KMC yaichapa Singida FG, yaisogelea Coastal Union

BAO la Ibrahim Elias dakika ya 20 akimalizia vizuri pasi ya Wazir Junior, limetosha kuipa ushindi KMC wa 1-0 dhidi ya Singida Fountain Gate katika mchezo wa Ligi Kuu Bara uliochezwa Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam.

Katika mchezo huo uliokuwa na ushindani mkubwa, ilishuhudiwa nafasi nyingi zikitengenezwa kila upande lakini ilikuwa ngumu kutumiwa vizuri.

Timu hizo ziliingia uwanjani zikifahamu kwamba kila moja ikishinda inasogea nafasi za juu, KMC ikatumia vizuri uwanja wake wa nyumbani kuibuka na ushindi huku Singida Fountain Gate ikijilaumu kwa kukosa nafasi kadhaa za kufunga.

Kabla ya mchezo huo, KMC ilikuwa nafasi ya sita ikicheza mechi 26 na kukusanya pointi 33, lakini sasa imepanda nafasi moja hadi ya tano kwa kufikisha pointi 36 zikiwa tofauti ya pointi mbili nyuma ya Coastal Union iliyopo nafasi ya nne.

KMC ushindi huo umewafanya kuishusha Tanzania Prisons yenye pointi 33 ikicheza mechi 33, hivyo Maafande hao wana nafasi ya kurudi eneo lao endapo watashinda mchezo wao ujao dhidi ya Mashujaa, Mei 20 mwaka huu.

Endapo Singida Fountain Gate ingefanikiwa kuibuka na ushindi, basi ingefikisha pointi 33 na kupanda kutoka nafasi ya 12 hadi sita na kuishusha KMC, lakini imeshindwa kufanya hivyo.

Baada ya mchezo huo, nyota wa Singida Fountain Gate, Deus Kaseke amesema: “Tunamshukuru Mungu tumemaliza mechi salama, mechi ilikuwa na upinzani mkubwa kwani tungeshinda tulikuwa tunawapita na wao walifahamu wakishinda wanapaa juu, hivyo wameitumia vizuri nafasi moja waliyoipata kati ya zile walizozipata huku sisi tukishindwa. Tunawapongeza.

“Bado tuna mechi mbili za kucheza, hivyo tunakwenda kujipanga kuona tunafanya vizuri na kumaliza ligi sehemu nzuri.”

Kwa upande wa mfungaji wa bao pekee, Ibrahim Elias, amesema: “Nimefurahia mechi ya leo tumepata ushindi na ilikuwa muhimu kushinda, namshukuru Mungu tumeshinda.

“Tunaichukulia kila mechi kwa nafasi yake, malengo yetu ni kumaliza nafasi ya nne, tunajipanga na mchezo ujao dhidi ya Simba ambapo mara ya kwanza tulitoka nao sare, kisha tunakwenda kumaliza na Coastal, hivyo mechi zote muhimu kushinda kufikia malengo.”

Baada ya leo, KMC itacheza dhidi ya Simba (Mei 20) kisha itapambana na Coastal Union (Mei 28) katika mchezo wa mwisho msimu huu.

Singida Fountain Gate yenyewe itacheza dhidi ya Geita Gold (Mei 25) na kumaliza dhidi ya Kagera Sugar (Mei 28) ambapo mechi zote hizo itacheza nyumbani.

Related Posts