Wanafunzi saba wafukuzwa shule Geita, wengine 64 wasimamishwa

Geita. Bodi ya Shule ya Sekondari Geita imewafukuza shule wanafunzi saba na kuwasimamisha kwa vipindi tofauti wanafunzi wengine 64 wa kidato cha sita, baada ya kubainika kushiriki kwenye vurugu zilizotokea shuleni hapo Februari 20, 2025 na kusababisha hasara ya zaidi ya Sh2.9 milioni.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Jeshi la Polisi leo Februari 24, 2025, uchunguzi uliofanywa na jeshi hilo kwa kushirikiana na bodi, ulibaini vurugu hizo zilifanywa na wanafunzi 71 wa kidato cha sita.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Safia Jongo ametaja waliofukuzwa shule kuwa ni Laban Manjano aliyekuwa kiranja mkuu wa shule mwaka 2024, anayedaiwa kuhamasisha mgomo na vurugu hizo wakipinga adhabu ya mwenzao aliyekutwa na simu shuleni kusimamishwa kwa siku 73.

Wengine ni Elias Zacharia, Harrizon Malinga, AhmedMashaka, Frank Paulo, Erick Atanga na Alphonce Makelemo.

Mbali na waliofukuzwa, wanafunzi 19 wamesimamishwa kuendelea na masomo hadi Mei 5, 2025 huku wengine 45 wakisimamishwa kwa muda wa siku 21.

Kamanda Jongo amesema katika uchunguzi huo, wanafunzi 71 walihojiwa na kubainika kuhusika kwenye tukio hilo.

Related Posts