Unguja. Jumla ya Sh209 milioni zimetolewa kuviwezesha vikundi 18 vya vijana kwa lengo la kuendeleza shughuli za ujasiriamali na biashara, kupitia fedha zinazotolewa na Serikali za mitaa.
Vikundi hivyo vyenye wanachama 134 vimepata fedha hizo kupitia asilimia 10, ambapo wanawake ni asilimia nne, vijana asilimia nne na watu wenye ulemavu asilimia mbili.
Hayo yamebainishwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Kazi, Uchumi na Uwekezaji Zanzibar, Shariff Ali Shariff leo, Jumatano, Februari 24, 2025, wakati akijibu swali la Mwakilishi wa Mwanakwerekwe, Ameir Abdalla Ameir.
Mwakilishi huyo alitaka kujua hatua zinazochukuliwa na Serikali katika kuwakwamua vijana kiuchumi na kutatua changamoto ya ajira nchini.
Akijibu hoja hiyo, Waziri Shariff amesema Serikali imeanzisha programu maalumu ya kutoa mikopo kwa makundi maalumu, ambayo inatokana na asilimia 10 ya mapato ya ndani ya mamlaka za Serikali za mitaa ili kupunguza changamoto hiyo.
“Hadi Desemba mwaka jana, jumla ya vikundi 18 vya vijana vyenye wanachama 134, kati yao wanaume 93 na wanawake 41, vimepatiwa mikopo ya Sh209 milioni kwa lengo la kuimarisha shughuli zao za ujasiriamali na biashara ili kujiajiri,” amesema Shariff.
Pia, amesema hivi karibuni wameanzisha programu ya kuwawezesha wanafunzi wa vyuo vikuu katika masuala ya ujasiriamali. Programu hiyo itawafundisha wanafunzi hao masuala ya ujasiriamali na kubuni mawazo ya kibiashara ili kuanzisha shughuli zao za kiuchumi wanapohitimu chuo.
Waziri Shariff amesema programu hiyo ilizinduliwa Novemba mwaka jana na ilihudhuriwa na wanafunzi 227 wanaosoma fani mbalimbali, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa Serikali kuwawezesha vijana kujiajiri katika shughuli zao za uzalishaji kupitia uchumi wa buluu na mafunzo ya amali.
Akijibu swali la nyongeza, Waziri Shariff amesema wengi wanakosa mikopo hiyo na kujiendeleza kwa sababu wanapoipata wanaitumia kinyume na mawazo waliyoyainisha katika uombaji, na ndiyo sababu wanashindwa kurejesha mikopo ikifika wakati wa urejeshwaji.
Naye, Mwakilishi wa Kuteuliwa na Rais, Juma Khatibu Juma, alitaka kutambua mpango wa Serikali juu ya kutatua kilio cha wafanyabiashara wa mbogamboga na mamalishe katika upatikanaji wa mikopo hiyo.
Akitolea ufafanuzi wa hoja hiyo, Waziri Shariff amesema vikundi vingi vya mbogamboga na mamalishe vinavyoleta maombi hayakidhi matakwa ya mikopo hiyo, ndiyo sababu ya kukosa kwao.
Hivyo, amesema ili kutatua hilo, wanachukua jitihada za makusudi za kutoa elimu kwao ili waweze kutoa mawazo yanayoendana na masharti ya mikopo na kuomba tena.
Pia, amesema zipo baadhi ya manispaa na halmashauri ambazo hazirejeshi asilimia 10 za mapato katika Serikali za mitaa, jambo linalosababisha baadhi ya vikundi kukosa mikopo hiyo katika manispaa zao.
Bila kutaja manispaa hizo, Waziri Shariff amesema wameshakaa chini na uongozi wa manispaa hizo kwa kuwapatia elimu na kujadiliana kwa pamoja ili kutatua changamoto hiyo.
Sambamba na hilo, Waziri amesema wizara hiyo imeamua kutoa mikopo kwa mtu mmoja mmoja kwa watu wenye ulemavu na hawatachukua tena mikopo hiyo kwa vikundi.
Zanzibar na kanuni za kusimamia watoa huduma
Imeelezwa kuwa licha ya Zanzibar kuwa na vyama vya ushirika vya kuweka na kukopa fedha (Saccos) 7,131 vinavyojishughulisha na uendeshaji wa fedha na taasisi zingine, Serikali imesema bado hakuna kanuni zinazosimamia taasisi hizo kisiwani Zanzibar.
Kutokana na hilo, Serikali imesema hadi kufikia sasa haina tathmini yoyote inayohusu utendaji kazi wa taasisi hizo.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Fedha na Mipango Zanzibar, Dk Saada Mkuya, ametoa kauli hiyo akizungumza katika mkutano wa Baraza la Wawakilishi Chukwani.
Alikuwa akijibu hoja ya Mwakilishi wa Mwanakwerekwe, Ameir Abdalla Ameir.
Mwakilishi huyo alitaka kujua ni watoa huduma wangapi wa kifedha waliosajiliwa na kusimamiwa na Benki Kuu ya Tanzania na tathmini ilivyo juu ya utekelezaji wao wa majukumu kwa mujibu wa kanuni.
Akijibu swali hilo, Dk Saada amesema mpaka sasa hakuna tathmini yoyote iliyofanyika juu ya utekelezaji wa kanuni, kwani bado kanuni hizo zipo katika mchakato wa maandalizi chini ya ofisi hiyo.
Amesema ofisi hiyo, kwa kushirikiana na Benki Kuu ya Tanzania (BoT), imekuwa ikitoa elimu ya fedha katika kila mwaka wa fedha kwa njia ya semina na warsha mbalimbali kwa wananchi zinazolenga kutoa ujuzi wa kupanga bajeti na kujua haki na wajibu wao wakati wanapotumia huduma za kifedha.
“Licha ya kuwa na vikundi vya ushirika (Saccos) 7,131, bado hakuna tathmini yoyote iliyofanyika juu ya utekelezaji wa kanuni, kwani kanuni bado zipo katika mchakato wa maandalizi chini ya Ofisi ya Rais, Fedha na Mipango,” amesema Dk Saada.
Amesema hadi Desemba mwaka jana, watoa huduma za kifedha walikuwa wakitoa huduma za benki za biashara 14, zikiwa na matawi 43; 10 kwa upande wa Pemba na 33 kwa Unguja.
Pia, taasisi za huduma ndogo za kifedha zilikuwa tisa, ambapo taasisi hizo husajiliwa na kusimamiwa na ofisi hiyo, huku vyama vya ushirika vya kuweka na kukopa (Saccos) 7,131 vikisimamiwa na Idara ya Maendeleo ya Ushirika chini ya Ofisi ya Rais, Kazi, Uchumi na Uwekezaji.
Pia, Dk Saada ameeleza kuwa malalamiko ya wateja wa huduma za kifedha yanashughulikiwa kwa kuzingatia taratibu zilizopo katika kanuni za Benki Kuu ya Tanzania (Financial Consumer Protection Regulations, 2019).
Amesema kanuni hizo zimeweka taratibu kwa ajili ya kupatia ufumbuzi wa malalamiko ya wateja, ikiwemo kila taasisi ya kifedha kuwa na idara au dawati la kupokea na kushughulikia malalamiko ya wateja.
Nyingine, iwe na sera inayobainisha haki za wateja na utaratibu wa kushughulikia malalamiko, ambapo mteja anapaswa kupeleka malalamiko yake kwa taasisi husika. Iwapo hataridhika, anapaswa kuwasilisha malalamiko yake Benki Kuu ya Tanzania.
Hata hivyo, amesema Benki Kuu imeanzisha mfumo wa kuwasilisha malalamiko unaojulikana kama Sema na Benki Kuu ya Tanzania, ambao unalenga kurahisisha ufumbuzi wa malalamiko ya wateja.
Akiuliza swali la nyongeza, Mwakilishi Ameir alitaka kujua kauli ya Serikali juu ya mikopo mtandaoni na utaratibu wa uendeshaji wa taasisi hizo.
Dk Saada amesema kuwa taasisi za huduma za kibiashara hutoa huduma kwa kufuata taratibu zote zilizowekwa na Benki Kuu ya Tanzania, na kwamba kanuni kwa taasisi ndogo bado zipo katika mchakato wa maandalizi.
Pia, Dk Saada alitoa wito kwa wananchi kuomba mikopo katika taasisi zilizosajiliwa na Serikali. Wakiona taasisi ambayo hawaelewi utaratibu wake, ni vyema kuwasiliana na Serikali ili kuepuka kuingia katika mitego.