Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu-Kazi , Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Ridhiwani Kikwete amezindua miradi ya Elimu, Umeme na barabara yenye thamani ya shilingi bilioni 1.6 katika Halmashauri ya wilaya ya Songwe mkoani Songwe
Akiongea wakati wa uzinduzi wa Miradi hiyo tarehe 24 Februari 2025, amesema Mradi wa Ujenzi wa shule ya Maweni B ambao umegharimu shilingi milioni 583 utasaidia kuondoa adha ya kutembea umbali mrefu kwenda shule kwa watoto wa Mkwajuni, kupunguza msongamano darasani pamoja na utoro wa rejareja.
Mhe.Kikwete amezindua pia madarasa Sita yatakayotumika kwa kidato cha Tano na Sita katika shule ya sekondari Kanga. Mradi huo wenye thamani ya shilingi milioni 150 utawezesha pia vijana kuishi bweni na kuboresha mazingira ya malazi na Ujifunzaji kwa wanafunzi.
Amezindua ujenzi wa barabara za Mkwajuni mjini kwa Kiwango cha lami wenye thamani ya shilingi milioni 760, Mhe. Kikwete amempongeza Mbunge wa jimbo la Songwe, Mhe. Philipo Mulugo kwa kuelekeza kiasi cha shilingi Milioni 500 za mfuko wa maendeleo ya Jimbo kwa ujenzi wa miundombinu ya barabara.