Dar es Salaam. Wakati wananchi, wadau na viongozi wa mitaa wakionesha changamoto iliyopo kwenye udhibiti wa taka za kielektroniki, viongozi wa halmashauri na Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) wametaja njia ya kuzishughulikia.
Mkuu wa Kitengo cha Udhibiti wa Taka Ngumu na Usafirishaji wa Manispaa ya Ubungo, Lawi Bernard anasema wananchi wapo tayari kutenganisha taka, lakini changamoto kubwa, huishia sehemu moja kwenye dampo.
“Tunaanza kwa baadhi ya taka, kama zile zinazooza. Kadri teknolojia inavyobadilika, tunajitahidi kutoa elimu ili watu watenganishe angalau kwa makundi makubwa, kama zinazooza na zile za plastiki. Hata hivyo, changamoto ni kwamba taka hizo zinapofika dampo huishia kuchanganywa tena,” anasema Bernard.
Anasema Manispaa ya Ubungo ina magari manne ya kubebea taka ambayo huzisafirisha zote hadi dampo kuu.

Kwa upande wa Manispaa ya Temeke, Mkuu wa Kitengo cha Usimamizi wa Taka na Usafi wa Mazingira, Mkana Mkana anasema wameweka taratibu za kutenganisha taka hasa kwenye maeneo ya masoko.
Hata hivyo, changamoto ipo kwa wananchi wanaokusanya taka hizo pamoja, kabla ya kufikishwa dampo.
“Kuna vizimba vya kutenganisha taka, lakini wananchi wanazikusanya pamoja. Hali hii inawafanya wahudumu wa magari ya taka wasiweze kuzitenganisha wanapozikusanya na kuzipeleka dampo,” anasema.
Hata hivyo, Mkana anasema manispaa hiyo inatoa semina za kila mwezi kwa wananchi kwenye maeneo ya mikusanyiko kama masoko, kwa kushirikiana na viongozi wa mitaa.
Pia, anasema elimu inatolewa shuleni, akiitaja Shule ya Kibasila kuwa ya kupigiwa mfano Mkana.
“Tunapowafundisha watoto tunaamini nao watafundisha wazazi, walezi na jamii kwa jumla,” anasema.
Akizungumza na Mwananchi, Meneja wa Dampo la Pugu Kinyamwezi, lililopo Manispaa ya Ilala, Richard Kishere anasema aina ya taka wanazopokea hupata changamoto kuzitenganisha.

“Sheria inasema taka zitenganishwe kwenye chanzo. Sasa zikifika pale dampo, utatenganishaje? Umejionea mwenyewe foleni ya magari yanayosubiri kumwaga taka na kuondoka,” anasema Kishere.
Kishere anasema dampo hilo limeweka utaratibu maalumu wa kusajili waookota taka ambao wanaruhusiwa kuchukua zinazoweza kurejelewa.
“Vifaa au taka zinazochukuliwa ni plastiki, taka za kielektroniki na nyingine kulingana na mahitaji ya watu,” anasema Kishere.
NEMC, wizara zaonyesha njia
Meneja wa Utekelezaji wa Sheria wa NEMC, Taimuru Kissiwa anasema taka za kielektroniki na zile hatarishi zinapaswa kukusanywa na kupelekwa maeneo maalumu ya urejelezaji au kuuzwa nje ya nchi kwa mujibu wa kanuni.

“Utaratibu ni kwamba, unapomaliza matumizi ya vifaa kama kompyuta au kiyoyozi, mwananchi haruhusiwi kuvitupa ovyo. Vifaa hivyo vina thamani na vinaweza kununuliwa. Kuna wakusanyaji waliosajiliwa rasmi ambao wana vibali kutoka ofisi ya Makamu wa Rais, na mchakato wao unasimamiwa na NEMC,” anasema Kissiwa.
Anasema taka hizo sasa zimekuwa mali: “Taka zote, hususan za kielektroniki ni mali. Zinakusanywa, zinarejelezwa na baadhi huuzwa nje ya nchi.”
Ofisa Mazingira Mwandamizi wa NEMC, Kuluthumu Shuhu anasisitiza umuhimu wa jamii kutunza mazingira kwa kuhakikisha taka zinatupwa katika maeneo maalumu yaliyotengwa.
“Tunaendelea kuhimiza jamii kuhakikisha zinahifadhi vizuri taka hizi. Tunafahamu kwamba ni changamoto kubwa, lakini tunaendelea kuchukua hatua, ikiwamo kuboresha maeneo ya kuhifadhi na kukusanyia taka hizi,” anasema.
Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Khamis Hamza Khamis anasema Serikali ipo kwenye mikakati ya kuangalia namna bora ya kupunguza taka za kielektroniki, huku ikiwahamasisha wananchi kushiriki katika juhudi hizo.
“Vifaa hivi, iwe ni vipya, vibovu au vilivyoharibika ni tatizo ambalo linaathiri mazingira. Kwa kupitia ushirikiano wa pamoja, tumeona umuhimu wa kutoa elimu kwa wananchi na nchi wanachama juu ya njia bora za kukusanya, kusafirisha na kupunguza taka hizi,” anasema.
Khamis anasema juhudi za pamoja kati ya Serikali, wananchi na wadau zitaleta suluhisho endelevu kwa changamoto ya taka za kielektroniki nchini.
Kanuni za Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta za mwaka 2020, zinasisitiza usimamizi bora wa taka za kielektroniki ili kulinda mazingira na afya ya umma.

Kifungu cha 3 kinafafanua taka za kielektroniki kama vifaa vilivyotupwa, huku kifungu cha 12 kikihimiza wazalishaji na waagizaji kubuni bidhaa zinazoweza kurejelezwa na kuanzisha vituo vya kukusanya taka.
Kifungu cha 13 kinakataza utupaji usio sahihi kama kuchoma au kutupa kiholela na kifungu cha 14 kinataka kampeni za uhamasishaji. Wahusika wenye leseni wanapaswa kutoa ripoti kwa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (kifungu cha 16). Kanuni hizi zinalenga usimamizi endelevu wa taka za kielektroniki.
Akizungumzia hilo, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Dk Jabiri Bakari anasema mamlaka hiyo inahusika na udhibiti wa taka za vifaa vya kielektroniki vya mawasiliano pekee.
Hatua ya kifaa cha mawasiliano cha kielektroniki kufikia kuitwa taka, Dk Bakari anasema inatokana na kuisha kwa muda wa matumizi yake.
“Simu na vifaa vingine vya mawasiliano vina ukomo wa muda wa matumizi, ukifika huo ndiyo vinaitwa taka inayopaswa kuteketezwa,” anasema Dk Bakari.
Anasema kwa sababu vifaa hivyo hutengenezwa na malighafi mbalimbali zikiwamo hatari kwa binadamu, havipaswi kutupwa kama zinavyotupwa taka nyingine, bali huteketezwa.
Dk Bakari anasema kuna mwongozo wa kimataifa unaozipa wajibu kampuni zinazozalisha vifaa hivyo, kulipa ada itakayowezesha kugharimia uteketezaji wa vifaa hivyo vitakapoisha muda wake wa matumizi.
“Ada hiyo inalipwa na mzalishaji kwenda nchi ambayo kifaa husika kimeuzwa au kinapokwenda kutumika,” anasema.