Aliyemuua mkewe, kumchoma kwa magunia ya mkaa ahukumiwa kunyongwa

Dar es Salaam. Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, imemhukumu mfanyabiashara Hamis Luwongo, kunyongwa hadi kufa baada ya kupatikana na hatia ya kumuua mke wake wa ndoa, Naomi Marijani.

Uamuzi huo umetolewa leo Februari 26, 2025 na Jaji wa Mahakama hiyo, Hamidu Mwanga, baada ya kuridhishwa na ushahidi wa mashahidi 14 na vielelezo 10 uliotolewa mahakamani hapo.

Kabla ya kutolewa kwa adhabu hiyo, jopo la mawakili wawili  Serikali ukiongozwa na Wakili Mkuu wa Serikali Yasinta Peter akisaidiana na Wakili Wa Serikali Mwandamizi, Ashura Mnzava, uliomba Mahakama itoe adhabu kali dhidi ya mshtakiwa huyo ili iwe fundisho kwa wanaume wote wanaowafanyia ukatili wanawake wao kwa kigezo kuwa wapo kwenye ndoa.

Khamis Luwongo, akiwa ndani ya Mahakama, baada ya kuhukumiwa kifungo cha kunyongwa hadi kufa kwa kosa la kuua mke wake, Naomi Marijani. Picha na Hadija Jumanne.

“Kitendo kilichofanywa na mshtakiwa ni cha ukatili na unatupa mashaka kwa wanawake waliopo katika ndoa na wanawake wanaingia katika ndoa, hivyo tunaomba Mahakama yako itoe adhabu kali ili iwe fundisho kwa wanaume wanaotumia kigezo cha ndoa kufanya ukatili kwa wake zao” amedai wakili  Mnzava

Katika kesi hiyo ya jinai namba 44/2023, Hamis, mkazi wa Gezaulole, wilayani Kigamboni,  alikuwa anakabiliwa na shtaka la mauaji ya mkewe Naomi Orest Marijani kinyume cha kifungu cha 196 na 197 cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu, kama ilivyorejewa mwaka 2019.

Anadaiwa kutenda kosa hilo Mei 15, 2019 nyumbani kwao kisha akauchoma mwili kwa kutumia magunia mawili ya mkaa ndani ya banda la kuku. Inadaiwa masalia ya mwili na majivu alikwenda kuyazika shambani na kupanda migomba juu yake.

Upande wa mashitaka ulifunga ushahidi Novemba 18, 2024 baada ya kuwaita mashahidi 14 na kuwasilisha vielelezo tisa, huku upande wa utetezi ukiufunga Novemba 19, 2024 baada ya kumuita shahidi mmoja ambaye ni mshtakiwa mwenyewe, bila kuwasilisha kielelezo chochote.

Mshtakiwa katika utetezi alikana kumuua mkewe akidai hajafa bali alitoroka na kwamba, taarifa alizowaeleza Polisi kuwa alimuua na kuchoma moto mwili wake akazika majivu na masalia yake shambani hazikuwa za kweli.

Alidai aliwadanganya ili kujinusuru na mateso ya kipigo kutoka kwa askari polisi waliomtaka awaonyeshe iliko maiti ya mkewe.

Mshtakiwa alieleza hata masalia ya mifupa aliyowaonyesha Polisi shambani kwake si ya mkewe bali ni ya mzoga alioukuta wakati akisafisha shamba lake na mingine ilisalia kwenye kaburi lililohamishwa kwenye shamba lingine alilonunua eneo la Mwongozo, Kigamboni.

Alidai mifupa iliyofukuliwa na mafundi waliokuwa wakichimba udongo kutengeneza msingi wa nyumba aliyokuwa akiijenga, aliichukua na kwenda nayo shambani akaiweka pamoja na ya mzoga kisha akaichoma pamoja na takataka nyingine.

Alidai ndiyo maana hata uchunguzi wa kisayansi uliofanywa na Mkemia Mkuu wa Serikali matokeo yake hayakutoa uthibitisho kuwa ni ya mkewe Naomi.

Upande wa mashitaka baada ya mshtakiwa kumaliza utetezi, uliiomba Mahakama iamuru daktari bingwa wa magonjwa ya akili kutoka Hospitali ya Taifa ya Afya ya Akili Mirembe, Dk Sadiki Mandari aitwe.

Dk Mandari ambaye pia ni Mkurugenzi wa Huduma za Tiba ndiye aliyemfanyia mshtakiwa uchunguzi wa afya ya akili kwa amri ya Mahakama.

Katika ripoti ya uchunguzi wa afya ya akili ya mshtakiwa iliyowasilishwa mahakamani ilionyesha wakati wa tukio la mauaji anayodaiwa kutenda mshtakiwa alikuwa na tatizo la kiakili.

Upande wa mashitaka uliiomba Mahakama daktari huyo aitwe kizimbani kwa ajili ya kumfanyia mahojiano kuhusu ripoti hiyo. Jaji Mwanga alikubali ombi hilo na akuamuru afike mahakamani kuhojiwa Novemba 25.

Alipohojiwa na mawakili wa pande zote kuhusu ripoti hiyo, Dk Mandari aliikana akidai haitambui, akiwasilisha nyingine inayoeleza wakati mshtakiwa akitenda kosa hilo hakuwa na tatizo la kiakili bali alikuwa na akili timamu.

Jaji Mwanga alionyesha kukasirishwa na hilo akahoji kwa nini mtaalamu kama yeye awasilishe mahakamani ripoti mbili tofauti katika kesi nyeti kama hiyo inayohusu maisha ya watu. Mshtakiwa alidai daktari huyo ameiaibisha taasisi yake.

Dk Mandari alipobanwa kwa maswali alisema kuna mmoja wa ndugu wa mshtakiwa alimpigia aende aitetee ripoti iliyoko mahakamani.

Alipoulizwa na Jaji kama alimweleza huyo ndugu wa mshtakiwa kuwa anakwenda na ripoti nyingine alijibu hakumwambia, alipoulizwa huyo ndugu wa mshtakiwa alijuaje kama anakwenda na ripoti nyingine alijibu hajui.

 Endelea kufuatilia mitandao ya kijamii

Related Posts