Bratislava. Waziri wa Mambo ya Ndani wa Slovakia, Matus Sutaj Estok amesema mtuhumiwa aliyekamatwa kwa kumpiga risasi Waziri Mkuu Robert Fico ameshtakiwa kwa jaribio la mauaji.
“Polisi wanafanya kazi, mtuhumiwa anashtakiwa kwa jaribio la kuua kwa kukusudia,” Estok amewaambia waandishi wa habari alipozungumzia shambulio lililochochewa kisiasa.
Kwa mujibu wa Shirika la Habari la AFP, Waziri Mkuu Fico (59), alipigwa risasi nne jana Mei 15, 2024 alipokuwa katika mji wa Handlova baada ya kuondoka kwenye mkutano.
Taarifa zinasema Fico alikuwa katika hali mbaya na baada ya kufanyiwa upasuaji afya yake inaimarika.
Inaelezwa moja kati ya risasi alizopigwa ilipenya tumboni.
Mshambuliaji alikuwa katika kundi la wafuasi wa Fico waliokuwa wamekusanyika nje ya kituo cha utamaduni cha Handlova, ambako kulifanyika mkutano.
Tukio hilo liliwashangaza maofisa usalama wa Fico, ambao picha zilizosambaa kwenye mitandao ya kijamii ziliwaonyesha wakimbeba na kumuingiza kwenye gari, kisha kuondoka eneo la tukio.
“Jana usiku madaktari waliwezesha kuimarika hali ya afya ya mgonjwa,” amesema Robert Kalinak, Waziri wa Ulinzi wa Slovakia.
Viongozi mbalimbali wamekuwa wakituma salamu kumtakia kheri apone mapema.
Duru za kisiasa zinasema Fico amekuwa akitoa wito wa kusitisha msaada wa kijeshi kwa Ukraine na vikwazo kwa taifa la Russia.
Kutokana na tukio hilo, Rais wa Marekani, Joe Biden amesema:
“Nimeshtushwa kusikia ripoti za kushambuliwa kwa Waziri Mkuu wa Slovakia, Robert Fico. Tunaomba Mungu ili apone haraka, na mawazo yetu yako pamoja na familia yake na watu wa Slovakia.”
“Tunalaani kitendo hiki cha kutisha na cha ukatili. Ubalozi wetu unawasiliana kwa karibu na Serikali ya Slovakia na uko tayari kusaidia,” amesema katika taarifa ya Ikulu.
Imeandikwa na Sute Kamwelwe kwa msaada wa mitandao