Hai. Mamia ya waombolezaji wamejitokeza katika Usharika wa Nkwarungo Machame, kushiriki ibada ya maziko ya Sifael Shuma (92) aliyekuwa mmoja wa vijana wanne walioshiriki tukio la kuchanganya udongo wa Tanganyika na Zanzibar Aprili 26, 1965.
Tukio hilo lilifanyika ikiwa ni mwaka mmoja baada ya kuasisiwa kwa muungano Aprili 26, 1964.
Sifael ambaye alifariki dunia Februari 20, 2025 katika Hospitali ya Mzena, Dar es Salaam, alipokuwa akipatiwa matibabu, anazikwa leo Jumatano, Februari 26, 2025 nyumbani kwake, Machame, Wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro.

Katika ibada ya mazishi inayofanyika usharika wa Nkwarungo, Dayosisi ya Kaskazini ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), ambayo inaongozwa na Mkuu wa Dayosisi hiyo, Askofu Fredrick Shoo, imehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali na kisiasa.
Kifo cha Sifael, kimefunga ukurasa wa vijana wanne, wawili kutoka Zanzibar na wawili kutoka Tanganyika, walioshiriki tukio la kuchanganya udongo, ikiwa ni ishara ya muungano wa nchi hizo mbili na kuzaliwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Vijana wengine walioshiriki tukio hilo ambao walishafariki ni Hassan Omar Mzee (76) na Khadija Abbas Rashid (74) wote kutoka Zanzibar na Hassaniel Mrema (80) na Sifael waliotoka Tanganyika.
Kwa mujibu wa historia Hassaniel Mrema na Hassan Omar Mzee ndio walioshiriki kushika chungu kilichowekwa udongo wa nchi hizo mbili, huku Khadija na Sifael wao wakibeba vibuyu vilivyokuwa na udongo wa nchi hizo.

Licha ya Sifael kufunga kumbukumbu bado wanne hao wataendelea kubaki kwenye historia ya vijana walioshiriki tukio la Aprili 26, 1965, kwenye uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Endelea kufuatilia Mwananchi kwa taarifa na habari mbalimbali