TPA yataja mkakati wa kukabiliana na foleni ya malori bandarini

Dodoma. Kilio cha wafanyabiashara na wamiliki wa malori kuhusu msongamano bandarini kimeiamsha Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) ambayo imepanga mkakati maalumu ya kukabiliana na changamoto hiyo.

Msongamano huo unaolalamikiwa ni unaosababishwa na ongezeko la idadi ya makontena na bidhaa zinazohudumiwa bandarini.

Kwa mujibu wa TPA miongoni mwa mikakati hiyo ni ujenzi wa kituo cha reli na mtandao wake, mradi ambao unatarajiwa kugharimu jumla ya Sh308.6 bilioni.

Mradi huu unatarajiwa kupunguza msongamano wa malori kwa kiasi kikubwa na kuboresha usafirishaji wa bidhaa kutoka bandari.

Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Plasduce Mbossa, akizungumza na waandishi wa habari amesema mradi wa ujenzi wa kituo cha reli na mtandao wake utasaidia kuboresha usafiri wa shehena kwa kupunguza utegemezi wa barabara.

“Kwa sasa, asilimia 98 ya shehena inayotoka bandarini hutegemea barabara, jambo ambalo limechangia kwa kiasi kikubwa foleni ya malori ndani na nje ya bandari.

“Mradi huu unapotarajiwa kukamilika, utatoa fursa ya kupunguza matumizi ya barabara na hivyo kupunguza msongamano,” amesema.

Amesema mradi mwingine wa kimkakati ambao TPA inatekeleza ni wa kupokelea na kuhifadhia mafuta (SRT), ambao umekamilika kwa asilimia 17 na unagharimu Sh681.8 bilioni.

Mbossa amefafanua mradi huo unatarajiwa kupunguza muda wa kuhudumia meli zenye ujazo wa 150,000 DWT kutoka siku 10 hadi tatu, jambo litakalosaidia kuongeza ufanisi katika sekta ya usafirishaji wa mafuta.

Mbossa pia amezungumzia mapato ya bandari kwamba yameongezeka kwa kiasi kikubwa, kutoka Sh1.1 trilioni mwaka 2021/22 hadi Sh1.4755 trilioni mwaka 2023/24.

Amesema mchango wa sekta ya bandari katika pato la Taifa umeongezeka, na sasa unafikia Sh10.8 trilioni, sawa na asilimia 7.3 ya pato la Taifa.

Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Kariakoo jijini Dar es Salaam, Severine Mushi amesema suala la ucheleweshaji wa mizigo bandarini ni kama limekwisha baada ya mfumo (system) kuwa sawa kwa asilimia 96.

Hata hivyo, amesema kuwa bado msongamano ni changamoto hivyo  Serikali iangalie jinsi watakavyoweza kuupunguza kwa kuwa malori hukaa kwa siku mbili kutokana na shida hiyo.

Mwenyekiti wa Wamiliki wa Malori Tanzania, Machuuki Msamba amesema wanaendelea na mchakato wa kuhakikisha kuwa foleni bandarini inapungua kwa kushirikiana na mamlaka husika.

Related Posts