BAADA ya nyota wa kimataifa kutoka Burkina Faso, Stephane Aziz KI kufunga ndoa na Hamisa Mobetto wiki iliyopita na kufanya sherehe kubwa kwenye Ukumbi wa Super Dom, Masaki, jijini Dar es Salaam, kumekuwa na stori za pembeni kuhusu wawili hao.
Hata hivyo, baada ya tukio hilo baadhi ya mastaa waliwapongeza wanandoa hao akiwamo nyota wa Yanga, Clement Mzize ambaye licha ya kuwapongeza kwa kufikia hatua hiyo, amempa neno staa mwenzake Aziz KI kuhusu Hamisa anayemwita kama ‘Dada yake’.
Mzize amesema alimwambia Aziz KI kabla ya ndoa hiyo ahakikishe anampenda sana dada yake Hamisa kwani Watanzania wanawapenda sana watu wa nje ya nchi na kuwachukulia kama ndugu zao.

“Kwanza niipongeze hii ndoa ya Aziz KI na mke wake, Hamisa, pili wakati Aziz KI anafanya maandalizi ya kufunga ndoa, niliongea naye chemba, ampende sana dada yetu Hamisa, kwani Watanzania wanapenda watu wao wathaminiwe na wasinyanyasike, hivyo awe makini asije mtenda kwenye ndoa.”
“Nina imani sana na Aziz KI, kwani ni mtu mwenye upendo na ni mcheshi sana, hivyo dada yetu amepata mtu sahihi kabisa, sema kumpa tahadhari ni muhimu sana, mambo yasije kuwa tofauti akapaona pachungu Tanzania (anacheka),” amesema Mzize.

Aidha Mzize amekana habari za mtu akiingia kwenye ndoa basi kiwango cha uchezaji kinashuka.
“Hakuna kitu kama hicho, hizi ni habari zipo tu mtaani, tumeona wachezaji wengi wameoa na wapo kwenye ndoa wanafanya vyema kwneye mechi za timu zao? Sidhani kama kuna kitu hicho,” amesema Mzize.