Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Umoja wa Walimu Wasiokuwa na Ajira Tanzania kuanzia mwaka 2015 hadi 2023 (Neto), Joseph Kaheza anadaiwa kutiwa mbaroni na Polisi mkoani Geita.
Chanzo cha Kaheza kukamatwa kinatajwa kuanzisha vuguvugu la kuishinikiza Serikali kuwapatia ajira.
Taarifa za kukamatwa kwake, zimethibitishwa na Katibu wa umoja huo, Daniel Edgar baada ya kupata taarifa hizo kutoka kwa mjomba wake, Barnabas Daud aliyekuwa naye wakati tukio hilo linatokea.
“Alikamatwa jana jioni akiwa nyumbani kwake Geita na anashikiliwa kituo cha Polisi Geita Mjini, amekamatwa katika kipindi ambacho tulikuwa hatua za mwisho kwenda Dodoma kufanya mazungumzo na Serikali juu ya kujua hatima yetu,” amesema.
Daud amekiri kukamatwa kwa ndugu yake huyo akiwa kwenye shughuli zake za ujasiriamali, huku akieleza alikuja kukamatwa na askari wengi waliokuwa wamevalia nguo za kiraia na silaha za moto.
“Ingawa walivaa nguo za kiraia baadhi ya askari waliomkata nawafahamu, nimeshawahi kufanya nao kazi katika mgodi wa GGM, walikuwa wengi na walikuwa na gari mbili aina ya teksi zote ni za kiraia zikiwa na vioo vya ‘tinted’ ‘,” amesema.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Geita, Hashim Komba alipotafutwa leo Jumanne, Februari 25, 2025 saa 4:22 asubuhi kuhusu kushikiliwa kiongozi huyo amejibu: “Yeye si msemaji wa Jeshi la Polisi.”
Mwananchi limemtafuta Komba baada ya Polisi Mkoa wa Geita kutafutwa tangu jana hadi asubuhi ya leo Jumanne pasipo mafanikio. Ingawa vyanzo vya ndani Polisi mkoani humo vinadai vitatoa taarifa baadaye.
Daud katika maelezo yake amesema baada ya kumkamata walimfunga pingu na alipowauliza sababu ya kukamatwa kwake mmoja wa askari aliyekuwa amekaa mbele ya gari iliyombeba akiwa na bastola alimjibu, “kwani na wewe ni mtuhumiwa? Ndugu yako atajua makosa yake hukohuko tunakompeleka.”
“Nilipowaomba vitambulisho walikataa kunionyesha nikawaomba waniambie ndugu yangu wanampeleka wapi? Walinipatia namba ambayo hata nikipiga haipatikani wakaomba ya kwangu wakanipigia kisha nikasevu,” amesema.
Amesimulia wakati wanataka kuondoka aliwaomba waondoke wote lakini walimkatalia kwa kile walichomueleza hata wakati wanakuja kumkamata eneo hilo, hawakuwa naye na hawakumpigia simu.
“Walipoondoka waliniambia ndugu yangu nitamkuta ofisi ya RCO, baadaye nilipoenda ofisi hiyo nilikutana na askari mwingine ambaye namfahamu pia akiwa amevaa sare tuliongozana kuzunguka selo zote hawakumuona nikatoka kwa unyonge kweli,” amesema.
Amesimulia baadaye alimtafuta askari aliyempatia namba wakati anamkamata kila alipokuwa anapiga namba hiyo ilikuwa haipatikani ndipo alipojaribu kutuma ujumbe mfupi na baada ya muda alipigiwa simu kwamba ndugu yake anahojiwa.
“Anahojiwa kituo cha Polisi Geita Mjini nilipofika nikaambiwa yupo na hawezi kuongea na mimi na wakanitaka niondoke na akitoka watanipigia simu na nikaanza kuwapigia simu ndugu zangu ili kama akipotea tujue kwa kuanzia,” amesema.
Katika maelezo yake, Daud amesema ndugu yake huyo bado anashikiliwa katika kituo hicho cha polisi, “hata asubuhi ya leo (saa 3 asubuhi) tupo hapa kwenye kituo cha Polisi tumeleta chai na tumewaomba tuongee naye tumejibiwa tusubiri.”
Katika hatua nyingine, Katibu wa Neto, Edgar amesema sababu ya kukamatwa kwa kiongozi wao amedai ni mkutano walioufanya Februari 21, 2025 katika Hoteli ya Land Mark Ubungo jijini Dar es Salaam kuishinikiza Serikali wapatiwe ajira.
“Tunataka tupatiwe ajira bila masharti ya kufanya usaili kwani wakati Serikali inasitisha mpango wa kutoa ajira mwaka 2015 walituahidi wakimaliza kutoa watumishi hewa wataanza kuajili lakini imekuwa kimya,” amesema.
Amesema hata ajira walizozitoa hivi karibuni zimekuwa na masharti mengi ikiwemo kuweka kiwango cha umri kwa wanaotaka kuomba ajira, lakini hata mtihani waliopewa ulikuwa na maswali 25 ambayo hayahusiani kabisa na taaluma waliyosomea.
Edgar amesema baada ya kufanya mkutano huo na vyombo vya habari Serikali iliwapigia simu waende Dodoma kufanya mazungumzo wakiwa kwenye hatua za mwisho kiongozi wao huyo alikamatwa.
“Tumeshaijibu Serikali hatuwezi kwenda kufanya mazungumzo wakati kiongozi wetu amekamatwa, tumewaambia aachiwe ndipo tutakuwa tayari kwenda kufanya mazungumzo hayo,” amesema Edgar.
Endelea kufuatilia Mwananchi kwa habari na taarifa mbalimbali