CMSA YAJIVUNIA MAFANIKIO LUKUKI 2024, THAMANI MASOKO YA MITAJI YAFIKIA TRILIONI 46.7

 

MAMLAKA ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA) imesema katika mwaka 2024 kumekuwa na mafanikio makubwa ambayo yamewezesha pia thamani ya uwekezaji katika masoko ya mitaji kuongezeka kwa asilimia 24.7 na kufikia Sh.trilioni 46.7 katika kipindi kilichoishia Desemba 2024, ikilinganishwa na Sh.trilioni 37.4 katika kipindi kilichoishia Desemba 2023.

Pia thamani ya uwekezaji katika hisa za kampuni zilizoorodheshwa katika Soko la Hisa yaani imeongezeka kwa asilimia 22.3 na kufikia Sh.trilioni 17.87 katika kipindi kilichoishia Desemba 2024, ikilinganishwa na Sh.trilioni 14.61 katika kipindi kilichoishia Desemba 2023.

Aidha, thamani ya Mifuko ya Uwekezaji wa Pamoja imeongezeka kwa asilimia 41.6 na kufikia shilingi trilioni 2.6 katika kipindi kilichoishia Desemba 2024,ikilinganishwa na shilingi trilioni 1.8 katika kipindi kilichoishia Desemba 2023.

Mafanikio hayo yameelezwa leo Februari 26,2025 jijini Dar es Salaam na Ofisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana(CMSA), CPA. Nicodemus Mkama wakati akitoa tathimini yq utendaji wa masoko ya mitaji kwa mwaka 2024.

“CMSA ina jukumu la kuendeleza na kusimamia masoko ya mitaji hapa nchini, ikiwa ni pamoja na kuwezesha utoaji wa bidhaa mpya na bunifu zinazovutia wawekezaji wa ndani na kimataifa. Katika kutekeleza jukumu hili, katika kipindi cha mwaka 2024, masoko ya mitaji yamepata mafanikio.”

Ametaja baadhi ya mafanikio mengine ambayo yamepatikana ni uwepo wa Bidhaa Mpya na Bunifu ambapo amesema mwaka 2024 umeshuhudia utoaji wa bidhaa mpya na bunifu zinazovutia wawekezaji wa ndani na wa kimataifa.

Amefafanua mathalani, Hatifungani ya kijani ya taasisi ya umma iliyotolewa na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira ya Jiji la Tanga (Tanga-UWASA) kwa ajili ya kutekeleza miradi ya miundombinu ya maji na utunzaji wa mazingira,ambayo ilikusanya Sh.bilioni 54.72, na kuvuka lengo la kukusanya shilingi bilioni 53.2, sawa na mafanikio ya asilimia 103

Vilevile, Hati Fungani ya Miundombinu ya Samia iliyotolewa na Benki ya CRDB ilikusanya Sh.bilioni323.09, kuvuka lengo la kukusanya shilingi bilioni 150,sawa na mafanikio ya asilimia 215.4.

Amesema fedha zilizopatikana zinatarajiwa kuwezesha wakandarasi wa ndani wanaofanya kazi na Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini Tanzania (TARURA), kutekeleza miradi ya ujenzi wa miundombinu ya barabara vijijini na mijini.

Aidha, Hatifungani kwa ajili ya kuendeleza kampuni ndogo na za kati za ujasiriamali (SMEs) iliyotolewa na Benki ya Azania, ambapo kiasi cha Sh.bilioni 63.3kimepatikana, sawa na mafanikio ya asilimia 210.9.

Pia, Hatifungani aina ya Sukuk iliyotolewa na kampuni ya iTrust Finance, kwa ajili ya kuwekeza katika biashara ndogo na za kati zinazokidhi misingi ya Shariah, ambapo kiasi cha Sh.bilioni 13.27 kimepatikana, sawa na mafanikio ya asilimia 265. Vile vile, Mauzo ya Hisa Stahiki za Benki ya DCB zenye thamani ya shilingi bilioni 10.74, ambapo mauzo haya yamepata mafanikio ya asilimia 100.

CPA.Mkama pia amesema mwaka 2024, umeshuhudia mwamko mkubwa wa utoaji bidhaa mpya na bunifu katika Mifuko ya Uwekezaji wa Pamoja, hivyo kuweka wigo mpana wa fursa za uwekezaji kwa watanzania wa kada mbalimbali, ikiwa ni Pamoja na vijana, wanawake na makundi maalumu.

“CMSA iliidhinisha Mifuko ya Uwekezaji inayoendeshwa na Kampuni ya iTrust Finance Limited, ambapo mifuko mipya mitano ilizinduliwa—iSave, iCash, Imaan, iIncome, na iGrowth.

“Vilevile, Zan Securities na Orbit Securities walizindua mifuko ya Timiza na Inuka, huku Alpha Capital ikianzisha Mfuko wa Halal. Aidha, Sanlam Investments East Africa ilizindua SUTS – SANLAM Unit Trust Scheme, ikijumuisha Sanlam Pesa Money Market Fund na US Dollar Fixed Income Fund.

“Kutokana na juhudi hizi, thamani ya Mifuko ya Uwekezaji wa Pamoja (NAV) iliongezeka kwa asilimia 41.63, kutoka shilingi trilioni 1.84 mwaka 2023 hadi shilingi trilioni 2.61 mwaka 2024. Ukuaji huu umetokana na mikakati ya utoaji wa elimu kwa umma unaofanywa na wadau katika masoko ya mitaji na matumizi ya mifumo ya kidijitali, ambayo imerahisisha upatikanaji wa huduma za masoko ya mitaji mijini na vijijini.”Amesema.

Kuhusu matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano amesema imekuwa na mchango mkubwa katika kuongeza mauzo katika soko la hisa. Matumizi ya teknolojia ya Habari, ikiwa ni pamoja na matumizi ya simu za mkononi yameongeza ushiriki wa wawekezaji wa ndani, hivyo kuongeza ukwasi katika soko la hisa.

Amefafanua katika mwaka 2024, asilimia 24.33 ya mauzo ya hisa yametokana na matumizi ya teknolojia ya habari, ikilinganishwa na asilimia 4.84 mwaka 2023 huku akitoa rai kwa wadau katika masoko ya mitaji kushirikiana na CMSA katika mwaka wa Fedha 2025/2026 kutekeleza mikakati mbalimbali.

Ametaja baadhi ya mikakati hiyo kuongeza juhudi za kutekeleza Mpango Mkakati wa elimu kwa umma kuhusu fursa na faida zinazopatikana kwenye masoko ya mitaji, ikiwa ni pamoja na kutoa machapisho mbalimbali magazetini.

Pia kushiriki kwenye mahojiano ya vipindi vya Redio na Runinga, kutoa semina, warsha na makongamano kwa makundi mbalimbali, ikiwa ni pamoja na vijana, wanawake na walemavu. Hafla ya leo iliyoandaliwa na Vertex International Securities ni sehemu ya utekelezaji wa mkakati huo.

Mengine ni kuongeza idadi ya bidhaa, ambapo Mamlaka itaendelea kutoa miongozo ya utoaji na usimamizi wa bidhaa na huduma mpya, bunifu, na zenye mlengo maalum.

Pia Kuimarisha matumizi ya teknolojia katika kutoa huduma za masoko ya mitaji, ambapo CMSA itapitia na kuidhinisha mifumo ya kidigitali inayowezesha ushiriki mkubwa wa wananchi kwenye masoko ya mitaji.

“Hatua hii inatarajiwa kuongeza ushiriki wa wananchi mijini, vijijini katika masoko ya mitaji, na hivyo kuchangia utekelezaji wa Mpango Mkakati wa Tatu wa Taifa wa Huduma Jumuishi za Fedha.Kwa ujumla, katika kipindi cha mwaka 2024, masoko ya mitaji nchini Tanzania yameimarika na kuonyesha ukuaji mzuri na wa kuridhisha…

“Yakichochewa na utoaji wa bidhaa mpya na bunifu, matumizi ya teknolojia ya Habari na Mawasiliano, Utoaji elimu kwa umma ulioleta mwamko mkubwa kwa wawekezaji wa ndani na wa kimataifa. Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA) itaendelea kutekeleza mikakati yenye lengo la kuchagiza na kujenga uchumi shindani kwa maendeleo ya watu,”amesema CPA.Mkama.


Related Posts