Wanaodaiwa kuiba mafuta ya Tipper kuendelea kusota rumande

Dar es Salaam. Washtakiwa  wa kesi ya wizi wa mafuta katika visima  vya kampuni ya Kimataifa ya Kuhifadhi Mafuta, Tiper Tanzania Ltd (Tiper), wataendelea kusota rumande kwa siku nyingine 14, kabla ya kurejeshwa mahakamani kujua hatima ya upelelezi wa kesi inayowakabili.

Hatua hiyo inatokana na upelelezi wa kesi yao kutokakamilika.

Washtakiwa hao ni aliyekuwa dereva wa Mamlaka ya Bandari (TPA), Tino Ndekela na wenzake saba, ambao wanakabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Dar es Salaam, Kisutu.

Mbali na Tino, washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni mfanyabiashara Fikiri Kidevu; Amani Yamba, Mselem Abdallah , Kika Sanguti, Twaha Salum, Gaudence Shayo na Hamisi Hamisi.

Kwa pamoja wanakabiliwa na  mashitaka 20 yakiwemo ya kutakatisha fedha na  wizi wa mafuta ya petroli na dizeli zaidi ya lita 9.9 milioni na kuisababishia hasara kampuni ya Tiper  ya zaidi ya Sh26 bilioni.

Walipandishwa kizimbani mahakamani hapo kwa mara ya kwanza Oktoba 22, 2024 na kusomewa mashitaka yanayowakabili.

Leo, Jumatatu, Februari 24, 2025, washtakiwa hao wamefikishwa tena mahakamani hapo kwa mara ya tisa kesi yao ilipoitwa kwa kutajwa na kujua hatima ya upelelezi wa shauri hilo.

Wakili wa Serikali, Winiwa Kasala ameieleza Mahakama kuwa upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika na akaomba Mahakama ipange tarehe nyingine ya kutajwa.

Kesi hiyo imeahirishwa na hakimu Geoffrey Mhini, kutokana na hakimu anayesikiliza kesi hiyo Beda Nyaki kuwa likizo.

Hakimu Mhini aliahirisha kesi hiyo hadi Machi 10, 2025 itakapotajwa.

Hata hivyo, washtakiwa wamerudishwa rumande kutokana na shitaka la kitakatisha fedha linalowakabili halina dhamana kwa mujibu wa sheria.

Katika mashitaka yanayowakabili, mashitaka mawili ni ya uharibifu wa mali wanayodaiwa kutenda kati ya Januari Mosi, 2019 na Desemba 31, 2022 eneo la Tungi, Kigamboni, wakidaiwa kuharibu bomba la kusafirishia mafuta aina ya petroli na dizeli mali ya kampuni ya Tiper.

Pia washtakiwa hao, wanakabiliwa na mashitaka 16 ya wizi wa mafuta wakidaiwa  kuiba lita 3,599,458 za mafuta ya aina ya petroli na lita 6,392,356 za mafuta ya dizeli yaliyokuwa yakishushwa kutoka katika meli yakipitishwa katika visima vya kampuni hiyo ya Tiper.

Vilevile, wanakabiliwa na shitaka la kuisababishia kampuni hiyo ya Sh26.01 bilioni, wakidaiwa kutenda kosa hilo  tarehe hizohizo eneo la Tungi, Kigamboni, Dar es Salaam.

Washtakiwa hao pia wanakabiliwa na shitaka moja la kutakatisha fedha kiasi cha Sh20.73 bilioni, kosa  wanalodaiwa kulitenda katika tarehe hizo na eneo hilo, huku wakijua fedha hizo zilitokana na kosa tangulizi la wizi.

Tiper ni kampuni ya kimataifa ya Kuhifadhi mafuta aina ya dizeli na petroli, inayomilikiwa kwa ubia kati ya Serikali ya Tanzia kupitia Msajili wa Hazina na kampuni ya Oryx Energies SA, ya Geneva, Uswis.

Related Posts