SERIKALI YAONGEZA VITUO SAIDIZI NA UNASIHI KWA WARAIBU HADI KUFIKIA 16


Na Gideon Gregory, Dodoma.
Serikali imeendelea kuboresha huduma za tiba kwa watu wenye uraibu wa dawa za kulevya ili kupunguza madhara yanayotokana na matumizi ya dawa hizo ambapo hadi kufikia Mwezi Desemba 2023, ilikuwa na vituo 16 vya tiba saidizi na unasihi kwa waraibu wa dawa za kulevya (MAT Clinics).

Hayo yameelezwa leo Mei 16,2024 Jijini Dodoma na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Jenista Mhagama wakati akitoa taarifa kwa wanahabari juu ya hali ya mapambano dhidi ya Dawa za kulevya na kuongeza kuwa vituo hivyo viliwahudumia waraibu wa dawa za kulevya 15,912.

“Katika kipindi hicho kulikuwa na nyumba 56 za upataji nafuu (sober houses) zikihudumia waraibu 3,488, Serikali ilisimamia kikamilifu uanzishaji
na Uendeshaji wa nyumba hizi”, amesema.

Pia, amesema tiba ya uraibu wa dawa za kulevya hutolewa kwenye vitengo vya afya ya akili vilivyopo katika Hospitali za Wilaya, Mikoa na rufaa nchini.

Ameongeza kuwa Serikali imetenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha Taifa cha Utengamao (National Rehabilitation Centre) kwa ajili ya kuwahudumia waraibu wa dawa za kulevya waliopata nafuu ambapo hatua za mwanzo za ujenzi wa kituo hicho kinachojengwa katika eneo la
Itega Jijini Dodoma zimeshaanza.

Ujenzi wa kituo hicho utasaidia kuwajengea uwezo waraibu wa dawa za kulevya waliopata nafuu ili waweze kujikimu kimaisha na hivyo kutokurejea kwenye matumizi ya dawa hizo.

Aidha ameongeza kuwa katika kuhakikisha kuwa mapambano dhidi ya dawa za kulevya yanaimarishwa nchini, Serikali imenunua Boti yenye mwendo kasi (Speed Boat) ambayo pamoja na shughuli zingine itakuwa ikifanya doria baharini ili kufuatilia vyombo vinavyohisiwa kuingiza dawa za kulevya nchini kama vile Heroini, Methamphetamine na nyingine.

“Boti hii ilizinduliwa rasmi tarehe 28 April, 2024 Jijini Dar es Salaam na Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa, Waziri Mkuu wa Jamuhuri ya
Muungano wa Tanzania na uwekezaji huu mkubwa juu ya vita dhidi ya dawa za kulevya na ukamataji mkubwa uliofanyika mwaka 2023, unadhihirisha dhamira ya dhati na utashi wa kisiasa wa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia”,amesema.

Related Posts