Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, imeelezwa kuwa Mkurugenzi wa kampuni ya mikopo ya Atlantic Micro Credit Limited, Wendy Ishengoma (38) anayekabiliwa na mashitaka ya kuendesha biashara ya upatu, ameshindwa kufika mahakamani hapo kutokana na kujifungua.
Mshtakiwa huyo ambaye alifutiwa shitaka moja la kutakatisha fedha, amejifungua mtoto wa kiume, Ijumaa Februari 21, 2025 akiwa gerezani.
Ishengoma na wenzake watatu wanakabiliwa na mashitaka ya kuongoza genge la uhalifu, kuendesha biashara ya upatu na kutakatisha Sh3.6 bilioni.
Wakili wa Serikali, Frank Rimoy ametoa taarifa hiyo leo Jumanne Februari 25, 2025 wakati kesi hiyo ya uhujumu uchumi 30853/2024 ilipoitwa kwa ajili ya kutajwa.
Wakili Rimoy ametoa taarifa hiyo mbele ya hakimu Mkazi Mkuu, Aaron Lyamuya, ambapo amedai ndugu wa mshtakiwa pamoja na taarifa aliyopewa kutoka magereza, inaeleza Wendy amejifungua mtoto wa kiume wiki iliyopita, hivyo ameshindwa kufika mahakamani hapo.
“Kutokana na hali hii, tunaomba Mahakama ipange tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa” amedai Wakili Rimoy.
Baada ya kueleza hayo, hakimu Lyamuya ameahirisha kesi hiyo hadi Machi 5, 2025 kwa kutajwa na washtakiwa wamerudishwa rumande.
Mbali na Wendy, washtakiwa wengine ni Sultan Mdee(29) Mhasibu na mkazi wa Goba, Frank Tengia(34) Meneja tawi na mkazi wa Mbezi Juu, pamoja na Mwiga Mwiga(31) ambaye ni Ofisa Masoko wa kampuni hiyo.

Mshtakiwa Wendy Ishengoma, anakabiliwa na mashtaka ya kuendesha biashara ya upatu, akiwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, hata hivyo mshtakiwa huyo amejifungua mtoto wa kiume wiki iliyopita akiwa gerezani. Picha na Hadija Jumanne
Itakumbukwa Januari 17, 2025 Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP), alimfutia Ishangoma shitaka la kutakatisha fedha.
Kutokana na kufutiwa shitaka hilo Ishengoma sasa atakuwa na mashitaka mawili huku wenzake watatu wakikabiliwa na mashitaka matatu.
Licha ya kufutiwa shitaka la kutakatisha ambalo linampa nafasi Wendy kwenda kuomba dhamana Mahakama Kuu, mshtakiwa huyo ameshindwa kwenda kuomba dhamana na hivyo anaungana na washtakiwa wenzake kuendelea kusota rumande.
Alidai katika shitaka la kwanza ni kuongoza genge la uhalifu, linalowakabili washtakiwa wote wanne, ambapo wanadaiwa kati ya Januari 18, 2024 na Oktoba 11, 2024 ndani ya Jiji la Dar es Salaam, kwa makusudi waliongoza na kusimamia genge la uhalifu kwa kufanya biashara ya upatu.
Shitaka la pili ni kuendesha biashara ya upatu, linalowakabili washtakiwa wote, tukio wanalodaiwa kulitenda kati ya Januari 18, 2024 na Oktoba 11, 2024 ndani ya Jiji la Dar es Salaam.
Inadaiwa washtakiwa katika kipindi hicho, walifanikisha mpango wa kuendesha biashara ya upatu kwa kutoa ahadi kwa wanachama na kuingia mikataba ya ubia yenye thamani ya Sh3.63 bilioni kitendo ambacho ni kinyume cha sheria.
Shitaka la tatu ni kutakatisha fedha, linalowakabili washtakiwa watatu ambao ni Mdee, Tengia na Mwiga.
Washtakiwa wanadaiwa katika kipindi hicho ndani ya Jiji la Dar es Salaam, wanadaiwa kujipatia Sh3.63 bilioni wakati wakijua kuwa wanapokea fedha hizo ni mazalia ya kosa tangulizi la jinai ambalo ni kuendesha biashara ya upatu.
Kwa mara ya kwanza, washtakiwa hao walifikishwa mahakamani hapo Oktoba 29, 2024 na kusomewa mashitaka hayo.