Dar es Salaam. Baadhi ya wahubiri wanapotekeleza majukumu yao ya kuhubiri neno la dini wamekuwa wakibadili sauti, huku wengine wakitumia nguvu kuzungumza.
Watumishi hao wa Mungu hufanya hivyo kwa muda mrefu pasipo kujua iwapo kuna athari za kiafya wanazoweza kupata.
Daktari bingwa wa koo katika Hospitali ya St Bernard, Daniel Massawe, anasema kubadilisha sauti kwa viwango vya juu au kwa muda mrefu kunaweza kusababisha uchovu wa misuli ya koo, kuvimba kwa nyuzi za sauti na hatimaye kupoteza sauti kwa muda.
“Wachungaji wanaotumia nguvu nyingi kwenye sauti kwa muda mrefu bila mapumziko wanakabiliwa na tatizo la uchovu wa nyuzi za sauti. Hali hii husababisha sauti kuwa dhaifu, kupoteza nguvu au hata kukauka kabisa na kuhitaji mapumziko ya siku kadhaa ili irejee katika hali ya kawaida,” anasema.
Anasema matumizi ya sauti kwa nguvu kupita kiasi husababisha shinikizo kwenye misuli ya koo, jambo linaloweza kuleta maumivu makali na kufanya mhubiri ahisi ugumu wa kumeza au kuzungumza.
Dk Massawe anasema kubadilisha sauti kwa nguvu au kupiga kelele mara kwa mara husababisha uvimbe kwenye nyuzi za sauti. Hali hii inaweza kuleta matatizo makubwa ya kupumua na hata kuhitaji matibabu maalumu.
“Misuli ya sauti inafanya kazi kama misuli mingine mwilini. Ikiwa inachoka au inachochewa kupita kiasi, inaweza kupata madhara ya kudumu. Ndiyo maana baadhi ya wahubiri hujikuta wakipata sauti mbaya au kuvimba kwa koo mara kwa mara,” anasema.
Anasema kupaza sauti kupita kiasi kwa muda mrefu kunawaweka katika hatari ya kupata vinyama vidogo kwenye nyuzi za sauti.
Hali hiyo, anaeleza, husababisha sauti kuwa na mikwaruzo, kupoteza uwezo wa kupanda au kushuka, na wakati mwingine inaweza kuhitaji upasuaji ili kuondoa uvimbe.
Anaeleza kuwa kubadili sauti kwa nguvu kunahitaji matumizi makubwa ya hewa, jambo linaloweza kuathiri mfumo wa kupumua, hivyo mhusika anaweza kukabiliwa na matatizo ya upumuaji na athari kwenye mapafu.
“Kupaza sauti kunaweza kusababisha upungufu wa hewa, hali inayofanya mhubiri ahisi kama anataka kuzimia, hasa anapokuwa anahubiri kwa muda mrefu bila mapumziko,” anasema.
Anaeleza pia kuwa kuna uwezekano wa kuathiri utendaji wa mapafu kwa wale wenye matatizo ya kiafya kama pumu au mzio wa hewa.
Akizungumzia hilo, Anna Mrope, muumini wa kanisa moja jijini Dar es Salaam, anasema wahubiri wanapokuwa katika hali hiyo kiroho huwafanya waumini kuhisi nguvu ya maombi.
“Tunapokuja kanisani, tunataka mahubiri yenye nguvu, lakini pia tunataka kuona uhalisia. Sauti ikienda juu sana au kubadilika, inaweza kuonekana kama maigizo badala ya ujumbe wa kweli,” anasema.
Mchungaji wa Kanisa la Christian, John Lukindo, anasema ubadilishaji wa sauti ni mbwembwe ambazo hazina maana bali ni kuongeza vionjo vya mahubiri.
“Kwa sasa imekuwa kama mtindo kwa baadhi ya wahubiri kubadili sauti na kuhisi kuwa akifanya hivyo ndiyo upako unashuka na waumini kumuamini kuliko anayeongea kwa sauti ya kawaida,” anasema.
Anasema kuna makanisa yenye waumini wengi, lakini katika mahubiri hutumia sauti ya kawaida kwa kuwa kinachoangaliwa ni neno na si kelele.
“Nasema hayo ni maigizo. Ni kama mtoto amuone mwenzake anaongea au amezaliwa na jambo fulani, akafikiri ndivyo inavyopaswa kuwa, na kuanza kuiga. Ndicho kilichotokea kwa wachungaji wengi,” anasema.
Amesema wapo marafiki zake waliokuwa na sauti za kawaida, lakini sasa wamebadilika na hawawezi kurudi katika hali yao ya kawaida, jambo ambalo anafikiri ni hatari kiafya.
Mchungaji na Mratibu wa Vijana wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Frank Mng’ong’o, anasema wanaobadili sauti wajue kuwa kuna madhara, kwani nguvu wanayotumia wanajikuta wanaendelea nazo hadi kwenye familia.
“Katika hali ya kawaida, mtu anayeiga sauti anajikuta anazoea kupiga kelele hata akiwa nyumbani na kuwa kero kwa wengine, hali inayoweza kusababisha madhara mengine kwa familia,” anasema.
Anashauri wahubiri watumie sauti walizopewa na Mungu, kwani waumini wanaelewa hata ikitumika sauti ya kawaida.
“Tunapaswa kuwa waangalifu tusije tukabadilisha injili kuwa burudani. Sauti ni nyenzo, lakini ujumbe ndio jambo la msingi,” anasema.