Makatibu wakuu SADC wajifungia siku mbili kujadili mgogoro wa DRC

Dar es Salaam. Makatibu wakuu kutoka nchi 16 za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), wanatarajiwa kuja na maazimio  ya pamoja yanayolenga  kutafuta suluhu ya mgogoro wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya  Congo (DRC).

Maazimio ya makatibu hao yatawasilishwa kwenye kikao cha mawaziri wa SADC ambao wanatarajiwa kuketi hivi karibuni.

Mbali na mgogoro wa kisiasa wa DRC, kamati  ya kudumu ya makatibu wakuu  hao wanaoshughulikia masuala ya siasa na diplomasia kwa nchi za  SADC watajadili uchaguzi uliofanyika na utakaofanyika kwenye nchi hizo.

Hayo yameelezwa na Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Samwel Shelukindo  leo Februari 25,2025  katika mkutano wake na waandishi wa habari wenye lengo la kuelezea mkutano huo unaoendelea jijini hapa kwa siku mbili Februari 25 na 26.

“Tupo hapa kujadili masuala ya usalama  na siasa na jambo kubwa kwa sasa ni mgogoro uliopo Mashariki kwa Congo kwa hiyo kikao hiki ni cha siku mbili na leo ndio tumeanza, kesho tutatoa taarifa kamili ya mkutano huu, lakini kufanyika kwa mkutano  hapa nchini kuna maana kubwa kwetu,”amesema.

Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,Balozi Samweli Shelukindo akizungumza kabla ya kufungua mkutano wa Makatibu wakuu kutoka nchi 16 za Jumuiya ya Maendeleo kusini mwa Afrika (SADC), jijini Dar es Salaam jana.Picha na Michael Matemanga

Katibu Mkuu huyo amesema matarajio ni viongozi hao kuja na maamuzi ya pamoja yatakayowasilishwa kwenye kikao cha mawaziri masuala ya uchaguzi nayo yakiwa sehemu ya mambo yatakayowasilishwa,  lengo kudumisha amani na kujikita katika ajenda nyingine za maendeleo.

Mkutano huo ni mwendelezo wa juhudi za SADC kuisaka amani Mashariki mwa Congo na Januari 28,2025  Rais Samia Suluhu Hassan ambaye  ni Mwenyekiti wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC-Organ), aliongoza  mkutano wa dharura wa wakuu wa nchi na Serikali wa asasi hiyo.

Lengo la mkutano huo lilikuwa ni kusaka suluhu ya mapigano yanayoendelea kati ya vikosi DRC vya FARDC dhidi ya waasi wa M23.

Rais Samia akifungua mkutano huo alisema Tanzania inaguswa na kukosekana kwa usalama mashariki mwa DRC akisisitiza mgogoro huo si tu unaiathiri DRC, lakini pia, unahatarisha juhudi za mara kwa mara za kuleta utengamano wa kikanda.

“Nchi yangu inaunga mkono kwa dhati jitihada za kidiplomasia zinazoendelea kumaliza migogoro mashariki mwa DRC. Kwa hiyo, tunayataka makundi yote yanayohusika katika mgogoro huo, kushiriki katika majadiliano ili kuleta ustawi wa watu wake na kuleta amani,” alisema Rais Samia.

Related Posts