Mashahidi waeleza walivyobaini mabaki ya mwili wa Josephine

Moshi. Mashahidi wa Upande wa Jamhuri katika kesi ya mauaji ya kukusudia inayomkabili, Josephine Mngara (30), aliyeuawa kwa kuteketezwa kwa moto, wameieleza Mahakama namna walivyobaini uwepo wa mabaki ya mwanadamu.

Mbali na mashahidi hao, daktari aliyeuchunguza mwili huo, ameeleza ulikuwa ni mkaa isipokuwa sehemu ya nyuma ya kichwa, mapafu na moyo, misuli ya makalio na sehemu ya nyonga ambayo ilionyesha sehemu ya siri ya jinsia ya kike.

Kesi hiyo ilianza kusikilizwa jana Jumatatu, Februari 24, 2025 mbele ya Jaji Adrian Kilimi wa Mahakama Kuu Kanda ya Moshi, huku upande wa mashitaka ukiongozwa na Wakili Mwandamizi wa Serikali, Kambarage Samson, akishirikiana na Frank Ong’eng’a na Grace Kabu.

Mbali na mawakili hao, lakini utetezi katika kesi ya mauaji namba 3382/2024, inayowakabili washtakiwa wawili, Erasto Mollel na Samwel Mchaki, unawakilishwa na mawakili wa kujitegemea, Alfredy Sindato Silayo na Lilian Mushi.

Washtakiwa hao kwa pamoja, wanashtakiwa kwa tuhuma za kumuua kwa makusudi, mwanamke huyo eneo la Mtemboni, Mji mdogo wa Himo, Wilaya ya Moshi, mkoani Kilimanjaro, Februari 19, 2023 kwa kumteketeza kwa moto.

Marehemu alikuwa akiishi na Mollel ambaye alikuwa ni mpenzi wake na aliuawa kikatili usiku wa kuamkia Februari 19, 2023 na mwili wake kuteketezwa kwa moto kwenye pagale kwa kile kilichodaiwa na Polisi kuwa ni wivu wa mapenzi.

Mabaki ya mwili huo wa marehemu yalikaa chumba cha kuhifadhia maiti Hospitali ya KCMC kwa zaidi ya siku 190 mpaka mwili huo ulipokabidhiwa kwa familia Agosti 26, 2023 na kwenda kuyazika usiku kwenye makaburi ya Mji mdogo wa Himo.

Shahidi wa kwanza ambaye ni Balozi wa Mtaa wa Mtemboni, Delineva Sam ameeleza, Februari 19, 2023 saa 10 usiku akiwa nyumbani kwake, aliona moto unawaka nyumba ya jirani.

Akiongozwa na mawakili wa Serikali kutoa ushahidi wake, Delineva aliiambia Mahakama, baada ya kuona moto huo alimpigia simu jirani yake, aitwaye Samwel Sam kumtaarifu kuhusu moto huo ili waongozane kwenda eneo la tukio.

“Nilimpigia simu jirani yangu nikamwambia mbona naona moto unawaka nyumba ya jirani? alikata simu kisha akanirudia, akasema ni kweli kuna moto, hivyo akaniambia niende na ndoo yenye maji,” ameeleza shahidi huyo wa Jamhuri.

Amesema alipofika eneo la tukio alimkuta mwenzake ametangulia na ameshaanza kuuzima ule moto huku akiendelea kupiga yowe kuomba msaada zaidi.

“Wakati tunaendelea kuzima moto, mwenzangu akaniambia mbona huu moto sio wa kawaida? siuelewi, baadaye tuliona kitu kama mguu wa binadamu wakati tunaendelea kuuzima moto,” ameendelea kueleza shahidi huyo.

Shahidi huyo amedai baada ya kuona kwenye ule moto kuna mwili wa binadamu unaungua, alimpigia simu mwenyekiti wa mtaa na ndipo alipofika eneo la tukio akiwa ameongozana na watu wengine waliojitokeza kutoa msaada.

Amedai baada ya moto ule kuzima na mwenyekiti kufika eneo la tukio aliwapigia simu askari na walipofika na kukuta ni mwili wa binadamu, walichukua mifupa na kuweka kwenye mfuko wakaondoka nayo.

Shahidi huyo ameeleza, kesho yake Februari 20, 2023 walipata taarifa kwamba kuna mtoto wa mama aitwaye mama Martha haonekani (marehemu) ambapo Polisi walirudi tena eneo la tukio Februari 21,2023.

“Wale askari walikwenda kwenye chumba alichokuwa akiishi marehemu na mume wake, tukakuta damu zimemwagika kwenye kitanda, chini kwenye sakafu na panga lenye damu kwenye kile chumba na godoro likiwa limeondolewa,” amedai.

Shahidi wa pili katika kesi hiyo, Samwel Sam, ambaye ni jirani, ameieleza Mahakama hiyo kuwa, baada ya kufika eneo la tukio na kuanza kuzima moto kwenye nyumba hiyo ambayo ilikuwa haiishi mtu (pagale) kuna chumba kimoja kilikuwa na moto mkali sana na ndipo alipoongeza nguvu kuuzima moto ule.

Kulingana na shahidi huyo, wakati anazima ule moto, aliona mguu, mbavu na fuvu la kichwa cha binadamu na ndipo yeye na balozi wa hilo eneo waliwatafuta viongozi wa eneo hilo akiwemo mwenyekiti wa mtaa ambaye alifika na kuwapigia simu askari Polisi ambao walifika eneo la tukio na kuanza uchunguzi.

Walichokisema mwenye nyumba, mama

Shahidi wa tatu katika kesi hiyo, ambaye ni mwenye nyumba, Godfrey Minja almeieleza Mahakama hiyo, Februari 19, 2023 alipigiwa simu na mwenyekiti wa eneo hilo kumjulisha kilichotokea kwenye nyumba yake.

Ameeleza alifika eneo la tukio siku hiyo alikuta tayari moto umezimwa na mali zake zilizokuwa chumba cha pili zikiwa nazo zimeteketea zote kwa moto.

Shahidi wa nne, Theodora Msuya ambaye ni mama wa marehemu, aliieleza siku iliyofuata baada ya tukio kutokea alifuatwa na mama mmoja akimuuliza kama amemwona mtoto wake (Josephine), ambaye sasa ni marehemu.

“Nilimwambia sijamuona, akaniambia kuna mtu kauawa Mtemboni. Tulienda nyumba aliyokuwa akiishi na kuvunja nyumba, tulikuta damu kwenye chumba na panga, ndipo tulienda kutoa taarifa kituo cha polisi Himo,” ameeleza shahidi huyo.

Shahidi huyo amedai, baadaye aliitwa Kituo cha Polisi Himo ili kwenda kufanya vipimo vya vinasaba (DNA) katika Hospitali ya Faraja iliyopo Mji Mdogo wa Himo, wilaya ya Moshi ambapo aliongozana na maofisa wawili wa polisi.

 Mtaalamu wa maabara, daktari

Shahidi wa tano katika kesi hiyo, ambaye ni mtaalamu wa maabara katika hospitali ya Faraja, Christopher Mariki amedai kuwa Februari 22, mwaka 2023 walifika maofisa wawili wa polisi wakihitaji huduma ya kuchukua sampuli ya DNA.

Askari hao walikuwa wameambatana na mwanamke mmoja, ambapo walimpa maelekezo kwamba wanataka kuchukua sampuli za DNA kutoka kwa yule mwanamke, akaandaa vifaa vilivyohitajika kuchukua sampuli.

“Nikachukua sampuli za damu baadaye niliziweka alama, nikakabidhi kwa maofisa wa polisi na waliondoka nazo,”ameeleza shahidi huyo.

Shahidi wa saba katika kesi hiyo, kutoka Hospitali ya KCMC, Dk Patrick Ams, ameieleza mahakama hiyo kuwa Februari 23, mwaka 2023 akiwa ofisini alijulishwa na muhudumu wa mochwari kwamba kuna askari wamekuja wanataka kufanya uchunguzi mwili wa marehemu.

“Askari waliuonyesha mwili ambao walitaka ufanyiwe ‘postmortem’ ili kutambua chanzo cha kifo kimesababishwa na nini,” amedai daktari huyo.

Shahidi huyo, ameeleza mwili huo ulikuwa umeungua sana na ulikuwa ni mkaa isipokuwa sehemu ya nyuma ya kichwa, mapafu na moyo, misuli ya makalio na sehemu ya nyonga ambayo ilionyesha sehemu ya siri ya jinsia ya kike.

Kwa mujibu wa shahidi huyo, amedai kuwa, walichukua sampuli na kuufanyia mwili huo uchunguzi na baadaye walikabidhi sampuli hizo kwa askari na kuweka lebo kwa maana ya jina la utambuzi wa sampuli hiyo.

“Baada ya uchunguzi kukamilika niliandika ripoti nikakabidhi kwa askari anayesimamia uchunguzi,” amedai daktari huyo ambaye ni bingwa wa magonjwa ya binadamu na kuomba Mahakama ipokee kielelezo hicho.

Kielelezo hicho kilipokelewa mahakamani hapo na Jaji Adrian Kilimi wa Mahakama Kuu Kanda ya Moshi, Mkoani Kilimanjaro ambaye ndiye anayesikiliza kesi hiyo.

Shahidi wa sita, katika kesi hiyo, ambaye ni mpelelezi wa makosa ya jinai, Kituo cha Polisi Himo, Koplo Athuman ameieleza Mahakama hiyo kuwa, Mei 16, 2023 alipata taarifa kutoka kwa msiri wake kwamba mtuhumiwa wa mauaji hayo, Erasto Mollel ameonekana Mtaa wa Zilipendwa katika mji wa Himo.

“Nikiongozana na maofisa wenzangu tulielekea mtaa wa Zilipendwa na kumkuta mtuhumiwa amekaa juu ya kiti, tulimweleza kosa lake na kumuweka chini ya ulinzi, tuliondoka naye hadi kituoni (kituo cha Polisi Himo).

Kesi hiyo inaendelea kusikilizwa leo ambapo mashahidi wengine watano wa upande wa mashitaka wataendelea kutoa ushahidi wao.

Related Posts