Benki ya Exim
imedhihirisha dhamira yake ya kujenga ujumuishi wa kifedha na kupanua huduma
zake kwa kuzindua rasmi tawi jipya katika Wilaya ya Kahama, Mkoani Shinyanga.
Tawi hili jipya linalenga kuboresha upatikanaji wa huduma za kifedha kwa
wafanyabiashara, watu binafsi, na taasisi katika wilaya hiyo. Mgeni rasmi
katika hafla hii alikuwa Mheshimiwa Doto Biteko, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa
Nishati.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya Exim,
Bw. Jaffari Matundu, alieleza umuhimu wa upanuzi huu kwa ukuaji wa sekta ya
kifedha: “Kahama ni moja ya vituo
muhimu vya uchumi nchini, ikiwa na sekta zinazochangia kwa kiasi kikubwa kwenye
maendeleo ya taifa. Mji huu unajulikana sana kwa mchango wake katika sekta ya
madini, hususan uzalishaji wa dhahabu, ambao umeifanya Kahama kuwa muhimu
katika uchumi wa taifa.”
Jaffari aliongeza kuwa, “Kwa kuanzisha tawi hili, tunalenga kuhudumia
mahitaji mbalimbali ya kifedha ya sekta hizi—iwe ni kwa ufadhili wa biashara,
huduma za kibenki za kidijitali, au bidhaa za kifedha zinazolenga kukuza
maendeleo ya kiuchumi.”
Tawi la Kahama litatoa huduma kamili za kibenki, ikiwemo akaunti za
biashara na binafsi, huduma za hazina (treasury services), na mifumo ya
kidijitali ya kibenki. Wateja watanufaika na huduma za Exim Bank zinazolenga
kutoa suluhisho bora, la kisasa, na lenye ushindani kwa kuzingatia mahitaji ya
soko yanayobadilika kila wakati.
Mheshimiwa Doto Biteko, alisifu juhudi za benki ya Exim za kupanua huduma
zake, akisisitiza mchango wa taasisi za kifedha katika maendeleo ya Uchumi wa
watu na taifa kiujumla: “Serikali imekuwa ikihimiza taasisi zetu kuipeperusha
bendera ya Tanzania nje ya nchi kwa kufanya uwekezaji wa kimkakati. Kwa kipekee
kabisa niwapongeze sana Exim bank kwa kutuwakilisha vyema katika nchi za
Comoros, Uganda, Djibouti, pamoja na Ethiopia.”
“Serikali imeweka mkazo mkubwa katika kuhakikisha huduma za kifedha
zinawafikia Watanzania wengi zaidi, hasa wale walioko nje ya mifumo rasmi ya
kifedha. Kwa niaba ya Serikali, naomba nitumie fursa hii kuipongeza Exim Bank
kwa hatua hii kubwa na kwa jitihada zenu za kuleta huduma za kifedha karibu
zaidi na wananchi,” alisema Mhe. Biteko.
Tawi hili jipya linaonesha azma ya benki ya Exim ya kutoa suluhisho
rahisi na jumuishi za kifedha huku ikiongeza uwepo wake katika maeneo muhimu
kote Tanzania. Kwa kujikita katika ubunifu na utoaji wa huduma bora kwa wateja,
benki ya Exim inaendelea kuwa mshirika muhimu wa maendeleo ya kifedha nchini.
Kadri benki ya Exim inavyoendelea kupanua huduma zake Kahama, benki hii
inaendelea kushikilia dhamira yake ya kuwawezesha watu binafsi na
wafanyabiashara kwa huduma za kifedha zinazopatikana kwa urahisi, za kuaminika,
na za kisasa.
Upanuzi huu ni sehemu ya mkakati mpana wa benki wa kuchochea maendeleo ya
uchumi, kuimarisha biashara za ndani, na kuongeza uelewa wa masuala ya kifedha
katika jamii. Kwa mtazamo unaoweka mteja mbele na dira ya mafanikio ya muda
mrefu, benki ya Exim iko tayari kubadilisha huduma za kifedha na kuleta
maendeleo endelevu nchini Tanzania.
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Mhe. Dkt. Dotto Biteko (wa tatu kutoka kulia), akiwa katika uzinduzi Rasmi wa tawi la benki ya Exim Tanzania wilayani Kahama mkoani Shinyanga. Kulia kwake ni Afisa Mtendaji Mkuu wa Exim Bank, Bw. Jaffari Matundu wakiwa katika picha ya pamoja na viongozi wengine wa Serikali na benki ya Exim katika tukio lililofanyika mnamo tarehe 25 Februari 2025 mjini Kahama.
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Mhe. Dkt. Doto Biteko (wa tatu kutoka kushoto), ambaye alikuwa Mgeni Rasmi akikata utepe wakati hafla ya uzinduzi Rasmi wa tawi la benki ya Exim wilayani Kahama mkoani Shinyanga Wa pili kutoka kushoto ni Afisa Mtendaji Mkuu wa Exim Bank, Bw. Jaffari Matundu na Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Anamringi Macha (wa nne kutoka kushoto) wakiwa katika picha ya pamoja na viongozi wengine wa Serikali na benki ya Exim katika tukio hilolilofanyika mnamo tarehe 25 Februari 2025 mjini Kahama.