Sababu ya kupata hasira kipindi cha hedhi

Dar es Salaam. Tatizo la mabadiliko ya kihisia kipindi cha hedhi, ni changamoto inayowakumba baadhi ya wanawake.

Utafiti wa jarida la The Lancet Psychiatry mwaka 2020 ulionyesha mabadiliko kama wasiwasi, huzuni, na hasira, ni matokeo ya usawa wa homoni katika mwili wa mwanamke.

 Hali hii inayojulikana kwa jina la ‘Pre-menstrual Syndrome (PMS), inatokana na mabadiliko ya homoni za estrojeni na prostrojeni, ambazo huathiri ubongo na kuleta mihemko.

Ingawa PMS ni jambo la kawaida, baadhi ya wanawake hupata dalili kali ambazo huathiri maisha yao ya kila siku, uhusiano na utendaji wao kazini au shuleni.

Kwa mujibu wa utafiti wa Psychoneuroendocrinology kwa mwaka 2022, wanawake wenye historia ya matatizo ya kihisia, huwa na PMS ambazo husababishwa na maandalizi ya kupata mtoto au kuingia hedhi.

Mchakato huo, huanzia kwenye ovari ambazo huwa na mayai ambayo kila mwezi hutolewa na kuchukua siku tatu kufika kwenye kizazi.

Wakati yai likisafiri, kuelekea kwenye kizazi, kizazi nacho kinaanza kujiandaa kwa kujaza virutubisho vyote vinavyohitajika kuanzisha maisha mapya.

 Homoni za estrojeni na prostrojeni, huwa na kazi ya kuandaa virutubisho muhimu vinavyohitajika kwa ajili ya maisha ya mtoto, huku chache zikiingia kwenye mtiririko wa damu na kusambaa mwilini na kuanza kusababisha mabadiliko ya kihisia.

Mabadiliko haya, huanzia siku ya saba mpaka ya 14 kabla ya kuingia hedhi wakati huo kiwango cha homoni za estrojeni na prostrojeni kikiwa juu.

Wakati huu, baadhi ya tafiti zinaonyesha kuwa wanawake huwa na dalili za kimwili au kisaikolojia ambazo zinaweza kudumu mpaka atakapomaliza kipindi cha hedhi.

Dalili za kimwili zinaweza kujumuisha maumivu ya kichwa, shida za kulala, maumivu ya tumbo au kutapika.

 Lakini wakati hedhi inaanza, kiwango cha homoni hizi hupungua kwa haraka,wakati mwili unapojua kwamba hakukuwa na mbolea, virutubisho vyote vilivyotengenezwa na kizazi hutolewa kama damu na mzunguko huu huendelea tena na tena.

Aidha, mtaalamu wa magonjwa ya wanawake na uzazi Dk Isaya Mhando anasema licha ya hali hiyo kuwepo ila haimtokei kila mwanamke.

“Hali hii ni kwa kuwa mfumo wa uzazi wa mwanamke umeunganishwa na sehemu ya ubongo ambayo huitwa ‘haipothalamasi’,”anaeleza.

 Anasema sehemu hiyo huamrisha homoni zote zinazohusika na mfumo wa hedhi kwa mwananmke kufanya kazi zake.

“Kwenye ubongo kuna sehemu mbili ambayo ni haipothalamasi ambayo inahusika na hisia na nyingine huachia homoni inayoenda kuhakikisha ukuaji wa mayai,”anaeleza.

Muhando anasema mayai yanapokua, na yenyewe hutoa homoni za kwenda kuandaa mji wa mimba na utengenezaji wa maziwa.

“Hali hiyo, husababisha mabadiliko ya kihisia na pengine msongo wa mawazo,”anaeleza.

Mtaalamu wa afya, Dk Paul Masua anasema mwanamke huwa na Premenstrual Syndrome (PMS) ambayo huambatana na homoni wakati wa hedhi.

“Hayo mabadiliko ndiyo chanzo hasa cha hisia za mwanamke kubadilika badilika wakati wa mzunguko wa hedhi,”anaeleza.

Anasema, mwanamke kuwa na hali hiyo ni suala la kimaumbile na kuwa wapo wanaopata maumivu, ambayo wakati mwingine huwa ni ugonjwa.

Related Posts