Mapya afya ya Papa Francis, Vatican yasema…

Roma. Afya ya Papa Francis (88) imeanza kuimarika ikilinganishwa na hapo awali, ambapo kwa mujibu wa taarifa kutoka Ofisi ya Papa (Holy See) matatizo ya figo yaliyoibuka kwa kiongozi huyo wa kiroho siyo ya kutia hofu tena.

Taarifa iliyotolewa usiku wa kuamkia leo Jumanne Februari 25,2025, inasema,  “hali ya kiafya ya Baba Mtakatifu, ingawa ni mahututi, inaonyesha kuboreka kidogo. Hata leo hakukuwa na dalili za matatizo ya kupumua kama pumu, baadhi ya vipimo vya maabara vimeonyesha kuboreka.”

Papa Francis anapokea matibabu ya nimonia katika Hospitali ya Gemelli mjini Rome na leo ikiwa ni siku ya 12 tangu apelekwe hospitalini hapo na hali yake imeanza kuimarika tofauti na siku mbili zilizopita.

Jumapili jioni, Vatican ilitoa taarifa kuwa hali ya Papa Francis ilizidi kuzorota na aliwekwa kwenye chumba cha uangalizi maalumu, huku akipumua kwa msaada wa mashine.

Vatican iliongeza matatizo madogo ya figo ya Papa, yaliyotangazwa mara ya kwanza Jumapili, hayatoi wasiwasi huku akiendelea kupatiwa tiba ya oksijeni.

Vatican ilipozungumza leo na CNN imesema, Francis bado anaweza kusogea, si mgonjwa kitandani na anakula kawaida.

Asubuhi ya Jumatatu, Francis alipokea Ekaristi na kuendelea na kazi mchana, Vatican ilisema. Jioni, alimpigia simu Paroko wa Parokia ya Gaza ambaye amekuwa akiwasiliana naye mara kwa mara tangu Israel ilipoanza kuzingira eneo hilo, baada ya mashambulizi yaliyoongozwa na Hamas Oktoba 7,2023.

Papa alilazwa kwa mara ya kwanza katika kliniki moja mjini Roma siku 11 zilizopita, akifanyiwa vipimo kwa ajili ya maambukizi ya mfumo wa upumuaji. Baadaye aligunduliwa kuwa na nimonia na kuhamishiwa hospitali ya Gemelli.

Viongozi wa kidini na waumini duniani kote wamekusanyika kumuombea kiongozi huyo wa Argentina, ambaye ratiba yake imesitishwa kutokana na matibabu hayo.

Watu walikusanyika katikati ya Mji wa Buenos Aires nchini Argentina alikozaliwa kiongozi huyo jana (Jumatatu) ili kumuombea afya yake iimarike. Baadhi yao walionekana wakilia huku wakiwa wameshikilia picha za Papa.

Binamu wa Papa, Carla Rabezzana, mwenye umri wa miaka 93, anayeishi katika mji wa Portacomaro, Kaskazini Magharibi mwa Jimbo la Asti nchini Italia, alisema familia ina wasiwasi kuhusu afya yake.

“Sote tuna wasiwasi mkubwa. Tunatumaini atapona haraka na kuvuka kipindi hiki kigumu. Ninafuatilia kila kitu kupitia habari ninapata hofu sana,” alikiambia kituo cha Serikali ya Italia, RAI, jana.

Wakati wa misa Jumapili huko Manhattan, Askofu Mkuu wa New York, Kardinali Timothy Dolan, alitoa kauli iliyoibua hisia kali miongoni mwa waumini wa kanisa hilo kwa alichodai kuwa “Francis yuko katika afya dhaifu sana na huenda yuko karibu na kifo.”

Hata hivyo, hakunukuu chanzo chochote cha kitabibu kutoka Gemelli kuwa ndiyo kimempatia taarifa hiyo.

Jumapili, Vatican ilisema baadhi ya vipimo vya damu vya Papa vilionyesha dalili za awali  za figo zake kushindwa kufanya kazi hali ambayo kwa sasa inatajwa kudhibitiwa.

Mtaalamu wa Upasuaji wa Figo kutoka Taasisi ya Orlando Health Medical Group Urology,  Dk Jamin Brahmbhatt aliiambia CNN kuwa mtu hapaswi kuwa na hofu kutokana na taarifa ya Vatican kuhusu afya ya figo ya Papa.

“Sidhani kama ni jambo kubwa sana, lakini tunaweza kuona hali yake bado ni mbaya.”

“Figo ni viungo dhaifu lakini pia vina uwezo wa kujirekebisha,” amesema daktari huyo.

Amesema kwa wazee, maambukizi yanaweza kuzidi haraka ikiwa mwili utashambuliwa kwa nguvu jambo tunaloita sepsis.

Brahmbhatt amesema nimonia ikisababisha sepsis, kuvimba kwa mwili mzima kunaweza kuathiri viungo vingi vya mwili ikiwemo figo.

“Kwa Papa Francis, hili linaonekana kama kushindwa kwa figo kwa kiwango kidogo. Uharibifu wa figo unaweza kuwa wa muda mfupi na kuboreka kwa matibabu ama wa kudumu,” amesema.

Papa Francis ana historia ya kuwa na maambukizi katika mfumo wa upumuaji.

Akiwa kijana, aliwahi kuugua nimonia kali iliyosababisha kuondolewa kwa sehemu ya pafu lake.

Pia mwaka 2021, madaktari waliondoa sehemu ya utumbo wake kutokana na tatizo la ‘diverticulitis’, hali inayosababisha kuvimba ama maambukizi ya utumbo mpana.

Pia aliwahi kulazwa hospitalini  akisumbuliwa na tatizo la ‘bronchitis’ mwaka 2023 na katika miezi ya hivi karibuni amedondoka mara mbili, ambapo aliumia sehemu ya kidevu na mkono wake.

Madaktari wa Papa wamemshauri apumzike kabisa. Hata hivyo, ameendelea kufanya baadhi ya kazi ikiwa ni pamoja na siku mbili za kwanza za kulazwa hospitalini.

Papa Francis pia amekuwa akitia saini maamuzi kutoka kliniki, msemaji wa Vatican Matteo Bruni ameiambia CNN Jumatano iliyopita.

Miongoni mwa walioguswa na hali hiyo ya Papa Francis ni Imamu Mkuu wa Al-Azhar, ambacho ni Kitovu cha elimu ya Kiislamu ya Sunni huko Cairo, Misri, ambapo amesema alikuwa akimuombea.

Wawili hao wameunda uhusiano wa karibu katika miaka ya hivi karibuni.

“Naomba kwa Mungu ampe ndugu yangu mpendwa Papa Francis ahueni ya haraka na ambariki kwa afya njema ili aendelee kuhudumia ubinadamu,” amesema Imamu Mkuu Ahmed El-Tayeb.

Imeandikwa na Mgongo Kaitira kwa msaada wa mashirika.

Related Posts