Mbeya. Mahakama imeamuru kusikilizwa upya kwa kesi ya mauaji dhidi ya mkazi wa Limseni wilaya ya Mbarali, Silivanus Nyaululi, anayedaiwa kumuua mtoto wake mwenye umri wa mwaka mmoja kwa kumkatakata kwa panga na kumzika.
Awali, Nyaululi aliomba kukiri kosa dogo la mauaji ya bila kukusudia na Mahakama ikaridhia baada ya upande wa Jamhuri kutokuwa na kipingamizi, hivyo kuhukumiwa kifungo cha maisha jela, lakini akakata rufaa kupinga adhabu hiyo.
Lakini wakati anakiri kosa hilo, Nyululi alikuwa akikabiliwa na makosa mengine mawili ya kujaribu kumuua mkewe, Njendina Kilunduma na mwanaye wa kike, Eliza Nyaululi (3) kwa kuwakata na panga kichwani siku hiyohiyo ya Januari 31, 2017.
Hata hivyo, jana Jumatatu, Februari 24, 2025, Mahakama ya Rufani Tanzania iliyoketi jijini Mbeya, imeamuru kusikilizwa upya kwa shauri hilo baada ya kubaini dosari za kisheria, wakati mshtakiwa alipokubaliwa kukiri kosa dogo la mauaji ya bila kukusudia.
Hukumu hiyo ambayo imewekwa kwenye mtandao wa Mahakama leo Februari 25, 2025, ilitolewa na jopo la majaji watatu ambao ni Winfrida Korroso, Pantrine Kente na Leila Mgonya.
Tukio la mauaji lilivyotokea
Maelezo ya ushahidi ambao ulimtia hatiani na kupewa adhabu ya kifungo cha maisha, yanaeleza siku ya tukio Januari 31, 2017, Nyaululi alidaiwa kusababisha kifo cha mtoto wake Mavuno Nyaululi mwenye umri wa mwaka mmoja.
Inadaiwa alimkatakata kwa panga kichwani kabla ya kumzika katika kibanda ambacho alikuwa akiishi yeye na familia yake na baadaye kujaribu kumuua mkewe, Njendina na mtoto wao mwingine, Eliza katika tukio hilohilo la Januari 31.
Ilielezwa na upande wa mashitaka kuwa usiku wa siku hiyo ya tukio, mshtakiwa alipofika nyumbani alimkuta mkewe amelala pamoja na watoto wao wawili katika kibanda ambacho alikijenga kwenye shamba lake.
Bila kutarajia, mrufani huyo alimweleza mkewe kuwa usiku huo atammaliza (kumuua) na akimaliza kufanya hivyo atawamaliza pia watoto wake hao, kwa hisia kuwa mkewe ana mahusiano ya kimapenzi na kaka wa mshtakiwa.
Ghafla mrufani alishika panga na kumkata mkewe kichwani, usoni na kwenye goti na kuangukia nje ya kibanda wanachoishi akivuja damu nyingi.
Mrufani anadaiwa pia kumkata kichwani mtoto wake aitwaye Eliza kwa kutumia panga hilohilo na kumrusha nje ya kibanda huku mtoto wake mdogo mwenye umri wa mwaka mmoja aliyebakia ndani ya kibanda akilia, kisha akanyamaza.
Kulingana na maelezo hayo, mshtakiwa huyo alitoweka eneo hilo na kwenda kusikojulikana ambapo siku iliyofuata taarifa ziliufikia uongozi wa kijiji na baadhi ya viongozi wa kijiji walifika katika eneo ambalo tukio lilitokea.
Walimkuta mke wa mshtakiwa na mtoto wake wakiwa wamejeruhiwa vibaya na kwa kuwa mtoto yule mdogo alikuwa haonekani, walianza kumtafuta ndani ya kibanda na kubaini eneo ambalo kulikuwa na mchanga mbichi.
Baada ya upekuzi wa kina, waligundua mwili wa mtoto huyo ukiwa na majeraha mabaya ya kukatwa na kitu chenye ncha kali, ukiwa umezikwa ndani ya kibanda ambapo majeruhi wote walipelekwa hospitali kwa ajili ya matibabu.
Mshtakiwa alivyonaswa kwenye Pub
Taarifa za tukio la mauaji na shambulio dhidi ya mke na mtoto, zilitolewa kituo cha Polisi Rujewa ambao walianza kumsaka mtuhumiwa na kumkamata katika eneo la kuuza vinywaji (Pub) huko Igawa, Mbarali akinywa pombe.
Mshtakiwa alitiwa nguvuni na kufunguliwa mashitaka ya mauaji ya kukusudia na baada ya kusomewa shitaka hilo mbele ya Jaji Lilian Mongella ambapo alikana kosa hilo na pia mashitaka mawili ya kujaribu kuua.
Kulingana na maelezo yaliyochambuliwa na majaji hao, siku kesi hiyo ilipoitwa kwa ajili ya kusikilizwa, alisomewa tena makosa yanayomkabili akakanusha kutenda makosa, lakini baadaye akaomba kukiri kosa dogo la kuua bila kukusudia.
Lakini akaomba asomewe upya kosa la pili na la tatu ambayo yalikuwa ni ya kujaribu kuua kwa vile pia alikuwa anataka kukanusha mashitaka.
Kwa kuwa maombi hayo hayakupingwa na upande wa Jamhuri, Mahakama ilikubali maombi hayo na kumbukumbu za rufaa katika ukurasa wa 25, mashitaka ya mauaji ya kukusudia yalibadilishwa na kuwa kosa la kuua bila kukusudia.
Mshtakiwa akasomewa maelezo yanayohusiana na kosa la mauaji ya kukusudia pamoja na kujaribu na kukiri makosa yote hayo matatu kwa pamoja na kutokana na kukiri kwake, Mahakama ikamhukumu kutumikia kifungo cha maisha jela.
Mshtakiwa huyo ambaye aliwakilishwa kortini na wakili wa Mahakama Kuu, Caroline Mseja, hakuridhika na adhabu aliyopewa Mahakama Kuu na hivyo kuwasilisha sababu nne za rufaa na baadaye kuongeza sababu nyingine mbili.
Akijenga hoja katika sababu ya kwanza, wakili Mseja alisema baada ya hati ya mashitaka ya mauaji ya kukusudia ilipobadilishwa na kuwa mauaji ya bila kukusudia na kukiri makosa yote, mrufani hakueleza ni kosa lipo amekiri.
Wakili huyo alisema kukiri kwake hakuonyesha kama alielewa msingi wa hati ya mashitaka kubadilishwa na kusomewa upya shitaka la kuua bila kukusudia, na kutoa mifano ya maamuzi ya kesi akisema taratibu hazikuwa zimefuatwa.
Katika hoja ya pili ya rufaa, wakili huyo akaeleza kuwa mrufani hakusomewa vielelezo vyote vilivyotolewa na kupokelewa mahakamani wakati huo wa usikilizaji kama kielelezo kinyume cha taratibu, akitaka upokeaji wake ufutwe.
Akijibu hoja hizo, wakili mwandamizi wa Serikali, Caroline Matemu aliyesaidiwa na wakili wa Serikali Lordgerd Eliaman, aliunga mkono kutiwa kwake hatiani na adhabu aliyopewa na kusema ni mrufani mwenyewe alikiri makosa yote matatu.
Hata hivyo, alisema wameshindwa kuona katika kumbukumbu za kesi hiyo hati mpya ya mashitaka ya kuua pasipo kukusudia baada ya shitaka la mauaji kubadilishwa, na kuiomba Mahakama iamuru kesi hiyo isikilizwe upya.
Katika hukumu yao, majaji wa Mahakama ya Rufaa walisema katika kuamua rufaa hiyo, watajikita katika mapungufu ya kisheria yaliyojitokeza kutokana na hoja za wakili wa Serikali juu ya kutoonekana kwa hati mpya ya mashitaka iliyobadilishwa.
Majaji hao walisema ni sahihi alichokisema wakili wa Serikali kwamba hakuna ubishi kuwa si hati mpya ya mashitaka ya kuua bila kukusudia, au maelezo ya kosa la kuua bila kukusudia yalikuwa yanaonekana katika kumbukumbu za Mahakama.
“Ni wazi kuwa katika mazingira kama hayo, hati ya mashitaka ya mauaji ya bila kukusudia dhidi ya mrufani na maelezo hayajulikani mbele ya Mahakama,” walieleza majaji hao,” walieleza majaji hao katika hukumu yao na kuongeza;-
“Kwa hiyo kutiwa kwake hatiani na adhabu dhidi ya mrufani inabaki kuwa haieleweki bila uwepo wa hati hiyo mpya ya mashitaka ya kuua bila kukusudia ili kuichambua. Hoja hapa ni tunaendaje katika mazingira haya”
Wakiegemea misimamo iliyopo katika mashauri mengine yanayofanana na shauri hilo, majaji hao walisema kwa kutazama kumbukumbu za shauri hilo haikuwa wazi ni kifungu gani cha kanuni ya adhabu alichoshtakiwa nacho na kutiwa hatiani.
“Kwa hicho tulichokibaini, ni maoni yetu kuwa kwa mazingira tuliyonayo, sio upande wa mashitaka wala wa mrufani wa kulaumiwa. Wala hatuna uhakika kama mrufani alitendewa haki wakati wa usikilizaji kwani kutiwa kwake hatiani si salama.”
Kutokana na mazingira hayo ya kukosekana kwa hati mpya ya mashitaka iliyobadilishwa kutoka mauaji ya kukusudia hadi mauaji ya bila kukusudia, tunaona Jamhuri wanapaswa kupewa nafasi kuendesha kesi dhidi ya mrufani.
Majaji hao wakatoa amri kuwa jalada la shauri hilo lirudishwe mara moja kwa mahakama iliyosikiliza shauri hilo ili kuendelea na kesi kuanzia pale kabla mshtakiwa hajasomewa hati mpya ya kosa la mauaji ya bila kukusudia.
Kwa kuzingatia muda ambao mrufani ameshakaa mahabusu, usikilizwaji wa shauri hilo ufanyike kwa haraka na kama itatokea mrufani atatiwa tena hatiani, basi muda ambao atakuwa ameutumia gerezani uondolewe kwenye adhabu.
Katika kipindi mchakato huo ukiendelea, mshtakiwa ataendelea kuwa mahabusu.