VIDEO: Mtifuano wa ‘Kenya Power’, Jiji la Nairobi zaidi ya filamu

Nairobi. Hali ya taharuki imeibuka jijini Nairobi baada ya Halmashauri ya Jiji la Nairobi kukatiwa umeme na Shirika la Umeme la Kenya Power (KPLC), kutokana na deni kubwa la Sh3 bilioni (zaidi ya Sh60 bilioni za Tanzania) linalodaiwa na halmashauri hiyo.

Katika kujibu hatua hiyo, Halmashauri ya Jiji la Nairobi nayo iliamua kutekeleza hatua kali kwa kupeleka magari ya kubeba taka na kuzimwaga taka hizo mbele ya ofisi za Kenya Power.

Halmashauri hiyo pia ilikata maji safi na ya mifumo ya maji taka katika jengo la Stima Plaza, kituo cha biashara cha Kenya Power.

Meneja Mkuu wa Huduma za Kibiashara wa Kenya Power, Rosemary Oduor, jana Jumatatu Februari 24,2025 alilalamikia hatua hiyo akisema kuwa si sahihi na akashutumu Halmashauri ya Jiji kwa kushindwa kutimiza makubaliano ya kulipa bili za umeme kila mwezi.


Filamu ya manispaa na KPLC ngumu kumeza

Oduor alisisitiza kuwa bila malipo hayo, sekta ya umeme inakosa mapato muhimu ya kuendelea kutoa huduma muhimu kwa wananchi.

Hata hivyo, Serikali ya Jiji la Nairobi ilijibu kwa kusema kwamba Kenya Power pia ina madeni kwao, yakiwemo ada za huduma za miundombinu (wayleave fees) ambazo hadi sasa zimefikia Sh4.8 bilioni (Sh97 bilioni za Tanzania).

Kaimu Katibu wa Jiji la Nairobi, Godfrey Akumali, alisema kwamba Kenya Power haijatekeleza majukumu yake ya kisheria, kama vile kulipa ada za njia za miundombinu na kodi ya ardhi, na hivyo kuikosea Halmashauri ya Nairobi.

Akumali aliongeza kuwa hatua ya kuingilia huduma za Kenya Power ilikuwa ni ya mwisho katika kulazimisha kampuni hiyo kulipa madeni yake, akisema kuwa kama kuna mtu mwingine yeyote anadaiwa, hatua kama hiyo itachukuliwa dhidi yao pia.

Kwa upande mwingine, Ofisa wa Kamati ya Fedha na Mipango ya Kaunti, Charles Kerich, aliishutumu Kenya Power kwa kutumia mkakati wa kujifanya kama mwathirika ili kupotosha mjadala, kuhusu madeni yao ya ada za miundombinu.

Kerich alisisitiza kuwa Kenya Power imekuwa ikikwepa kulipa ada hizo licha ya mawasiliano mengi yaliyofanywa na halmashauri.

Wakati huohuo Kerich, aliilaumu Kenya Power kwa kuleta mtafaruku ili kupotosha mjadala kuhusu madeni yao.

Alidai kuwa kampuni za mawasiliano ambazo hapo awali zilikuwa zikilipa ada hizo kwenye ofisi za jimbo ili kupitisha nyaya chini ya ardhi, sasa hazilipi tena kwa kuwa zimeanza kutumia nguzo za Kenya Power kusambaza huduma zao.

Imeandikwa na Mgongo Kaitira kwa msaada wa mashirika ya habari.

Related Posts