Kocha Tanzania Prisons akataa unyonge

ACHANA na kupoteza mechi tatu mfululizo, Kocha Mkuu wa Tanzania Prisons, Aman Josiah amesema hatarajii wachezaji wake kurudia makosa wakati wakiivaa Fountain Gate leo akisisitiza pointi muhimu.

Prisons inatarajia kuwa ugenini kukipiga dhidi ya wapinzani hao mchezo ukipigwa Uwanja wa Kwaraa huko mkoani Manyara ukiwa wa raundi ya 22, huku kila timu ikihitaji pointi tatu kujiweka pazuri.

Timu hizo zinakutana ikiwa Maafande hao wanakumbuka ushindi wa mabao 3-2 katika mchezo wa mzunguko wa kwanza walipokuwa nyumbani Sokoine na kufanya mechi ya leo kuwa visasi na rekodi.

Hata hivyo, Prisons haijapata ushindi kwenye michezo minne mfululizo, ikipoteza mitatu dhidi ya Simba 3-0, Namungo 1-0 na Dodoma Jiji 3-2 na sare ya 1-1 mbele ya Tabora United.

Pia katika michezo mitano nyuma, timu hiyo imeruhusu bao ikifungwa jumla mabao tisa na kuwa nafasi ya 14 kwa pointi 18, ambapo leo itatafuta ‘cleensheet’ ya pili chini ya kocha huyo.

Kwa upande wa Fountain Gate nao hawajawa na mwenendo mzuri baada ya kucheza michezo minane bila kuonja ushindi ikiwa ni sare mbili na kupoteza sita na kuwa nafasi ya 13 kwa pointi 22.

Josiah alisema mechi hiyo itakuwa ngumu lakini matarajio yake ni kushinda baada ya kupitia kipindi kigumu, akitamba kuwa makosa yaliyoonekana michezo iliyopita hatarajii kujirudia.

“Zaidi ni tunaangalia pointi tatu kwakuwa tumekosea mara kadhaa, tumesahihisha makosa yaliyoonekana, tunafahamu wapinzani nao wamejipanga lakini tutakuwa makini dakika zote 90,” alisema kocha huyo.

Related Posts