Dar es Salaam. Mahakama Kuu, Divisheni ya Ardhi, imepanga Machi 28, 2025 kuendelea na usikilizwaji wa kesi ya ardhi iliyofunguliwa na mtoto wa Sepeku, Bernardo Sepeku dhidi ya Bodi ya Wadhamini wa Kanisa la Anglikana Tanzania, Askofu Jackson Sostenes wa kanisa hilo pamoja na Kampuni ya Xinrong Plastic Waste Industry Co Ltd.
Bernado, ambaye ni mtoto wa marehemu John Sepeku, alifungua kesi hiyo ya ardhi namba 378/2023, akipinga kunyang’anywa zawadi ya kiwanja alichopewa baba yake mwaka 1978 na kanisa hilo.
Sepeku alipewa zawadi na kanisa hilo ambayo ni nyumba iliyopo Buguruni na kiwanja chenye ukubwa wa ekari 20 kilichopo Buza, wilayani Temeke na kama zawadi kwa kutambua mchango wake katika kanisa hilo, kama Askofu wa Mkuu wa kwanza kanisa hilo.
Kesi hiyo ilipangwa leo Jumanne, Februari 25, 2025 kuendelea na ushahidi wa upande wa mdai, lakini imeshindika kutokana na Jaji Arafa Msafiri anayesikiliza kesi hiyo kuwa na majukumu mengine ya kikazi.
Naibu Msajili wa Mahakama hiyo, Sara Buya ametoa taarifa hiyo wakati kesi hiyo ilipoitwa kwa ajili ya kuendelea.
Awali, mawakili wa Bernardo kutoka kampuni ya uwakili ya Diakonus Attorneys, Deogratias Butawantemi na Gwamaka Sekela wamedai kuwa shauri limeitwa kwa ajili usikilizwaji na tayari wanao mashahidi watatu.
Kwa upande wake wakili Dennis Malamba, amepata msiba na aliomba kuahirishwa kwa kesi hiyo.
“Jaji anayesikiza kesi hii ana majukumu mengine ya kikazi, hivyo naiahirisha hadi Machi 28, 2025 kwa ajili ya kuendelea,” amesema Naibu Msajili.
Tayari mashahidi saba wa upande wa madai wameshatoa ushahidi wao dhidi ya wadhamini wa Kanisa hilo.
Bernardo katika kesi hiyo, anadai alipwe Sh3.72 bilioni ambayo ni fidia ya hasara ya kifedha iliyopatikana kutokana na uvamizi wa mali ya ardhi katika kiwanja hicho.
Pia anaiomba alipwe fidia ya Sh493.65 milioni ambayo ingepatikana baada ya kukomaa na mavuno ya mazao yaliyokuwepo kwenye shamba hilo.
Haya hivyo, mdaiwa wa tatu katika shauri hilo, kampuni ya Xinrong Plastic Waste Industry Co Ltd, hajawahi kufika mahakamani hapo tangu kesi hiyo ilipofunguliwa licha ya kupokea wito wa kuitwa mahakamani.
Madai yake ya msingi katika shauri hilo
Katika kesi hiyo, Bernardo ambaye ni msimamizi wa mirathi ya baba yake, aliwasilisha maombi saba mahakamani hapo, kwanza anapinga kunyang’anywa zawadi ya kiwanja namba 2689 chenye ukubwa wa ekari 20 kilichopo Buza mtoni, wilayani Temeke ambacho anadai mwaka 1978, waumini na Wakristo wa dayosisi hiyo, walimpa askofu Sepeku kama zawadi.
Pili, anaomba Mahakama hiyo iamuru Bodi ya Wadhamini ya kanisa hilo, Askofu Sosthenes na kampuni ya Xinrong Plastic Waste Industry Co Ltd kwa pamoja kulipa Sh33 milioni ikiwa ni hasara aliyoipata mlalamikaji kutokanana na uharibifu wa mazao yaliyowekezwa katika shamba lililo ndani ya kiwanja hicho.
Mlalamikaji huo alidai mazao yaliyoharibiwa shambani ni pamoja na miti 200 ya malimao, miti 55 ya mikorosho, ekari mbili za mbaazi, ekari mbili za mihogo na ekari mbili za viazi vitamu.
Mazao mengine yaliyoharibiwa shambani hapo ni miti 30 ya mapapai, minazi, miti 60 ya miembe, miti 25 ya michikichi pamoja na miti 45 ya minazi.
Tatu, Bernardo anadai alipwe Sh3.72 bilioni ambayo ni fidia ya hasara ya kifedha iliyopatikana kutokana na uvamizi wa mali ya ardhi iliyopo katika kiwanja hicho.
Nne, ameiomba Mahakama alipwe fidia ya Sh493.65 milioni ambayo ingepatikana baada ya kukomaa na mavuno ya mazao yaliyokuwepo kwenye shamba hilo.
Tano, anaomba Mahakama iamuru wadaiwa wote katika shauri hilo wamlipe mlalamikaji hasara ya jumla iliyopatikana.
Vilevile, Mahakama hiyo iangalie unafuu mwingine wowote ambao itaona inafaa kutoa.
Pia, Bernado anaomba mahakama iamuru wadai hao walipe gharama za kuendesha kesi hiyo ya madai.