Siri nyuma ya misamaha ya Rais kwa January, Nape

Dar es Salaam. Siku moja baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kuamua ‘kumrudisha kwake’ Mbunge wa Bumbuli, January Makamba, baada ya kumwengua kwenye baraza lake la mawaziri, baadhi ya wachambuzi wameielezea hatua hiyo kama njia ya kuleta maridhiano ndani ya chama kuelekea uchaguzi mkuu.

Mbali na maoni hayo, ingia toka ya mwanasiasa huyo ndani ya Baraza la Mawaziri, inaelezwa mwanasiasa huyo ana kitu, ambacho wakubwa hawawezi kukiacha kipotee nje ya Serikali kutokana na uzoefu na nafasi alizowahi kushika na matokeo chanya kwenye utendaji wake.

Mbali na kuongoza wizara mbalimbali kama Nishati, Mazingira na Muungano na Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Makamba amewahi kuwa kwenye timu ya kampeni ya mgombea urais wa CCM (John Magufuli) iliyoteuliwa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) Agosti 17, 2015.

Katika uchaguzi huo na hata ule wa mwaka 2020, Makamba alihusika zaidi kampeni kwa vyombo vya habari na takwimu.

Makamba pia alikuwa miongoni mwa wagombea urais watano waliteuliwa Kamati Kuu ya CCM kwenda hatua ya mchujo wa NEC, ulioibuka na majina matatu, akiwemo Rais Magufuli mwaka 2015 na amekuwa akitazamwa kama wanasiasa wenye nia ya kuwania tena nafasi hiyo katika siku za usoni.

Rais Samia alitangaza ‘kumrudisha kwake Makamba juzi akiwa ziarani Lushoto Mkoa wa Tanga. Makamba ni mbunge wa Bumbuli wilayani humo.

“Mwisho kabisa nataka nimwite mwanangu January (Makamba) hapa, aje huku arudi kwa mama. Sisi wamama mnatujua, ukimkera mama anakupiga kikofi anakufichia chakula, si ndio? Sasa mwanangu nilimpiga kofi, nikamfichia chakula, lakini leo namrudisha kwa mama. Haya mwanangu njoo,” ilikuwa ni kauli ya Rais Samia alipomuita Makamba jukwaani na kumkumbatia.

Hata hivyo, Rais Samia hakueleza Makamba alimkera katika jambo gani, lakini alitengua uteuzi wake kwenye nafasi ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Julai 22, 2024, sambamba na naibu wake, Stephen Byabato. Katika mkumbo huo alikuwemo pia Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye.

Ilikuwa baada ya Nape kunukuliwa akisema angemsaidia Byabato ambaye ni mbunge wa Bukoba Mjini, kushinda ubunge katika uchaguzi wa 2025 kwa sababu anafahamu mbinu za uchaguzi na kwamba matokeo ya uchaguzi hayategemei sanduku la kura, bali yanategemea nani anasimamamia uchaguzi na kuhesabu kura.

Hii haikuwa mara ya kwanza kwa Makamba kuenguliwa kwenye Serikali na baadaye kurejeshwa kwa msamaha wa Rais Samia, baada ya mara ya kwanza kukutwa na hali hiyo wakati wa uongozi wa Rais John Magufuli.

Rais Magufuli kwa nyakati tofauti alitengua uteuzi wa Makamba, Nape na William Ngeleja (aliyekuwa mbunge wa Sengerema) baada ya sauti zinazodaiwa zao kusambaa mitandani kwa kile kilichodaiwa kumzungumzia vibaya Rais.

Kama ilivyokuwa kwa Rais Samia, ambaye alitangaza msamaha kwa Makamba kwenye hotuba yake kwa wananchi wa Lushoto akiwa ziarani mkoani Tanga, ndivyo ilivyokuwa kwa Magufuli ambaye Septemba 4, 2019 alitangaza msamaha kwake kwenye mkutano wa wataalamu wa ujenzi.

Kwenye mkutano huo, Magufuli alisema ana uhakika kuwa sauti zile zilikuwa zao (Makamba, Nape na Ngeleja), lakini amefikiria na kuwasamehe.

“Siku za hivi karibuni kuna watu walinitukana na kuthibitisha kuwa sauti zile ni zao, nikawa nakaa nafikiria, nikasema hawa wakipelekwa katika kamati ya siasa, adhabu itakuwa kubwa. Nikasema ngoja ninyamaze, lakini wakajitokeza wawili wakaniomba msamaha.

“Nilijiuliza kila siku, mimi huwa naomba msamaha kwa Mungu, kwa ile sala ya ‘tusamehe makosa yetu kama tunavyowasamehe wengine’, nikaona hawa waliokuja kuniomba msamaha nisipowasamehe nitabaki na maumivu makubwa, hivyo nikaamua kuwasamehe.

“Hawa waliokuja kuniomba msamaha na kutoa kweli katika dhamira yao ni January Makamba na William Ngeleja. Niliwasamehe na kusahau,” Magufuli aeleza.

Licha ya msamaha huo, kwenye baraza la mawaziri wawili hao – Makamba na Nape walirejeshwa baada ya Rais Samia kuchukua usukani Machi, 2021.

Hata hivyo, tofauti na Rais Magufuli aliyeeleza makosa yao na sababu za msamaha, Rais Samia hakuweka bayana ni kosa lipi lililofanywa na Makamba hadi akatengua uteuzi wake.

Licha ya kutokutajwa sababu hizo, bado kulikuwa na taarifa zisizo rasmi kwenye masuala ya kisiasa na kimataifa.

Baadhi ya wachambuzi wa masuala ya kisiasa nchini wameuchambua msamaha huo wa Makamba, wakisema una kitu ndani yake na pia huenda ni utekelezaji kwa vitendo wa falasafa ya maridhiano hasa wakati huu wa kuelekea uchaguzi mkuu.

Ramadhan Manyeko, mchambuzi wa masuala ya kisiasa alisema ingia toka ya Makamba na kauli za msamaha za wakuu wa nchini, kuanzia kwa Magufuli na sasa Rais Samia zinaashiria mwanasiasa huyo ana kitu ndani yake.

“Ukimuona mtu anaingia na kutoka ana kitu, inawezekana uwezo wake, hivyo yanayotokea hadi kuwekwa kando ni kwa kutokuelewana na kutokubaliana,” alisema.

Akimtolea mfano pia Nape na Mwigulu Nchemba, mchambuzi huyo alisema pia ni watu ambao wanapitia hekaheka za kutenguliwa na kurejeshwa.

“Mtakumbuka kuna wakati Mwigulu alitenguliwa, baadaye akarudishwa kuwa Waziri wa Katiba na Sheria (ilikuwa Mei 2, 2020 akichukua nafasi ya Dk Augustine Mahiga aliyefariki dunia).

“Makamba na Nape pia, inaonyesha hawa watu watatu (Nape, Mwigulu na Makamba) wana ushawishi na nyuma yao kuna watu wengi, hivyo kuwapoteza kwenye mfumo kuna athari,” aliongeza Manyeko.

Mchambuzi mwingine, Profesa Mohammed Makame alisema nyuma ya msamaha huo kuna vitu vingi.

“Vijana hawa (Makamba na Nape) historia inaonyesha wameanza siasa mapema, kwa maana kwamba hivi sasa wamekomaa kisiasa na kiutendaji pia.

“Tukiiangalia siasa yetu bila shaka inakwenda vipindi vya mabadiliko katika hatua mbalimbali, siasa tunayoizungumzia hivi sasa si ya miaka ya ujamaa na kujitegemea, inabadilika, vitu vingi vikitokea kuna utashi na maono,” alisema.

Alisema ingia toka ya Nape na Makamba na vipindi vya msahama kunaashiria uimara wa chama na wanasiasa wenyewe.

“Yawezekana kuna kasoro za mitazamo na kufanya vitu muda ukiwa bado haujafikia, vitu vipo vingi. Kuingia kwao na kutoka hakumaanishi kasoro, ni uimara wa chama kuweza kusimamia misingi na si ajabu kuchukuliwa hatua na si kwamba watu hao hawafai kabisa, wana nguvu na uwezo, ndiyo sababu ya yote. Mtu anayesamehewa akikubali kosa ni hatua ya kujifunza na kurudi kwenye mstari,” alisema.

Katika hatua nyingine, uamuzi huo wa Rais Samia unaangaliwa kama mkakati wa chama chake kukusanya upya kura zilizotawanyika, ikiwa ni njia ya kujiimarisha kuelekea uchaguzi mkuu wa Oktoba.

Kupitia mijadala mbalimbali iliyotokana na hatua hiyo, ilielezwa hiyo ni nguvu ya CCM ya kutokubali kuacha kura zimesambaratika, badala yake huzikusanya kwa njia hiyo, ili waingine katika uchaguzi wakiwa kitu kimoja.

CCM kinatajwa kuwa chama chenye makada walio tayari kumaliza tofauti miongoni mwao ili kuingia kwenye uchaguzi wakiwa wamoja.

Kutokana na hilo, kila unapokaribia uchaguzi, CCM husambaza viongozi wake ambao ni walezi kwenye mikoa mbalimbali kukutana na makundi yote yenye misuguano kwenye vikao vya ndani kujadili na kutatua matatizo yao.

Related Posts