Geita. Mzee mwenye umri wa miaka 103, Hussen Bundala ameuawa kwa kukatwa na kitu chenye ncha kali sehemu mbalimbali za mwili wake na watu wanaodaiwa kuwa ni watoto wake.
Mzee huyo, mkazi wa Kitongoji cha Ihanamilo kilichopo kata ya Nyamtukuza, Wilaya ya Nyanghwale mkoani Geita, aliuawa Februari 5, 2025.
Kufuatia mauaji hayo ambayo chanzo chake hakijajulikana, Jeshi la Polisi Mkoa wa Geita linawashikilia watoto watatu wa kikongwe huyo, wakituhumiwa kuhusika na mauaji hayo.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Jeshi la Polisi Mkoa wa Geita, leo Februari 24, 2025, mzee huyo aliuawa kwa kukatwa na kitu chenye ncha kali sehemu za kichwani, usoni na shingoni.
Katika taarifa yake, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Safia Jongo amewataja waliokamatwa kuwa ni Yombo Bundala (75) Makame Bundala (53) na Shija Bundala (50).
Kamanda Jongo amesema bado uchunguzi wa tukio hilo unaendelea kwa kushirikiana na vyombo vingine vya uchunguzi na uchunguzi ukikamilika watuhumiwa watafikishwa mahakamani kujibu tuhuma zinazowakabili.