubwa wa na kiwango cha jeraha lililopatikana kwenye fuvu kupitia x-ray.

“Suala kuu katika kesi hii ni jeraha alilopata ikiwa lilikuwa la aina hiyo la kutishia maisha? Jeraha lilikuwa kubwa kiasi gani na jinsi fuvu lilivyoathirika haikuthibitishwa na shahidi wa upande wa mashitaka,” alisema Jaji.

Awali, Novemba 11, 2021 Zilipa alidaiwa kumjeruhi George ambapo shahidi wa nne, Laurent Samwel aliiambia Mahakama kuwa alisikia kelele ya kuomba msaada kutoka mlimani na alipofika alimkuta George akivuja damu kichwani na alipomuuliza alidai amepigwa na Zilipa.

Shahidi wa pili, Dk Crispin Mosabi aliyemtibu George, aliiambia Mahakama alishuhudia George akiwa amejeruhiwa kichwani (karibu na paji la uso), akivuja damu na kuwa aliathirika zaidi kwenye fuvu la kichwa kutokana na jeraha la kukatwa na kitu chenye ncha kali.

Related Posts