Maafisa waandamizi wa Tanzania na Malawi wamekutana jijini Lilongwe, Malawi, katika kikao cha sita cha Tume ya Pamoja ya Kudumu ya Ushirikiano (JPCC), kujadili masuala ya kimkakati yanayolenga kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia, kijamii na kiuchumi kati ya mataifa hayo mawili.
Kikao hicho, kilichoongozwa na wenyeviti wenza, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wa Tanzania, Balozi Said Shaib Mussa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje wa Malawi, Balozi Mwayiwayo Polepole, ni hatua muhimu katika kufuatilia utekelezaji wa maazimio ya vikao vilivyopita na kuibua fursa mpya za ushirikiano.
Katika hotuba yake ya ufunguzi, Balozi Mussa alipongeza jitihada za pande zote mbili katika kudumisha ushirikiano wa muda mrefu na kusisitiza umuhimu wa ushirikiano wa kiuchumi, kijamii na kiusalama kwa maendeleo ya kikanda.
Vilevile, alisisitiza umuhimu wa kujadili kwa kina sekta muhimu zinazogusa maendeleo na ustawi wa Mataifa haya mawili na kikanda kwa ujumla. Maeneo hayo ameyataja kuwa ni pamoja na kuboresha mazingira ya ufanyaji wa biashara hasa za mipakani, uendelezaji wa miundombinu ya usafiri, ushirikiano katika sekta ya nishati na kuimarisha mwingiliano wa watu.
“Ni muhimu tushiriki majadiliano haya kwa mtazamo chanya na ari ya ushirikiano, kwani maendeleo ya kiuchumi, usalama wa kikanda, na ustawi wa jamii yanaweza kupatikana tu kupitia mshikamano wa kweli.” Alisema Balozi Mussa.
Kwa upande wake, Mwenyekiti Mwenza wa kikao hicho na Kiongozi wa Ujumbe wa Malawi, Balozi Polepole alisema kuwa kikao hicho kinatoa fursa adhimu ya kujadili masuala muhimu ya ushirikiano kwa manufaa ya pande zote mbili.
Pamoja na masuala mengine, kikao hicho kimeangazia nyanja za diplomasia na siasa, ulinzi na usalama, masuala ya uchumi, miundombinu na mawasiliano, pamoja na masuala ya kijamii na kibinadamu.
Kikao hichi ni maandalizi ya Mkutano wa Sita wa Tume ya Kudumu ya Ushirikiano kati ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Jamhuri ya Malawi ngazi ya Mawaziri, unaotarajiwa kufanyika Februari 26, 2025.