Dar es Salaam. Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Mohamed Mchengerwa amesimulia dakika za mwisho za uhai wa baba yake mzazi, Omary Mchengerwa huku akisema: “Nitamkumbuka baba kwa ucha Mungu wake na uzalendo mkubwa aliokuwa nao.”
Mzee Mchengerwa amefikwa na mauti alfajiri ya leo Jumatatu, Februari 24, 2025, katika Mji Mtukufu wa Madina, alikokuwa amekwenda kwenye Ibada ya Umrah kwa siku 10 Makkah na Madina.
Akizungumza na Mwananchi, Waziri Mchengerwa amesema: “Amefariki mji Mtukufu wa Madina Saudi Arabia, mji wa Mtume Muhammad, atasaliwa leo msikiti wa Haram Madina (msikiti wa Mtume saa saba mchana).”

Waziri Mchengerwa aliyekuwa njiani kutoka mkoani Tanga alikokuwa kwenye ziara ya Rais Samia Suluhu Hassan kwenda jijini Dar es Salaam kushiriki dua na kisomo nyumbani kwake Masaki, amesema mzee wake alikuwa amemaliza ibada Makkah siku tano na Madina siku tano na alitarajia kurudi kesho Jumanne.
Akielezea kifo kilivyotokea, Waziri Mchengerwa amesema jana Jumapili alipata changamoto ya mafua akawa amelala, akashtuka usiku akataka kwenda kuswali, kwa sababu hakuwa amesali Isha (saa 2 usiku) akaelezwa atasali alfajiri kwani kwa wakati huo muda ulikwisha kupita.
Kutokana na hali ile ya mafua: “Wakampa dawa ya mafua kama dakika 20 akashtuka kuomba chai, kwa hali ya baridi akapewa,” lakini hakuimaliza hali yake ilibadilika na kuwahishwa hospitali hapo hapo nyuma ya msikiti, ambapo alifikwa na mauti.”
Waziri Mchengerwa ambaye ni Mbunge wa Rufiji amesema baba yake, “alikuwa mtu wa ibada sana, mwenye upendo, msomi, mcha Mungu, mzalendo wa kweli amefanya kazi nzuri.”
Katika kusisitiza hilo, amesema mzee wake ambaye alifanya kazi serikalini na baadaye sekta binafsi akiwa mbobezi wa masuala ya mafuta amesema: “Hakuwahi kuchukua rushwa kwenye utumishi wake na hakuwa mdanganyifu na mkweli sana.”
“Unajua alianza kuitwa Alhaji miaka ya 70 kwa sababu ya ibada, alikuwa hawezi kukosa ibada na ndiyo maana akaitwa Alhaji hata kabla ya kwenda Hijja na alikuja kwenda Hijja miaka ya 2000,” amesema.

Waziri huyo amesema katika mazungumzo na baba yake mwenye miaka zaidi ya 70 amesema, “alikuwa akinieleza hakuwahi kumdhulumu mtu, kuchukua rushwa na ukichukua basi unagombana naye.”
Amedokeza kuwa baba yake alikuwa msomi mzuri, “na hata akikuandikia sms (ujumbe mfupi wa maandishi) anaandika kwa Kiingereza tena safi kabisa na siyo Kiswahili, akiwatumia wajukuu zake au wakwe zake ni Kiingereza tu.”
Katika mazungumzo baina ya Mwananchi na Waziri Mchengerwa amehitimisha akisema, “Kwa historia ya kifo chake kila Mwislamu anatamani apite hivyo, mwisho mwema na hasa kifo cha Madina eneo tukufu, afie pale Madina Mtume alizikwa na alimaliza uhai wake pale.
Kwa mujibu wa ratiba ya familia, Kesho Jumanne, kutafanyika dua ya kisomo jimboni Rufiji, Mkoa wa Pwani na Jumatano itafanyika dua nyumbani kwa marehemu Alhaj Omary Mchengerwa Yombo, jijini Dar es Salaam.