Medo avunja ukimya kutimuliwa Kagera Sugar

ALIYEKUWA kocha mkuu wa Kagera Sugar, Melis Medo anayedaiwa kutemwa na timu hiyo kutokana na matokeo mabaya iliyonayo katika Ligi Kuu, amevunja ukimya kwa kuandika kilichomuondoa ndani ya timu hiyo inayochungulia shimo la kushuka daraja ikishika nafasi ya 15 kati ya timu 16 za ligi hiyo.

Kocha huyo raia wa Marekani inaelezwa amepigwa chini saa chache baada ya Kagera kupasuliwa mabao 2-0 na JKT Tanzania kwenye Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo, Dar es Salaam, bila taarifa rasmi kuwekwa bayana,  lakini mwenyewe ameibuka na kusema yeye ndiye aliyeomba kuondoka klabuni hapo.

Kocha huyo wa zamani wa Gwambina, Coastal Union na Dodoma Jiji, aliliambia Mwanaspoti kuwa, amechana na kikosi hicho tangu juzi, licha ya klabu hiyo kutotoa taarifa rasmi ya kuondoka kwake, ikiwa ni muda mfupi tangu ichapwe na  JKT Tanzania Februari 21.

“Nimeamua kuandika barua kwa viongozi tangu juzi asubuhi ya kuwaomba niondoke kwa hiari yangu mwenyewe, nimechukua pia uamuzi huo ili kulinda heshima yangu, kwa sababu kwa mwenendo ninaouona kikweli ni vyema akaendeleza mwingine,” alisema Medo.

Medo alisema kuondoka kwake haina maana amefeli isipokuwa ameamua kuwajibika kama kocha mwenye weledi, ili atoe fursa kwa wengine kuendeleza pale alipoishia, huku akiwashukuru wachezaji na viongozi kwa ushirikiano waliompa tangu mwanzoni.

Kocha huyo aliyejiunga na Kagera Oktoba 17, mwaka jana akitokea Mtibwa Sugar inayoshiriki Ligi ya Championship kwa sasa, tangu ajiunge nayo ameiongoza katika michezo 14 ya Ligi Kuu Bara, akishinda miwili, sare mitano na kuchapwa saba.

Katika michezo hiyo, kikosi hicho kimefunga mabao 13 na kuruhusu 22, japo kwa ujumla kimecheza michezo 21, ambapo kimeshinda mitatu tu, sare sita na kupoteza 12, huku Medo akikiacha kikishika nafasi ya 15, kwenye msimamo na pointi 15.

Medo alijiunga na Kagera akichukua nafasi ya Mganda Paul Nkata aliyetimuliwa pia Oktoba 10, mwaka jana baada ya mwenendo mbaya wa michezo mbalimbali ya Ligi Kuu Bara aliyoiongoza, tangu aliporithi mikoba ya Fredy Felix ‘Minziro’.

Tangu Nkata achukue mikoba ya Minziro, aliiongoza Kagera katika jumla ya michezo saba ya Ligi Kuu Bara kwa msimu huu wa 2024-2025, ambapo kati yake alishinda mmoja, sare mmoja na kupoteza mitano, akiiacha nafasi ya 14 na pointi nne.

Related Posts