BALOZI MUSSA AKAGUA MAJENGO YA UBALOZI WA TANZANIA NCHINI MALAWI.

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki ambaye pia ni Mwenyekiti wa kamati ya miradi ya Wizara, Balozi Said Shaib Mussa, ametembelea majengo ya Ubalozi wa Tanzania nchini Malawi na kukagua kiwanja cha Ubalozi huo jijini Lilongwe.

Katika ziara hiyo, Balozi Mussa aliwaambia Watumishi wa Ubalozi huo kuwa Serikali inatambua umuhimu wa kuwa na miundombinu bora katika ofisi zake za uwakilishi nje ya nchi na kufafanua kuwa licha ya changamoto ya ufinyu wa bajeti, Serikali ina dhamira ya dhati ya kukarabati na kuimarisha majengo hayo ili yawe katika viwango vinavyostahili.

Alisema Serikali itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali ili kuboresha mazingira ya kazi kwa watumishi wa ubalozi na kuhakikisha mali zake zinatumika kwa tija.

Aidha, Balozi Mussa alitembelea pia kiwanja kinachomilikiwa na Serikali ya Tanzania nchini Malawi na kutoa wito wa kukitumia kiwanja hicho kwa njia inayoweza kuleta manufaa kwa Taifa.

Alibainisha kuwa kuna fursa ya kukiendeleza kiwanja hicho kwa kujenga miundombinu ikiwemo majengo ya biashara au makazi ya kupangisha, jambo ambalo litaongeza mapato ya serikali na kunufaisha Tanzania kwa ujumla.

Balozi Mussa amempongeza Balozi wa Tanzania nchini Malawi, Mhe. Agnes Kayola na watumishi wa Ubalozi huo kwa kazi kubwa wanayofanya ya kuiwakilisha nchi na kusimamia maslahi ya Watanzania wanaoishi na kufanya shughuli zao nchini humo.

Amesisitiza kuwa serikali itaendelea kuwaunga mkono ili waendelee kutekeleza majukumu yao kwa tija na ufanisi.

Balozi Mussa yupo nchini Malawi kwa ajili ya kushiriki Mkutano wa Sita wa Tume ya Pamoja ya Kudumu ya Ushirikiano kati ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Jamhuri ya Malawi utakaofanyika Februari 25, 2025 katika ngazi ya Maafisa Waandamizi, na Mkutano ngazi ya Mawaziri unatarajiwa kufanyika Februari 26, 2025.

Related Posts