Goma. Kundi la kwanza la askari wa Jeshi la Ulinzi la Afrika Kusini (SANDF) waliojeruhiwa katika mapigano nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), limeanza kurejea nyumbani kupitia Kigali, Rwanda baada ya kukwama katika kambi zao kwa takriban mwezi mmoja.
Wanajeshi hao ni miongoni mwa askari wa SANDF walioko chini ya Kikosi cha Walinda Amani wa Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SAMIDRC), wanaoimarisha ulinzi Mashariki mwa DRC sambamba na kukabiliana na uovu wa waasi wa M23 dhidi ya raia.
Televisheni ya Afrika Kusini ya SABC imesema, wanajeshi hao ambao walishindwa kupambana na M23 ambao waliitwaa miji ya mashariki mwa nchi hiyo, walionekana wakiondoka Mjini Goma kuanzia juzi jioni kwa barabara bila vifaa na sare zao za kijeshi.
Ripoti ya jarida la Afrika Kusini la Rapport iliyochapishwa Jumapili ilieleza kuwa wanajeshi wa Afrika Kusini waliojeruhiwa ni zaidi ya 189.
Kwa mujibu wa jarida hilo, miongoni mwa waliojeruhiwa ni wanajeshi wawili ambao ni wajawazito, huku idadi ya wanajeshi wa SANDF wanaoendelea kukwama nchini DRC ikikadiriwa kuwa kati ya 1,000 na 2,000.
Katika video zilizopakiwa na waandishi wa habari wa eneo hilo,zinaonyesha wanajeshi walionekana wakiondoka Mjini Goma Jimbo la Kivu Kaskazini na kuingia Rwanda wakiwa wamevalia mavazi ya kiraia.
Chanzo ambacho hakikutaka kutajwa jina lake kimedai kuwa wanajeshi hao walilazimishwa pia kuacha vifaa vyao nyuma. Idadi ya wale wanaohamishwa inaripotiwa kuwa kati ya 90 hadi 300.
“Hawa walikuwa sehemu ya kikosi cha ulinzi wa amani cha Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) katika DRC (SAMIDRC), ambacho kwa sasa kipo kwa jina tu,” kimesema chanzo hicho.
SANDF limeshindwa kutoa tamko kuhusu uondoaji wa waliojeruhiwa.
Waziri wa Ulinzi wa Afrika Kusini, Angie Motshekga, aliambia The Africa Report wiki moja iliyopita kuwa jeshi lilikuwa likiandaa mpango wa kuwaondoa waliojeruhiwa mara tu mipango itakapokamilika.
Haijabainika iwapo makubaliano yoyote yalifikiwa, lakini wiki mbili zilizopita zilishuhudia mazungumzo mfululizo kati ya ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini DRC (Monusco) na SAMIDRC.
Kwa mujibu wa mkataba wa Geneva, hakuna makubaliano yanayohitajika ili kuwaondoa majeruhi kutoka kwenye eneo la vita.
SADC na Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), katika mkutano wa dharura uliofanyika Tanzania wiki mbili zilizopita, ziliwaagiza maofisa wa kijeshi kutafuta suluhisho la mzozo huo.
Hata hivyo, maofisa hao walipokutana jijini Nairobi, Kenya wiki hii, kwa mujibu wa ripoti miongoni mwa maazimio ya mkutano huo ilikuwa ni pamoja na kuitaka Serikali ya Rais Felix Tshisekedi kukaa meza moja na waasi hao, ili kupata mwafaka na kuepusha janga la kibinadamu mashariki mwa nchi hiyo.
Tovuti ya Rapport iliripoti mwishoni mwa wiki kwamba waliojeruhiwa waliambiwa wajitayarishe kuondoka Ijumaa, lakini ilipofika jioni waliambiwa hawakuwa na ruhusa kutoka mwa wapiganaji wa M23 inayowaruhusu kutoka kambini.
Jumapili, akaunti moja inayohusiana na Rwanda kwenye mtandao wa X ilidai kuwa wanajeshi wa SANDF wangerudi nyumbani.
Miili ya wanajeshi 14 wa Afrika Kusini waliouawa wakati M23 ilipoutwaa Mji wa Goma Jimbo la Kivu Kaskazini ilirejeshwa nchini humo wiki moja iliyopita na kufanyiwa maziko ya heshima.
Kumekuwa na shinikizo kubwa kwa Rwanda kusitisha msaada wake kwa waasi wa M23, huku Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa wiki iliyopita likipitisha azimio la kulaani msaada huo.
Hata hivyo, Rwanda kupitia Rais Paul Kagame imekuwa ikikanusha vikali kuwaunga mkono waasi hao huku ikiituhumu DRC kwa kuwakingia kifua waasi wa FDLR, wengi wao jamii ya Kihutu wanaodaiwa kuhusika kwenye mauaji ya kimbari ya mwaka 1994 nchini Rwanda.
Aidha, Waziri wa Mambo ya Nje ya Marekani, Marco Rubio, alisema taifa hilo limeweka vikwazo dhidi ya waziri wa Rwanda anayeshughulikia Uhusiano wa Kanda, James Kabarebe na Msemaji wa Alliance Fleuve Congo (AFC/M23), Lawrence Kanyuka Kingston, kwa madai ya kuchochea vurugu mashariki mwa DRC.
Rwanda ilipinga vikwazo hivyo ikivitaja kuwa visivyo na msingi.
Imeandikwa na Mgongo Kaitira kwa msaada wa Mashirika.