Rais Samia: Nimemrudisha Makamba kwa mama

Lushoto. Rais Samia Suluhu Hassan amesema ameamua kumrudisha kwake Mbunge wa Mumbuli, Januari Makamba baada ya kile alichodai alimpiga kikofi.

Kauli ya Rais Samia inakuja miezi saba, tangu alipotengua uteuzi wa Makamba katika nafasi ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.

Ingawa taarifa ya utenguzi wa Makamba ya Julai mwaka jana haikuhusisha sababu ya uamuzi huo wa mamlaka ya uteuzi, alichokisema Rais Samia leo kinaashiria msamaha kwa mwanasiasa huyo.

Utenguzi wa Makamba ulioambatana na wa aliyekuwa Mbunge wa Mtama, Nape Nnauye katika wadhifa wa Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari (kwa sasa ni Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari).

Rais Samia ameyasema hayo leo, Jumatatu Februari 24, 2025 katika hotuba yake kwa wananchi wa Wilaya ya Lushoto, ikiwa ni mwendelezo wa ziara yake mkoani humo.

Baada ya kuhitimisha hotuba hiyo, Rais Samia amemwita Makamba akisema anamrudisha mwanawe huyo kwa mama.

Ameeleza alimpiga kile alichokiita kikofi (alimwadhibu), lakini kama ilivyo kawaida ya mama, anadhifu huku akiwa na msamaha ndani yake.

“Mwisho kabisa nataka nimwite mwanangu Januari hapa aje huku, arudi kwa mama. Sisi wamama mnatujua ukimkera mama anakupiga kikofi anakufichia chakula si ndio?

“Sasa mwanangu (January) nilimpiga kikofi nikamfichia chakula, lakini leo namrudisha kwa mama.  Aya Januari na Bumbuli,” amesema kisha akamkumbatia Makamba na kuibua shangwe na vigelegele kutoka kwa wananchi.

Awali, Makamba katika salamu zake kwenye mkutano huo, ametoa shukrani kwa Rais Samia kwa nafasi zote alizowahi kumteua kuziongoza.

Kwa mujibu wa Makamba, uteuzi katika nafasi hizo, umemjenga kiuongozi, umemheshimisha na hatasahau katika maisha yake.

Amekwenda mbali zaidi na kueleza, mizizi ya utumishi wake katika nafasi za wizara ilianza na Wizara ya Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira.

Akiwa katika wizara hiyo, amesema Rais Samia ndiye aliyekuwa Makamu wa Rais, hivyo alihudumu chini ya usimamizi na mafunzo yake.

“Kama kuna uwezo nilionao kwenye uwaziri mheshimiwa Rais umetokana na malezi yako,” amesema.

Tangu Rais Samia aingie madarakani, Makamba amehudumu katika wizara mbili tofauti, ikianza na Wizara ya Nishati na baadaye, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, kabla kutenguliwa Julai mwaka jana.

Kadhalika, Makamba ameilekeza hotuba yake kushukuru hatua ya Rais Samia kutoa kibali cha ujenzi wa barabara ya Soni hadi Korogwe, akisema hilo linamhakikishia mkuu wa nchi kura katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu.

Hilo linatokana na kile alichoeleza, ni takriban miaka 20 sasa wamekuwa wakiomba ujenzi wa barabara hiyo na sasa mkandarasi anatafutwa.

Rais Samia Suluhu Hassan leo Jumatatu, Februari 24, 2025, amezindua rasmi jengo la Halmashauri ya Bumbuli, Wilaya ya Lushoto, mkoani Tanga, ikiwa ni mwendelezo wa ziara yake mkoani humo. Picha na Rajabu Athumani

Hata hivyo, amesema katika historia ya uchaguzi wa vyama vingi, mara zote kura za CCM Lushoto zimekuwa si chini ya asilimia 80 na kwamba watafanya kazi kuhakikisha ushindi unaendelea.

Tukio la Rais Samia kumkumbatia Makamba, limeibua furaha kwa wakazi wa Lushoto wakisema, hawakutarajia lakini limewafutahisha.

Mmoja wa wananchi wa Lushoto, Hamis Shekizengi amesema hakutarajia kuona tukio kama hilo likitokea, hivyo amefurahishwa nalo.

Amesema kwa imani waliyonayo kwa Makamba, ilihitajika kifanyike kitu kama kilichofanywa na Rais Samia ili wananchi wake wasibaki na wasiwasi.

“Tulikuwa tunajiuliza kwa nini aliondolewa, leo mama kasema amemrudisha kwake, nimefurahi sana,” amesema.

Imeandikwa na Juma Issihaka, Bakari Kiango na Rajab Athumani

Related Posts