Twiga Stars ni jasho dakika 90

TIMU ya Taifa ya wanawake ‘Twiga Stars’ kesho itashuka uwanjani ugenini dhidi ya Equatorial Guinea, katika mchezo wa kufuzu kwa fainali za Mataifa ya Afrika kwa Wanawake (WAFCON) 2026 zitakazofanyika Morocco.

Huu utakuwa mchezo wa pili baada ya ule wa kwanza Stars ikiwa nyumbani Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, chini ya Kocha Bakari Shime kushinda mabao 3-1, yaliyofungwa kipindi cha pili na Stumai Abdallah na Enekia Lunyamila waliongia wakitokea benchi na lile la tatu la Diana Msewa.

Stars ikifuzu fainali hizo, itaungana na timu nyingine za taifa za Tanzania zilizofuzu kwenye mashindano makubwa ya Afrika, Taifa Stars iliyofuzu Afcon, 17 Serengeti Boys iliyofuzu Afcon U17 na Ngorongoro Heroes Afcon U20.

Mchezo huo wa Stars wa raundi ya kwanza imebakisha hatua moja tu kufuzu raundi ya pili kutoikana na ushindi wa nyumbani na  ikivuka itakutana na mshindi kati ya Uganda ambayo ilipata ushindi kwenye mchezo wa kwanza 2-0 dhidi ya Ethiopia.

Matumaini makubwa kwa Stars yapo kwa washambuliaji wake, Stumai ambaye ndiye kinara wa ligi kuu akiwa na mabao 18, Opah Clement aliyetambulishwa hivi karibuni na FC Juarez ya Mexico, Winifrida Gerald wa JKT Queens, ambao wanaweza kubadilisha taswira ya mchezo kwa kufunga mabao.

Hata hivyo, pamoja na safu bora ya ushambuliaji, Stars inapaswa kuwa makini na washambuliaji wa Equatorial Guinea ambao wanaonekana ni hatari kwa mashuti makali.

Akizungumza na Mwanaspoti, Shime alisema kikosi chake kiko tayari kwa asilimia kubwa kukabiliana na wapinzani wake.

“Tulikuwa na muda wa maandilizi, jana na juzi tulikuwa na mazoezi yalikwenda vizuri nafikiri tuko tayari kwa mchezo mgumu na tunajua wapinzani wetu wamejipanga na wao wakitafuta nafasi ya kufuzu.”

Related Posts