Dar es Salaam. Wakati baadhi ya wafanyabiashara wakiwa na wasiwasi kuhusu hali ya usalama kuelekea ufanyaji biashara kwa saa 24 katika eneo la Kariakoo jijini Dar es Salaam, Mkuu wa mkoa huo, Albert Chalamila amewaonya vibaka kutothubutu kulifanya eneo hilo sehemu ya majaribio yao.
Chalamila ameyasema hayo leo Jumatatu Februari 24, 2025 alipozindua shughuli za biashara kwa saa 24 kwenye eneo la Karikakoo, hafla iliyofanyika katika Mtaa wa Swahili jijini humo.
Amesema tangu aanze kampeni hiyo ya kuongeza muda wa ufanyajia biashara Kariakoo, watu wengi wamekuwa wakihoji kuhusu uhakika wa usalama katika eneo hilo.
“Naomba niwaondoe hofu na mashaka wananchi na wafanyabiashara nyakati za usiku, nyie fanyeni biashara kwa amani kwa kuwa ofisi yangu pamoja na vyombo vya ulinzi tumejizatiti vilivyo katika kusimamia amani na usalama.

“Katika hili tukibaini kuna mtu yeyote anaelekea kuwa na mkono mwepesi au wenye viashiria vya udokozi, ukibaka, ujambazi, ndani ya siku tano hadi sita atakuwa amepotea kabisa kwenye eneo hili la Kariakoo, kwa sababu hili si eneo la majaribio kwa wezi,” amesema mkuu huyo wa mkoa.
Akieleza sababu ya kutaka Kariakoo kufanya kazi saa 24, Chalamila amesema mbali ya kuongeza mapato na ajira, pia ni kwenda sambamba na maeneo mengine ya kibiashara, ambayo yamekuwa yakifanya kazi saa hizo.
Ameyataja maeneo hayo kuwa ni pamoja na Bandari, Uwanja wa Ndege, Stendi ya Magufuli na treni ya kisasa ya SGR.
“Bandari ya Dar es Salaam baada ya maboresho inafanya kazi saa 24, benki maeneo yale zipo wazi saa zote, hii ni kithibitisho kwamba harakati hizi tunapaswa kuzitumia kama fursa.
“Kwa upande wa usafiri, uwanja wa ndege abiria wanakuja na kuondoka hadi usiku, Stendi ya Magufuli mabasi yanaingia muda wote, treni ya kisasa ambapo watu wanashuka hadi saa sita usiku, hivyo kufanya biashara hadi usiku itasaidia sana kuongeza mapato.
‘Kwa hali hii itakuwa ni aibu kama mfanyabiashara katoka nje ya nchi au mkoani, anafika Dar es Salaam anakuta maduka yamefungwa usiku,” amesema Chalamila.

Akitoa takwimu za mchango wa mapato ya mkoa huo kwa sasa, Chalamila amesema robo tatu ya makusanyo ya Mamlaka ya Mapato Tanzania nchini yanatoka Dar es Salaam, ikiwa ni uthibitisho kuwa wafanyabiashara wengi wanatoka katika mkoa huo.
Pia amesema Shirika la Umeme Tanesco ambalo linaingiza Sh150 bilioni kwa mwezi, kati yake zaidi ya Sh70 bilioni zinatoka Dar es Salaam.
Akizungumzia suakla la usalama, Makamu Mwenyekiti Chama cha Wamachinga, Stephen Lusinde amesema suala la kuimarishwa kwa ulinzi katika eneo ni muhimu kwa kuwa ikitokea, mfano, mgeni akafika Kariakoo na kuibiwa, suala hilo litachafua jina la wafanyabiashara bali na nchi kwa ujumla.
“Sisi tumejipanga kwa kuwa ni fursa kwetu, tunachoiomba Serikali suala la ulinzi litiliwe msisitizo, ili baadaye nchi isije ikachafuliwa sifa yake.
“Ukizingatia kuwa mchana tu vibaka wapo huku tunapambana nao, sasa itakapokuwa biashara inafanyika na usiku nao watatumia kama fursa,” ametahadharisha kiongozi huyo.
Mfanyabiashara wa duka la urembo, Sakina Mushi wa Mtaa wa Msimbazi, amesema ni mapema kwake kujua iwapo atafanya biashara saa 24 baada ya uzinduzi huo, kwani amejipanga kuangalia kwanza namna hali itakavyokuwa na kama hakutakuwa na changamoto zozote naye atakuwa anakesha.

Mamalishe anayefanya shughuli zake Mtaa wa Congo, amesema anaangaalia namna anavyoenda kuongeza wateja nyakati za usiku kwa kuwa aliokuwa nao ni wale wa siku zote, ambao walikuwa wakifanya kazi usiku, haswa makuli na madereva wa daladala.
Akitoa maoni yake kuhusu utaratibu huo, Mhadhiri Mwandamizi Shule Kuu ya Biashara Chuo kikuu cha Dar es Salaam, Dk Winnie Nguni amesema waliokuja na wazo hilo wamelileta katika wakati muafaka, ambapo kwa sasa Watanzania wengi wapo katika kipato cha kati.
“Ili uchumi ukue ni lazima shughuli za kiuchumi nazo zikue, hivyo niwapongeze waliokuja na ubunifu huo wa kuifanya Kariakoo kuwa ya saa 24,” amesema Dk Winnie.
Pia Mhadhiri huyo amesema hapa anaona namna gani hata walio katika ajira rasmi, wanaenda kuongeza kipato chao kwani baada ya kutoka ofisini jioni anaweza kwenda kufanya biashara.
“Utaratibu huu nchi nyingi za Ulaya wanafanya na watu hujikuta wanafanya kazi saa 20, kwa kuwa na kazi tofauti hata nne, hivyo nasi tukiiga hayo hakika tunakwenda kubadili hali za wananchi wetu na nchi kwa ujumla katika mapato,” amesema.
Hata hivyo ili kufanikisha hilo, Dk Winnie ameshauri ziwepo sera zinazovutia ufanyaji biashara.
Pia amesema jamii inapaswa kuelimishwa kuhusu faida na hasara za ufanyaji biashara saa 24 kwa kuwa zipo faida za kiuchumi lakini pia kuna hasara katika masuala ya kijamii, hasa mahusiano ya wanandoa na mazingira katika upande wa upigaji kelele nyakati za usiku.