Matano mambo magumu Fountain | Mwanaspoti

HALI ni mbaya kwa Kocha Mkuu wa Fountain Gate, Mkenya Roberto Matano baada ya kikosi hicho kuchapwa juzi bao 1-0, dhidi ya Dodoma Jiji, na kuifanya timu hiyo kufikisha jumla ya michezo minane ya Ligi Kuu bila ya kuonja ladha ya ushindi.

Katika mchezo huo uliopigwa kwenye Uwanja wa Jamhuri Dodoma, wenyeji walipata bao la dakika ya 38 kwa penalti iliyozua utata ya Iddi Kipagwile, baada ya beki wa Fountain, Amos Kadikilo kumfanyia madhambi, Mwana Kibuta akiwa eneo la hatari.

Akizungumza na Mwanaspoti, Matano alisema hakuridhika na uamuzi wa mwamuzi wa mchezo huo, Ally Mnyupe wa Morogoro baada ya kuwazawadia wapinzani wao penalti aliyokiri haikuwa sahihi, huku akiwatupia lawama pia safu yake ya ushambuliaji.

“Beki wangu hakukusudia kufanya kilichotokea kwa sababu alikuwa haoni kama mwenzake alikuwa nyuma, kwangu haikustahili penalti, japo kabla ya hapo tulikosa nafasi ya wazi ya Elie Mokono dakika ya 30, ambayo labda ingebadili mchezo pia.”

Matano alisema licha ya hayo, ila ana kazi kubwa ya kupambana kutengeneza balansi ya timu hiyo, kwani licha ya kukiri kushindwa kutumia vyema nafasi za kufunga ila hata eneo la ulinzi limekuwa likifanya makosa yanayojirudia mara kwa mara.

Kocha huyo tangu ateuliwa Januari 10, mwaka huu akitokea Sofapaka ya kwao Kenya, amekiongoza kikosi hicho katika michezo mitano ya Ligi Kuu bila ya kuonja ladha ya ushindi, ambapo kati ya hiyo amepoteza mitatu, huku miwili pekee akitoa sare.

Matano aliyechukua nafasi ya Mohamed Muya aliyetimuliwa Desemba 29, mwaka jana baada ya kikosi hicho kuchapwa mabao 5-0, dhidi ya Yanga, katika michezo yake mitano aliyokiongoza, safu ya ushambuliaji imefunga bao moja tu na kuruhusu saba.

Kichapo hicho kwa Fountain Gate, kimeifanya timu hiyo kufikisha jumla ya michezo minane ya Ligi Kuu Bara bila ya kuonja ladha ya ushindi, tangu mara mwisho kilipoifunga Coastal Union nyumbani Tanzanite Kwaraa mabao 3-2, Desemba 13, 2024.

Katika michezo minane, Fountain imepoteza sita na kupata sare mbili, huku yenye ikifunga mabao mawili na  kufungwa 16, ikiwa ni wastani wa kuruhusu mabao mawili kwa kila mechi. Hadi Muya anaondoka aliiongoza mechi 16 ya Ligi Kuu, ikishinda sita, sare mbili na kupoteza nane, japo kiujumla imecheza 21, ikishinda sita, sare nne na kupoteza 11, ikiwa ya pointi 22 ikishika nafasi ya 12.

Related Posts